Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami nichangie Wizara hii ya Ujenzi. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambazo ameendelea kuzifanya ndani ya Taifa letu hususan katika hii Sekta ya Ujenzi. Tumeona miradi yote mikubwa ambayo ilikuwa imeachwa, anaendelea kuipatia fedha kuweza kuhakikisha kwamba inakamilika. Hongera sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, kaka yetu Mheshimiwa Abdallah Ulega, Baba Tulia, kwa kupewa nafasi ya kuwa Waziri wa hii Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Waziri umepewa Wizara hii kubwa na ni nzito, lakini pia umezaa mtoto umempa jina la Spika wetu, Tulia Ackson. Hebu linda hadhi ya hilo jina, na hii Wizara yenyewe jinsi ilivyo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu, hapo awali hii Wizara alipewa Mheshimiwa Prof. Mbarawa. Mheshimiwa Prof. Mbarawa, wakati akiwa Waziri alituahidi sisi watu wa Manonga hususan Wilaya ya Igunga kutupa kilomita 10 za mwanzo kwenye barabara ya Choma – Ziba kwenda Nkinga mpaka pale Puge mwaka ule 2023/2024 wa bajeti na alisimama hapa mbele ya Mheshimiwa Spika. Akasema kwamba, nawapa watu wa Manonga kilomita 10 pamoja na Mheshimiwa Dkt. Kigwangala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baadaye Mheshimiwa Waziri akawa ameweza kuondoka, akaja Waziri mwingine anaitwa Mheshimiwa Bashungwa na yeye akasimama kwenye hiyo Wizara mwaka unaofuatia 2024/2025, tukamwambia barabara yetu tupe fedha. Yeye kwenye Wizara yake hiyo hiyo ya Ujenzi akasimama kwenye hili Bunge akatuahidi kwamba yeye atatupatia kilomita 10 kwenye hiyo barabara ya Choma – Ziba.

Mheshimiwa Spika, sisi tukajua sasa, maana yake 10 za Mheshimiwa Prof. Mbarawa, 10 za Mheshimiwa Bashungwa maana yake tunaenda kutengeneza kilometa 20 katika barabara yenye urefu wa kilometa 109.

Mheshimiwa Spika, namwona Mheshimiwa Waziri Bashungwa anatikisatikisa kichwa kwamba, haya zilikuwa ni kilometa 10 tu, lakini ndiyo barabara ile ina urefu wa kilometa 109. Sasa kama wewe unatupatia kilometa 10, halafu tena mkatupatia kilometa 10 mpaka tukamalize kilometa 109, itatumia miaka mingapi au bajeti hizi tutazipitisha ngapi humu Bungeni? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri mwaka huu kwenye bajeti yake kwenye hii ameisoma vizuri sana, mwanzo mpaka mwisho. Sasa, yeye amefuta kilometa 10 za Mheshimiwa Prof. Mbarawa, na kilometa 10 za Mheshimiwa Bashungwa, amefuta zote na hakuna kitu.

Sasa, Mheshimiwa Waziri nataka katika wind up yako hapa utuambie sisi watu wa Igunga, je, wewe utatupatia kilometa 10 au umefuta zote kwamba, umefuta za Mheshimiwa Prof. Mbarawa na Mheshimiwa Bashungwa, na wewe kazi hapo imesimama?

Mheshimiwa Waziri tunataka majibu utakapokuja ku-wind up hapa. Usisahau, vinginevyo tutashika shilingi hapa kwamba zile kilometa 109 za ujenzi wa barabara ya lami Choma – Ziba mpaka Puge kule kwa Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, unatupatia kilometa 10, kilometa 20 au zote kilometa 109? (Makofi)

Mheshimiwa Waziri utambue mmeshafanya usanifu, mmetangaza kazi na mmepata mkandarasi, mkatuambia sasa imebaki kazi ya kusaini. Sasa, kama kazi ya kusaini tulitegemea kwenye hii bajeti yako, utuambie fedha za utekelezaji wa barabara hiyo ni hizi hapa. Sasa, maana yake yule Mkandarasi mlikuwa mnazungumza naye kupatana bei, ina maana mmefuta au imekuwaje? Au zoezi hilo la kusaini limeishia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, huyu Mkandarasi ambaye mlikuwa mmempatia kazi na ambapo tuliambiwa sisi wananchi tutasaini mwezi wa kwanza, Mheshimiwa Waziri Mkuu akaja mwezi wa tatu pale Igunga na Manonga na pia akaenda kwa Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, akasema kazi iliyobakia ni kusaini, kazi ya ujenzi wa barabara ianze. Sasa, Mkandarasi anasubiri tusaini, leo ni miezi sita hatujasaini. Leo tunataka sijui tushike shilingi Mheshimiwa Waziri? Maana yake kwa utaratibu huu sisi wananchi hawawezi kutuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu anategemewa katika Taifa hili awaambie wananchi wa Manonga na awahakikishie watu wa Igunga, aende na Nzega akawahakikishie watu wa Nzega na Puge kwamba tunachonga barabara hii.

Mheshimiwa Spika, tunaiamini Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inafanya kazi, na fedha inatoa. Tunaomba na sisi tupate fedha. Najua Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba anatakiwa naye atupatie fedha, lakini mwisho ninapomalizia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele imeshagonga.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia. (Makofi)