Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya, na wamefanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Ulega kwa kweli tumeona jinsi unavyochacharika kukimbia huku na huku na kuhakikisha kwamba, barabara zinakamilika. Pia, Naibu wako anafanya kazi nzuri sana, nawapongezeni sana na nina imani hata wananchi wenu watawarudisha tena katika nafasi hizi mnazoenda kugombea kwa kazi nzuri ambayo mmeifanya, hongera sana.
Mheshimiwa Spika, pia, niwapongeze watendaji wa taasisi zilizopo chini ya Wizara hii na hasa TBA, wanafanya vizuri sana lakini zaidi TANROADS wanafanya vizuri sana, wamejitahidi sana kujenga barabara pamoja na madeni makubwa ambayo yapo.
Mheshimiwa Waziri, hebu jitahidi sana kuongea na Wizara ya Fedha, watafute fedha tupunguze haya madeni ili TANROADS waendelee kujenga barabara na kuunganisha maeneo mbalimbali. Kazi ni nzuri, hongereni sana.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake wa kuamua kwamba, baada ya kuona Watanzania tunavyochacharika na tunavyohangaika kujenga nchi hii, aliona wanawake wako nyuma kiuchumi, akaamua kwamba, katika mojawapo ya barabara ambazo zinajengwa na TANROADS, basi itafutwe barabara moja wapewe wakandarasi wanawake ili wajenge.
Mheshimiwa Spika, kila mkandarasi apewe kilometa tano halafu wajijengee uwezo wa kiuchumi, lakini waondokane na umaskini. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, barabara iliyochaguliwa inaitwa njia Panda ya Iyula – Idiwili hadi Nyimbili kilomita 20, kwenye bajeti ya mwaka huu 2024/2025 ipo lakini mchakato wa manunuzi bado haujakamilika. Kumekuwa na changamoto za kukamilisha hiyo barabara.
Mheshimiwa Spika, sasa wale wanawake tuliwaahidi tukasema tutawajengea uwezo, tutawapa hizo barabara kila mtu kilomita tano mjenge. Wananchi kule wakaondoka kwenye maeneo wakapisha ile barabara ikamilike, lakini mpaka leo bado mchakato haujakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri Ulega, aangalie namna ya kukamilisha mchakato wa manunuzi, wakandarasi hawa wanawake wapewe hizo barabara waendelee kuzijenga ambazo zina manufaa makubwa sana katika uchumi wa eneo lile katika kusafirisha mazao na vitu vingine. Kwa hiyo, tunakushukuru sana kama hilo litakamilika.
Mheshimiwa Spika, pia namshukuru Mheshimiwa Waziri, TARURA wamejenga barabara kilomita 11 kutoka Vwawa kwenda Ndolezi. Palibakia kilomita 1.2 kwenye barabara ya TANROAD kufika kwenye kimondo chetu, naona amepeleka mkandarasi anajenga kile kipande, tunakushukuru sana. Kwa hiyo, ina maana sasa kimondo kile, barabara ikikamilika kitakuwa kimeongezewa thamani, tunashukuru sana kwa barabara ile.
Mheshimiwa Spika, tunaomba barabara ya kutoka Mahenge kuja hapo kwenye kimondo kwenda Hasamba – Nyimbili hadi Ileje kwa Naibu wake. Ile barabara ni muhimu sana katika maendeleo ya Mkoa wa Songwe. Ikikamilika itafungua njia, uchumi wa wananchi wa Ileje na wale wanaotoka Malawi na maeneo mengine watakatiza pale kuja mpaka Vwawa kuja Makao Makuu ya Mkoa na biashara zitaendelea vizuri sana. Kwa hiyo, hii barabara tunaona kwamba ni muhimu sana.
Mheshimiwa Spika, ipo Barabara ya Ihanda kwenda Ipunga hadi Chindi. Ile barabara itaunganisha Wilaya ya Momba, barabara hii nayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya uchumi wa Mkoa wa Songwe.
Mheshimiwa Spika, lipo eneo pale Iboya – Kata ya Ihanda. Eneo lile limetengwa kwa ajili ya kutengeneza check point ambapo eneo lilichukuliwa karibu miaka 10 sasa toka tunaimba. Wananchi wa eneo la Iboya wamekuwa kila wakati hawaendelezi lile eneo, wanasubiri fidia na kila mwaka tumeahidiwa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wananchi wanasikitika ni lini Serikali itawapa fidia wananchi wa Iboya ili ile check point ianze kujengwa tupunguze foleni iliyopo Tunduma? Hiyo ikikamilika, itasaidia sana kupunguza foleni ya pale Tunduma.
Mheshimiwa Waziri hebu lishughulikie hili suala wananchi wale wapewe fidia. Ni shilingi bilioni nne tu, na uhakika ukiongea vizuri na Wizara ya Fedha, wakalipwa, basi hali itakuwa ni nzuri na mambo yatakuwa mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naipongeza pia TANROADS kwa kujenga parking ya malori pale Chimbuya karibu na Mpemba, ambapo parking ile itasaidia sana kupunguza changamoto ya usafiri pale Tunduma, ambayo ni kitu muhimu sana.
Mheshimiwa Waziri, naunga mkono hoja endelea kuchapa kazi, Naibu wako na Watendaji wote chapeni kazi, maendeleo ya nchi hii yanawategemea sana. Ahsante sana. (Makofi)