Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru wewe binafsi kwa kunipatia nafasi. Pili, namshukuru sana Rais wetu, mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayofanya. Tatu, nawashukuru Mawaziri wote waliohudumu katika Wizara hii katika kipindi hiki cha miaka mitano. Kwa kweli katika kipindi chote hiki cha miaka mitano, Mawaziri wote waliopitia Wizara hii wamenipatia ushirikiano mkubwa sana na ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu la Mbagala, sina deni na Wizara hii. Barabara zangu zinazoshughulikiwa na Wizara hii ni barabara mbili; barabara inayotoka Kokoto kwenda Kongowe – Mwandege. Mheshimiwa Rais amelipa fidia ambayo ilikuwa shida yetu kubwa ya shilingi 16,800,000,000. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, isitoshe, barabara hii sasa ina Mkandarasi na ameshaweka camp ya kuanza kujenga. Tunatarajia muda wowote kuanzia sasa ujenzi utaanza. Pia, nawashukuru, nilikuwa muda mrefu naipigia kelele barabara ya kutoka Mbande - Kisewe mpaka Msongola. Barabara ile imepata Mkandarasi na anaendelea na kazi, lakini hapa ndiyo kwenye tatizo.

Mheshimiwa Spika, Mkandarasi yule sijui anataka tumfanye nini? Tunazo taarifa ameshapewa malipo yake, lakini kazi haziendelei, kwa nini? Leo hii amekwenda kutusababishia matatizo makubwa sana kwa watu wa Mtaa wa Kisewe. Maji yote ambayo yamekusanyika barabarani kutokana na kurundika vifusi yanatiririka sasa hivi kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri, utakumbuka umefanya ziara katika barabara ile na tulikubaliana mpaka mwezi wa Tatu barabara iwe imeisha. Hebu tuombe sana huyu Mkandarasi mzungumze naye, wengine tukianza kuzungumza hapa na tukianza kumwachia Mwenyezi Mungu mambo haya, huyu mkandarasi atakuja kupata matatizo maishani mwake.
Tunakuomba sana Mheshimiwa Waziri, unatufahamu sisi wengine karama yetu. Mwambie huyu Mkandarasi akasafishe vifusi vyake, aweke lami, amalize kazi. Wananchi wa Kisewe wanaathirika na ile barabara kwa sababu maji yote yanaenda katika mitaa ya watu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kumwomba Mheshimiwa Waziri, hebu afikirie hii barabara sasa inayotoka Rangi Tatu kuja mpaka Mbande. Barabara inayo lami, lakini barabara imezidiwa sana. Population ya Mbagala imekuwa kubwa mno. Kwa hiyo, tunahitaji barabra hii aiweke katika mchakato wa kuweza kuipanua na hatimaye iweze kuwa barabara ya njia nne au njia sita, ili mwendokasi sasa uweze kufika hadi Pugu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja ahsante. (Makofi)