Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Samweli Xaday Hhayuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hanang'

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na kuendelea kuwawakilisha vizuri wananchi wa Hanang hapa Bungeni. Pia nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Hanang kwa kuendelea kuniunga mkono kwenye kazi zangu za kuwawakilisha Bungeni.

Mheshimiwa Spika, hii ni bajeti ya tano nikiisemea barabara ya Haydom kwenda Mogitu kilometa 68. Nashukuru sana kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umekamilika, kinachonishangaza kwenye bajeti hii ya mwaka 2025/2026 Waziri wa Ujenzi ameandika tu kuwa Serikali inaendelea kutafuta fedha wakati wananchi waliahidiwa ujenzi wa barabara. Rejea ukurasa wa 31 sehemu ya 93 ya hotuba yake.

Mheshimiwa Spika, mbaya zaidi ukurasa wa 192 wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi Kasma 4114 eneo la Mogitu - Haydom imetengewa kiasi cha shilingi milioni 500 kwa kilometa 68 wakati maeneo mengine ya barabara hii ya Serengeti bypass zimetengewa fedha nyingi mfano Mbulu - Garbabi kilometa 25 shilingi milioni 2,000, Labay - Haydom kilometa 25 shilingi milioni 2,000 na Nkoma - Lalago kilometa 65 shilingi milioni 2,500.

Mheshimiwa Spika, je, eneo lenye urefu wa kilometa 68 kutengewa fedha kidogo kiasi hiki, ni kwamba sehemu hii ambayo inagusa zaidi wananchi wa Hanang umuhimu wake ni mdogo na Wanahanang siyo muhimu kama wananchi wa maeneo mengine?

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni ujenzi wa barabara ya Nangwa - Gisambalang hadi Kondoa kwa kiwango cha lami ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo ina daraja lililokatika, daraja la Munguri toka mwaka 2019 na hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Spika, naomba Waziri awaeleze wananchi wa Hanang na Kondoa kuwa je, lini kwanza, Daraja la Munguri ambalo linategemewa kwa shughuli za kiuchumi na kijami na wananchi wa Hanang hasa Kata za Nangwa, Wareta, Dirma, Sirop, Simbay, Lalaji, Balangdalalu na Gisambalang wanazozitegemea upande wa Mkoa wa Dodoma ambao ni makao makuu ya nchi itajengwa?

Pili, ujenzi wa Barabara ya Nangwa – Gisambalang - Kondoa utaanza. Jambo la tatu, Barabara ya Arusha -Singida hasa eneo la Dareda mpaka Gehendu ambayo ipo Wilayani Hanang imekuwa mashimo matupu. Naomba ukarabati wa haraka ukafanyike ili kuondoa kero na adha wanazopata watumiaji wa barabara hii hasa Wanahanang.

Mheshimiwa Spika, kazi ya ukarabati wa barabara hii ufanyike kwa dharura, kwani kwenye bajeti ya mwaka 2024/2025 ilishatengewa fedha za kurekebisha kilometa sita.

Mheshimiwa Spika, nawasilisha.