Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbeya Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee naomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza vyema miaka minne kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii.
Mheshimiwa Spika, pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Nchimbi na kumtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Mbunge na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu, ikiwa ni pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo sekta ya nishati.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Naibu Spika na pia uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.
Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Abdallah Ulega, Mbunge na Waziri wa Ujenzi kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ushindani wa Kimataifa (National competitiveness). Bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi chake akiwa Waziri wa Ujenzi, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimamizi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno, kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi tisa ya bajeti inayoishia Aprili, 2025, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, imetekeleza miradi mingi ya miundombinu ya barabara, reli, bandari na uimarishaji wa safari za anga ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege.
Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa hatua nzuri za utekelezaji wa mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR pamoja na uboreshaji wa bandari utaimarisha kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi yetu. SGR na bandari ni nguzo imara ya kiushindani katika biashara ya usafirishaji wa ndani na nchi za Maziwa Makuu na hata za Kusini mwa Afrika na Kati. Bandari za Tanzania ni lango la usafirishaji kwa Zambia, Malawi, DR Congo, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan ya Kusini na hata Zimbabwe na Msumbiji.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha ujenzi wa SGR unaendelea kwa kasi ile ile na pia napongeza jitihada za kuendelea kutafuta vyanzo vya fedha vya masharti nafuu kugharamia ujenzi huo. Pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, Serikali imefanya maboresho makubwa ya miundombinu na huduma katika bandari zetu hususan Bandari ya Dar es Salaam ili kukabiliana na ushindani mkubwa wa bandari nyingine za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Mheshimiwa Spika, Bandari ya Dar es Salaam inakumbana na ushindani mkubwa kutoka bandari za Mombasa (Kenya), Beira (Msumbiji), Nacala (Msumbiji), Durban (Afrika Kusini), Lobito (Angola) na Walvis Bay (Namibia). Ujenzi wa SGR ya bandarini na maboresho mengine ya bandari zetu iendane na kuondoa changamoto nyingine ambazo zinasababisha gharama kubwa za usafirishaji kwa bandari zetu na kusababisha kupoteza biashara ya usafirishaji kwa bandari shindani.
Mheshimiwa Spika, ufanisi wa bandari unategemea pia maboresho ya barabara, reli ya kati (TRL), reli ya TAZARA, utendaji wenye tija wa wadau wote wa bandari na hata watumishi ili kupunguza gharama za usafirishaji kwa wateja wa bandari zetu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za mfumuko wa bei za mafuta na pembejeo, kuna fursa kubwa na hasa mahitaji makubwa ya mazao ya kilimo kwa soko la ndani na nje. Uzalishaji kwa tija unategemea kwa kiasi kikubwa ubora wa miundombinu ya barabara, reli na hata anga. Serikali iweke msukumo zaidi kwenye kuboresha miundombinu ya barabara kurahisisha usafirishaji wa pembejeo na mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na fursa za uzalishaji mkubwa kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, napendekeza mwendelezo wa uboreshaji wa barabara za Tanzam kipande cha Igawa - Tunduma; barabara ya bypass ya Uyole - Songwe; barabara ya bypass ya Iwambi - Mbalizi; barabara ya Mbalizi – Shigamba – Isongole kutokana na uzalishaji wa mazao ya kilimo; barabara ya Mbalizi – Galula – Makongosi kutokana na uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na madini; na pia barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete ambayo ni muhimu sana katika kusafirisha mazao ya kilimo ikiwemo maua, parachichi na viazi kwa soko la nje.
Mheshimiwa Spika, uboreshaji wa barabara hizi pamoja na Uwanja wa Ndege wa Songwe ni muhimu sana kwa usafirishaji wa mazao yetu kwa soko la ndani na nje, na kwa kiasi kikubwa utaongeza mapato ya fedha za kigeni. Maboresho ya Uwanja wa Ndege wa Songwe uende sambamba na ujenzi wa maghala mahususi ya maua, mbogamboga, parachichi, nyama, viwanda vya kuongeza thamani za mazao na madini na EPZ/Industrial Park.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ajali za mara kwa mara za Mlima Iwambi Mbalizi na msongamano wa magari yakiwemo malori ya mizigo na mafuta ya petroli, tunashukuru kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuchukua hatua za haraka kuanza ujenzi wa barabara ya njia nne kwa barabara ya Tanzam kipande cha Uyole mpaka Uwanja wa Ndege wa Songwe.
Mheshimiwa Spika, katika vipindi mbalimbali, viongozi wa Kitaifa waliagiza upanuzi wa kipande hiki cha Tanzam pamoja na ujenzi wa bypass ya Uyole – Songwe kilometa 40 na bypass ya Mbalizi – Iwambi kilometa 6.5.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara hizi utanusuru wananchi kuendelea kupoteza maisha kwa ajali za mara kwa mara katika eneo hilo. Hatari zaidi ni kwa magari makubwa yanayosafirisha mafuta kupita barabara yenye msongamano mkubwa katikati ya Jiji la Mbeya. Msongamano wa magari makubwa katika barabara ya Tanzam ni sehemu ya changamoto zinazopelekea bandari zetu kupoteza biashara kwa bandari shindani.
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi kirefu sasa, wananchi waliopisha ujenzi wa barabara ya bypass ya Uyole mpaka Songwe wamekuwa wakipewa ahadi ya malipo ya fidia, lakini mpaka leo hii hawajalipwa. Naishauri Serikali ichukue hatua za haraka kuwalipa madai ya fidia kabla ya kuanza utekelezaji wa bajeti ya ujenzi ya mwaka 2025/2026.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.