Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa nami niweze kutoa mchango wangu kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini.
Mheshimiwa Spika, kuhusu bajeti hii muhimu ya ujenzi na nianze kwanza kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu kipenzi Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kuwatumikia Watanzania kwa uzalendo mkubwa na kwa upendo mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata juzi tarehe 1/5/2025 kujumuika na Wanasingida pamoja na Watanzania kwa ujumla katika kuadhimisha ile Siku ya Wafanyakazi, Wanasingida kwa kweli walifurahi sana kuwanaye siku ile na wewe nilikuona, hongera sana na karibu tena Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri sana na utendaji mzuri, pia ni msikivu Waziri wetu huyu wa Ujenzi pamoja na Naibu wake, kusema ukweli najivunia, kwa sababu mara kadhaa nimemfuata Mheshimiwa Waziri, hata juzi kabla ya bajeti tulinong’ona pale nje nikamwambia barabara yangu ile ya Ilongero isipoonekana patachimbika. Sasa kwa heshima kubwa sana nasimama hapa, nampongeza Waziri na Watendaji wake wote pamoja na Balozi Aisha, Katibu Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakumbuka miaka miwili 2023 mpaka 2024 iliyopita nilisimama hapa nikaongea mpaka na Kinyaturu kabisa. Sasa leo nakuja na mrejesho wa kusema Mwajefya, yaani ahsanteni sana kwa kuiona barabara ile ya Ilongero kutoka pale Singida Mjini – Igauri imeonekana kwamba sasa ujenzi utaanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimefurahi kuiona ile barabara kwenye kitabu cha bajeti sasa, kitu kikubwa hapa namwomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara ya Fedha, kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu wahakikishe ujenzi unaanza mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilipoona neno limeandikwa pale Singida – Igauri – Ilongero limeandikwa kwenye kitabu cha bajeti hata wananchi wenzangu pia nikawajulisha kule Ilongero. Maana yake wanaisubiri hii barabara kwa hamu sana kwa sababu ni barabara ya kimkakati, barabara ambayo ndiyo roho ya uchumi wao na maisha yao ya kila siku. Maana yake sasa hivi barabara ni mbaya sasa walivyoiona kwa kweli walifarijika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kikubwa tu ambacho wanakisisitiza, wanataka waone mitambo ikiwa barabarani pale inatengeneza ile barabara ili nao wa-enjoy angalau waonje matunda ya uhuru ambao wazee wetu walimwaga damu kwa ajili yetu.
Mheshimiwa Spika, hapa hapa pia namshukuru Meneja wetu wa TANROAD Mkoa wa Singida Eng. Singano kwa jinsi ambavyo anatupa ushirikiano na amekuwa msikivu wakati wote. Kila tukifika tunalia anatusikia japo ni mgeni, lakini ameonyesha kwamba ni mwamba, amekomaa, ni msikivu kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sasa nisisitize mara mbili, tatu. Leo nimesimama kwa ajili ya hii barabara, yaani jambo kubwa ni hii barabara nataka nione kazi ikianza kufanyika. Leo sitaki kutumia maneno ya ukali, nilishayatumia sana huko nyuma kuhusu hii barabara.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa leo imesikika, nitoe ombi tu kwamba kazi ianze, na ninatarajia kabla ya bajeti hii kuanza kutekelezwa huko, hapa sasa hivi kuanzia Mheshimiwa Waziri atakapokamilisha, nataka nione kule vumbi likianza kutimka kwenye site, kazi ikifanyika wananchi wanaisubiri barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kuwaambia Wanasingida Kaskazini tuwe na subira, tusisikilize redio mbao. Leo mmeona barabara yetu iko kwenye bajeti, nyie tu sasa hivi mwombeeni Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan afya njema na mumpe mitano tena ili wakati tunapiga kura huku na barabara inapitika. Nina imani kubwa na Rais wetu kwa kuwa ametusikia hata utekelezaji wake utafanyika ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapo hapo ipo ile barabara ya kutoka pale Ilongero inapoishia hii kuelekea Ngamu inakounganisha na kule Mkoa wa Manyara, nayo tuliambiwa itaanza kufanyiwa feasibility study. Naomba feasibility study ifanyike na yenyewe iwekwe lami. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, sitaki kukuudhi. Naunga mkono hoja, barabara ya Ilongero – Singida kazi ianze kufanyika. Ahsante sana. (Makofi)