Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hii Wizara ya Ujenzi. Nianze kwa kuwapa pole wananchi wa Jimbo la Hai kwa maafa ambayo yamejitokeza kwenye Jimbo letu la Hai. Naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu apokee taarifa kwamba kule Hai mvua zinazonyesha ni nyingi, miundombinu ya barabara imeharibika kweli kweli.
Mheshimiwa Spika, hivi ninavyozungumza, barabara ya kutoka kwa Mengi kwenda Kyalia haipitiki kabisa. Kwa hiyo, wananchi wanapata tabu. Barabara ya Makoa kwenda Mferejini kuna daraja pale Kikafu, kule watu wa Lyamungo hawawezi kwenda Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu atazame na hizi mvua zinaendelea kunyesha, zinanyesha kuanzia asubuhi mpaka jioni.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi ninavyozungumza, kule Weruweru pale Miembeni barabara imekatika, watoto hawajaenda shule leo. Karibu kama Kata nne watoto hawakuweza kufika shule. Namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hati ya dharura kabisa watusaidie michakato ya kutafuta fedha ianze mapema ili mvua zitakavyopungua tu hizi barabara ziweze kujengwa na watu wa Hai waweze kupata barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mara nyingi nimekuwa nikichangia hukuwepo kwenye Kiti, leo upo, nitumie nafasi hii pia kwa niaba ya wananchi na kwa niaba yangu binafsi, kukupongeza kwa kazi kubwa unayoifanya huko duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kweli unatuwakilisha vizuri sana. Niseme tu, huwa nakupenda na ninakufuatilia sana namna ambavyo unatuwakilisha vizuri. Inaonekana Watanzania na sisi tuna uwezo mkubwa, hongera sana. Nawaomba sana watu wa Mbeya, hiki kichwa hapa tunakihitaji hapa duniani na Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo niseme namshukuru Mheshimiwa Waziri, nimeona kwenye bajeti amenitendea haki. Alifanya ziara kwenye Mkoa wa Kilimanjaro na akaja Wilaya ya Hai, nampongeza ameanza vizuri pamoja na Naibu Waziri wake na watendaji wote, kwa kweli wanafanya kazi yao vizuri, ila kuna viporo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Daraja la Makoa limejengwa vizuri na TANROAD, lakini bado hawajamalizia na yule mkandarasi pale ameshalipwa, nimeambiwa hajamaliza ile kazi, lakini tayari wametangaza tenda ya daraja lile la Kikavu kutoka Kalali kwenda Uswaa mpaka sasa hivi mkandarasi hajaingia site. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kuna kiporo kingine ambacho yeye mwenyewe alitembelea pale. Barabara ya Moshi – Arusha kwenye lile Daraja la Kikavu wananchi kila siku wanaenda kufundishwa mafunzo ya kulipwa fidia ili wapishe mradi. Naomba waongeze speed walipe wananchi wa Masama Kusini ili eneo lile la kwa Sadara waachie ujenzi wa daraja na waanze kazi ya ujenzi wa barabara hii ya Moshi – Arusha.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine kwa Mheshimiwa Waziri wameweka kwenye mpango ujenzi wa barabara mbili, kupanua Barabara ya Moshi – Arusha, kuanzia Maili Sita kwenda Moshi Mjini. Naomba hebu waunganishe tufanye jambo likamilike pale Maili Sita ije mpaka Arusha. Mnaona sasa, hii baada ya Mheshimiwa Rais kutangaza Royal Tour, hii barabara imekuwa busy sana. Nawaomba mwongeze Mkandarasi, aliyeko site apewe hiyo kazi afike pale KIA kama itapendeza kwenda hadi Arusha sasa hilo ni jambo lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina barabara hapa ya Bomang’ombe – Cheki Maji – TPC, hii barabara tumeipitisha kwenye kikao cha barabara mkoa, kwamba ni Barabara ya Mkoa wa Kilimanjaro kwa sababu ndiyo barabara pekee inayochepusha kwenda Moshi Mjini. Najua barabara hii ni ya TARURA, tulishaomba barabara hii ipandishwe hadhi ili iwe ya TANROADS. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri hii barabara aiongezee fedha, pale tumepewa kilomita 3.5 ni ndogo mno kati ya kilomita 25 na sasa hivi likitokea matatizo pale Kikavu Chini hakuna sehemu ambayo tunaweza kupita na hii ni barabara ya Kitaifa maana inatuunganisha mkoa na mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waziri aliahidi yeye mwenyewe taa za barabarani. Kaka ehee, usiniangushe kwenye hili, ulilisema mwenyewe. Wanasema wako kwenye manunuzi tunataka tuone hizi barabara zetu pale kwa Sadala – Bomang’ombe, lakini na kile kipande Waziri anajua yaliyotokea pale kutoka Njia Panda - Machame kwenda Kyalia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haya yakifanyika, kwa kweli watakuwa wametusaidia sana. Nimeona wametuwekea kwenye bajeti ku-upgrade barabara ya Kwasadala kwenda Kware kilomita 15. Naomba Waziri asukume hili, ujenzi uanze kwenda, hiki Kiswahili cha kuwaambia wananchi kwamba tuko kwenye upembuzi yakinifu, nimeshasema sana…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA Haya, ahsante sana.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, nibadilishie msemo ili nikaseme, lami inaanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na ninaunga mkono bajeti hii. (Makofi)