Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. Nashukuru kwa kupata nafasi kuichangia hii Wizara yenye dhamana ya barabara zetu nchini. Kwanza, nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa miujiza aliyoifanya ndani ya Jimbo la Kibamba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapatie pongezi sana Wizara wakiongozwa na ndugu yangu Mheshimiwa Ulega, Naibu Waziri Mheshimiwa Kasekenya na hawa Watendaji Wakuu wa Wizara; Balozi Mhandisi Aysha Salum Amour na Naibu Katibu Mkuu ndugu yangu Charles Msonde. Ninawapongeza sana, watendaji hawa, wameisaidia Wizara kwa kiasi ambacho kila Mbunge hapa anaona aseme hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, niongelee maeneo ya mafanikio zaidi kwenye bajeti hii. Kwanza, niishukuru sana Serikali kwa kutuondolea ile foleni kubwa kwenye Barabara ya Kitaifa ya Kimara – Kibaha kilometa 19.2. Nataka niseme ukweli, sisi watu wa pembezoni mwa Dar es Salaam tulikuwa tunatumia hadi saa saba kutoka Kibamba kwenda Posta. Ikikukuta siku nyingine mnarudi kutoka ofisini mnafika saa nane za usiku. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kukamilisha hii barabara vizuri na tunamtarajia aje atuzindulie barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ziada ndani ya Jimbo; wananchi wengi wanajua na Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wanapita ndani ya Jimbo la Kibamba. Nataka niseme ukweli kabisa ndani ya sakafu ya moyo wangu, leo barabara zimetajwa kwenye bajeti hii, kitabu hiki ndani ya page ya 36 aya ya 107, maeneo haya katika vitabu vya nyuma huko hatujazoea kuviona. Leo hii inatajwa Barabara ya Goba – Matosa – Temboni kilometa sita, Goba Njia Nne kuelekea Matosa hadi Saranga ambapo ni Temboni kilometa sita, tayari kilometa moja, bado kilometa tano. Kitabu kinatuambia kazi inaendelea, lakini hapa ninalo ombi.

Mheshimiwa Spika, hii kilometa moja ni miaka mitatu sasa, hizi kilometa tano hatumwoni Mkandarasi kama anatamkwa. Hivi anakuja, haji? Nawaomba sana, mkandarasi aende amalizie hizi kilometa tano ambazo tunahitaji ziishe.

Mheshimiwa Spika, vilevile, ya pili Kibamba Shule – Mpiji Magohe. Tunashukuru sana, hii ni barabara kubwa, njia panda ya shule inaenda Mpiji Magohe inaelekea hadi Bunju, Barabara ya Kitaifa. Tayari ina zaidi ya kilometa saba na hata leo wakati natoka hii weekend nimewaacha wakandarasi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishukuru sana Serikali na lami ni nzuri ya kiwango cha Kimataifa. Kwa hiyo, niendelee kuwashukuru sana, lakini barabara ya tatu inatajwa kwenye vitabu hivi ni Barabara ya Mbezi - Msakuzi – Makabe Junction, tayari kilometa 8.36 ina urefu huo na tayari inaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami kwa hatua mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, ziada ni hii Barabara ya Kimara – Bonyokwa – Kinyerezi ilikuwa ni tatizo la muda mrefu pale Darajani. Mimi niheshimu sana na nishukuru sana Wabunge wenzangu wote; dada yangu Mheshimiwa Bonnah kule mwisho Kinyerezi na kaka yangu Mheshimiwa Profesa Kitila Alexander Mkumbo hapo katikati na mwanzo ninaanza mimi. Barabara hii sasa hivi imefikia 13% ina kilometa 6.73 na mkandarasi yupo site. Kwa hiyo, hizi ni pongezi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maombi yangu, ipo barabara inatamkwa humu ndani, Barabara ya Victoria Road. Viongozi wa Wizara mnaijua na ndiyo kilio changu kama Mbunge, kila mwaka ninaisema. Sasa hivi mliwahi kuitangaza mara mbili kilometa 9.55. Mara ya kwanza hawajatokea wakandarasi, hawajatosha, hawana sifa. Mara ya pili tena na sasa hivi mnazungumza mmeanza kilometa sita.

Mheshimiwa Spika, nataka nijue mkataba ulisainiwa lini na huyu mkandarasi anaingia lini? Hii barabara ni muhimu, ina wananchi zaidi ya 100,000. Barabara moja hii wanaita Mbezi Shule au Kwa Yusuph – Mpiji Magohe kilometa 9.55. Nawaomba sana Wizara kwa unyenyekevu mkubwa wampeleke mkandarasi aanze kazi kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni mafanikio makubwa sana ndani ya Jimbo la Kibamba. Hizi ni Barabara za TANROADS au Wakala wa Barabara Mijini. Hatujazungumza hayo mengine ya TARURA na DMDP huko, tumeshatoka kwenye Wizara nyingine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mafanikio ni makubwa ndani ya Wizara hii na Mheshimiwa Rais ameshafanya makubwa sana katika Jimbo letu la Kibamba. Mwisho, niwatakie kila la heri Wizara, kazi wanayoifanya ni nzuri lakini niwatakie heri kwa sababu tunafanya mapato na matumizi. Basi wayapate haya mapato tunayoyatarajia kwenye hii bajeti ya 2025/2026, ili kazi sasa tuliyoitarajia kama Taifa iweze kwenda kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, naiunga mkono hoja Wizara hii na ninamshukuru sana kwa nafasi. (Makofi)