Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sumve
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na uzima, na kabla sijazungumza sana ili nisisahau, niseme kwamba, siungi mkono hii bajeti ili tukae sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nadhani kumbukumbu zinaonesha nimekuwa nikizungumza mara nyingi hapa, nikisisitiza kwamba mimi natoka Sumve, na Jimbo la Sumve halina hata milimita moja ya lami. Tunazungumza hapa watu wazima, Mawaziri wapo na Serikali inatuahidi, lakini haitekelezi. Sasa ni vizuri tugawane mbao kila mmoja aendelee na mambo yake kwa sababu wameamua kutukwamisha kwa makusudi; na kwa ujeuri nami ninatawakwamisha leo kwenye bajeti yao.
Mheshimiwa Spika, sitaiunga mkono bajeti hii, nitashika Shilingi mpaka! Najua hapa hawaendi kujenga wala nini, maana wameshaniahidi mara nyingi sana, lakini bora hata kama siwezi kuwapiga mkaumia, bora nioneshe nimekasirika.
Mheshimiwa Spika, sasa hizi hasira za watu wa Sumve dhidi ya hii dharau inayoendelea kwenye Wizara ya Ujenzi, nimetumwa kuja kuziwasilisha. Ni kwamba, kumbukumbu zinaonesha Wilaya ya Kwimba ipo Mkoa wa Mwanza, lakini ni wilaya pekee ambayo haijaungwa na mkoa kwa lami.
Mheshimiwa Spika, sio mimi niliyeanza kusema. Mwaka 1995, Rais Mkapa akiwa anaomba kura aliahidi atatuunga, haikufanyika. Mwaka 2005 Rais Dkt. Kikwete wakati anaomba kura aliahidi, haikufanyika. Mwaka 2015 Rais Dkt. Magufuli anaomba kura aliahidi, haikufanyika. Mwaka 2022 kwa sababu tuna uhaba wa ziara za viongozi wa Kitaifa, kwa sababu wakifika Mkoa wa Mwanza wanakwamishwa kwenda Kwimba kwa sababu hakuna barabara zinazoeleweka. Makamu wa Rais alipita akaelekeza Wizara iende ikaone, watengeneze barabara ile, hawajaenda.
Mheshimiwa Spika, sasa nafikiri nimeshagundua kwamba, sisi Mkoa wa Mwanza tuliwekwa kimakosa, kwa sababu haiwezekani sisi ndio hatujaunganishwa. Ukiangalia historia ya Mkoa wa Nyanza, Wilaya ya Kwimba ni kongwe katika wilaya za kwanza Maswa, Kwimba, Musoma, Geita, Bukoba, Shinyanga na Mwanza yenyewe zina lami kasoro sisi. Tumezaa Wilaya ya Misungwi, Busega, na Magu zina lami kasoro sisi.
Mheshimiwa Spika, sasa leo nimetumwa tuje tugawane mbao humu, maana haiwezekani tukaendelea kuwa tunafuatafuata tu hapa, tunawaunga mkono, mnatudanganya.
Mheshimiwa Waziri, uongo wa Wizara yako wameshiriki Mawaziri wengi sana humu sio wewe tu. Tumeanza na Mheshimiwa Mzee Eng. Dkt. Chamuriho pale akashiriki uongo, akaja Mheshimiwa Prof. Mbarawa akashiriki uongo, akaja kaka yangu Mheshimiwa Bashungwa akashiriki uongo, na wewe uko kwenye huo huo uongo kwa sababu kuna kilometa 10 feki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nafikiri tuliwahi kukutana na watumishi hewa. Sasa kuna kilometa kumi hewa Sumve, barabara hewa ambayo tunaambiwa imesainiwa haijawahi kujengwa hata hiyo greda kuliona hatujawahi. Tukiwaambia kwamba, lami hatuijui mtuelewe. Wengine mnazibandua, wengine hatuna.
Mheshimiwa Spika, yule mkandarasi yuko pale ni hewa. Naona Waziri hapo anamnong’oneza Mheshimiwa Eng. Kasekenya, yaani watakushirikisha tu huo uongo, hawajawahi kujenga, lakini hapa tunaambiwa wamesaini, wanaandika kwenye makaratasi. Sisi tutapita kwenye makaratasi? Yaani gari zetu zitapita kwenye haya makaratasi yenu ya bajeti? Si yanatakiwa yapite kwenye lami? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kilometa 73 hatujawahi kuona lami. Hatupiti sisi, au tuko Tanzania kimakosa! Haieleweki, yaani kila siku mnatudanganya hapa! Sasa nimeona bora niwaoneshe kwamba tumechukia, hatukubaliani na huu uongo, na sisi watu wa Sumve tunataka tukitokea Magu, tukiwa tunapita Ngudu mpaka Hungumalwa, tupite kwenye lami.
Mheshimiwa Spika, tukitokea Fulo, tupite Nyambiti twende mpaka Maswa kwa lami, lakini ninyi hamtaki, mmethibitisha hili kabisa bila shaka. Hatujaungwa Mkoa mzima wa Mwanza, na viongozi wa kitaifa hawaji kwetu kwa sababu hamna namna watakuja, tumeachiwa tukae na vumbi letu tuendelee na maisha yetu ya shida na ninyi mnatudanganya kila siku na bajeti siiungi mkono, nashukuru. (Makofi)