Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Bajeti ya Wizara ya Ujenzi. Sera ambayo ipo chini ya Wizara hii ambayo Waziri anaisimamia ni kuziunganisha barabara zetu kati mkoa na mkoa kwa kiwango cha lami, na sera hii Waziri anapaswa kuisimamia, lakini wananchi tunapaswa tuione kwa vitendo.
Mheshimiwa Spika, imekuwa ni bahati mbaya sana sisi wananchi wa Wilaya ya Karatu hatujaiona hii, na siyo tu kuiona, pamoja na kwamba sera inaelekeza, lakini imekuwa ni ahadi ya viongozi. Tuna barabara kuu mbili muhimu ambayo ni Barabara ya Njia Panda – Mang’ola – Matala mpaka Lalago ambayo inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna barabara nyingine ya kutoka Karatu – Kilimapunda kwenda Mbulu. Hii ni barabara ambayo inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa Manyara. Ni barabara za muda mrefu. Tumesema hapa Bungeni na Wabunge waliopita wameongea, wametaka utekelezaji wa barabara hizi takribani miaka 10. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama haitoshi, mwaka 2005 Mheshimiwa Dkt. Kikwete wakati anakuja kuomba kura alitoa ahadi mpaka leo mmewadanganya, mmewahadaa wananchi wa Karatu, barabara hii haijawahi kufikiriwa kutengenezwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama haitoshi hii barabara ya kutoka Karatu kwenda Mbulu mwaka 2023 mkamleta mkandarasi, mkaja, mkasaini, mkasema barabara inaanza kwa kiwango cha lami. Mpaka ninapoongea sasa, kwa kweli hakuna chochote kilichofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, sasa atueleze kwa nini kwanza ametupiga sound muda mrefu kiasi hiki? Kwa nini ametudanganya? Kwa nini ameshindwa kusimamia sera yao wenyewe waliyojiwekea? Kwa nini wameshindwa kutekeleza ahadi za viongozi ambazo walizitoa kwa wananchi? Kwa nini wamewahadaa wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni vizuri tukapata haya majibu na kama hawawezi, watuambie kabisa kwamba hatuwezi na hatutajenga ili tujue kwamba sisi tupambane na hali yetu kwenye hizi barabara mbili ambazo tumezipigia kelele muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine tuna barabara ya kuelekea kwenye hospitali ya wilaya. Hospitali ya wilaya imejengwa vizuri ina kila kitu, lakini barabara ya kwenda pale takribani kilomita tatu mpaka nne ni mbovu na kipindi hiki cha masika hata ambulance ambayo inampeleka mgonjwa pale haiwezi kupita kama mvua zikiwa nyingi. Kuna daraja na mvua.
Mheshimiwa Spika, barabara hii pia tunaomba tupatiwe hizo kilomita kwa kiwango cha lami ili kile ambacho tumekijenga kule hospitali kutoa huduma kwa wananchi, kwa kweli wananchi waweze kupita kwa sababu uhakika wa barabara kupitika upo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine tuna barabara muhimu sana ambazo kwa sasa zinahudumiwa na TARURA, lakini wananchi wanaomba kwa uwezo wa TARURA kuhudumia zile barabara, haiwezekani. Tunaomba barabara hizi zitoke TARURA ziende kuhudumiwa na TANROADS na barabara hii ni barabara inayoanzia Rotia kwenda Mbulumbulu na nyingine inaanzia Manyara – Kibaoni kwenda Kata inaitwa Mbulumbulu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii barabara ikifika Mbulumbulu inaenda kuunganisha Wilaya ya Karatu na Wilaya ya Monduli kwa sababu ikifunguliwa wananchi pia wanaweza kutumia hiyo barabara kuelekea Wilaya ya Monduli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni muhimu sana hii barabara pia ikapandishwa hadhi kwenda kuhudumiwa na TANROADS ili basi wananchi waweze kupita barabara hiyo kwa kipindi chote. Kipindi hiki cha masika ni kibaya mno. Jana walikuwa na msiba, watu wametoka na maiti Dar es Salaam wameshindwa kupita kwenda kuzika, yaani wameshindwa kabisa. Kuna adha, kuna shida kubwa sana kwenye hii barabara Mheshimiwa Waziri tunaomba ombi hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama haitoshi, tuna barabara nyingine pia ambayo ni muhimu sana inapita Kata ya Endabash – Endamarariek – Endallah – Chemchem mpaka Manyara Kibaoni ambayo inaenda kuunga barabara hii kubwa ya kutoka Karatu kwenda Arusha. Tunaomba pia barabara hii itoke chini ya usimamizi wa TARURA iende kuhudumiwa na TANROADS ili iweze kuhudumiwa kwa viwango vinavyotakiwa na wananchi waweze kupata huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho, wananchi waliopisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Manyara mliwalipa fidia, lakini mliwaaidi mtawalipa riba ya fidia ambayo yalipaswa. Mpaka leo wananchi wale hawajalipwa, ni miaka karibia 30 mmeahidi, mmesema mmepokea, maombi yako Wizarani, sijui yameenda Wizara ya Fedha mpaka leo wananchi wanatamani kujua ni lini fidia hiyo italipwa kwa wananchi hawa ambao wamepisha upanuzi wa Uwanja wa Manyara – Kibaoni? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Ahsante. (Makofi)