Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Abdallah Ulega na Naibu wake Mheshimiwa Mhandisi Godfrey Kasekenya, watendaji wote walio chini ya Wizara hii kwa kazi kubwa wanazofanya kwenye kutengeneza mitandao ya barabara na madaraja maeneo mbalimbali nchini. Kipekee naipongeza TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro wakiongozwa na Mhandisi Palimaka Mota kwa ushirikiano wao mkubwa na Mbunge.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utahusu changamoto za barabara zinazojengwa na TANROADS katika jimbo langu la Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Moshi Vijijini liko katika maeneo ambayo wananchi wengi wanajishughulisha na shughuli za kilimo cha kahawa, ndizi, pamoja na mboga mboga na matunda ya aina mbalimbali. Vilevile wanajishughulisha na ufugaji pamoja na biashara na miji mbalimbali, ukiwemo Mji wa Moshi.
Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha shughuli za wananchi wa jimbo langu, uwepo wa barabara zinazopitika muda wote ni jambo muhimu sana. Ni kwa mantiki hiyo, naiomba Serikali itekeleze ahadi yake ya ujenzi wa barabara zinazojengwa na TANROADS ili ziweze kupitika kipindi chote cha mwaka na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wana Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kibosho Shine - Kwa Raphael - International School iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi toka mwaka 2005 na inajengwa na TANROADS, ila haijakamilika. Mkataba uliopo sasa hivi unaonesha kwamba ujenzi wa barabara hii unatakiwa kukamilika mwezi Novemba, 2025.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali itenge fedha za kutosha na kukamilisha ujenzi wa barabara hii kwani umechukua zaidi ya miaka 14.
Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali kwa kuanza ujenzi wa barabara ya Kiboriloni - Tsuduni - Kidia kwa kiwango cha lami. Barabara hii inajengwa na TANROADS na bado haijakamilika. Bado kuna malalamiko kutoka kwa wananchi wanaoitumia hii barabara kwamba kasi ya ujenzi ni ndogo na mkandarasi hajaonekana site kwa muda mrefu, ujenzi umelegalega.
Mheshimiwa Spika, kuna sehemu mbaya sana kwenye barabara hii na wananchi wanailaumu sana Serikali. Naiomba Serikali itenge kiasi cha fedha za kutosha na kukamilisha ujenzi wa barabara ya Kiboriloni - Kikarara - Tsuduni - Kidia kwa kiwango cha lami, kwani wananchi wanalalamika sana.
Mheshimiwa Spika, barabara hii ni ya kimkakati, kwani itatumika kuwasafirisha watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro kupitia lango la Kidia ambalo linatumiwa na watu mashuhuri (VIP). Barabara hii imetengewa shilingi milioni 900 katika bajeti ya mwaka 2025/2026 kufanya marekebisho ili iweze kupitika. Naiomba Serikali itenge kiasi cha fedha za kutosha na kukamilisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Rau - Uru - Shimbwe yenye urefu wa zaidi ya kilometa 13 ilikuwa kwenye ahadi za viongozi wa Kitaifa kujengwa kwa kiwango cha lami. Ujenzi wa barabara hii umeanza kwa kasi ndogo sana.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto ya ujenzi wa barabara hii kutokana na kupangiwa bajeti finyu kila mwaka. Ubovu wa barabara hii unasababishia usumbufu na gharama kubwa za usafiri kwa wananchi wanaoishi huko milimani.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali itenge fedha za kutosha na kukamilisha ujenzi wa barabara ya Rau - Uru - Shimbwe kama wananchi walivyoahidiwa na viongozi wakuu wa Serikali kwa nyakati tofauti, kwani ahadi ni deni.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Uru - Kishumundu - Materuni inajengwa kwa kiwango cha lami. TANROADS inajenga barabara hii kwa niaba ya TARURA. Kero kubwa ni kwamba kasi ya ujenzi ni ndogo sana.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali itenge fedha za kutosha na kukamilisha ujenzi wa barabara ya Uru - Kishumundu - Materuni kwani ina mchango mkubwa kupeleka watalii Materuni Water Falls.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Moshi Vijijini, barabara ya Kwa Rafaeli - Mto Sere inaunganisha Wilaya ya Moshi na ya Hai. Barabara hii inahudumiwa na TANROADS ambapo wameshaweka mitaro katika baadhi ya maeneo na haijajengwa hata kidogo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, barabara hii ni muhimu kwani ni sehemu ya kusafirisha watalii wanaokwenda kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia njia na mlango wa Umbwe.
Mheshimiwa Spika, pamoja na maagizo ya Waziri kwa TANROADS kuhusu kuzingatia ubora na viwango vya barabara wanazozijenga, ombi langu kwake ni kwamba asiishie kutoa maagizo tu, bali aje site mwenyewe katika Jimbo la Moshi Vijijini ajionee kazi zinavyotekelezwa na kutoa maelekezo.
Mheshimiwa Spika, baada ya ushauri niliotoa hapo juu, naunga mkono hoja.