Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anazoendelea kuzifanya katika nchi hii. Pia, namshukuru kwa kuendelea kuniamini katika nafasi hii ya Unaibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi. Pia, niendelee kumshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nikushukuru wewe mwenyewe, Naibu Spika, pamoja na Wenyeviti kwa jinsi ambavyo mmekuwa mnaliendesha hili Bunge kwa umaridadi na kwa kweli kwa hali ambayo ni ya Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, pia, niishukuru sana Kamati ya Miundombinu chini ya Mheshimiwa Selemani Kakoso, Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Anne Kilango Malecela pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Miundombinu kwa jinsi ambavyo wamekuwa wanatoa maelekezo na kutoa ushauri kwa Wizara.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge siyo tu kwa kuchangia hoja, lakini kwa jinsi ambavyo mmekuwa mnatoa ushauri kila inapobidi lakini sana sana kwa hoja mbalimbali ambazo mmezitoa leo wakati tukiwa tunajadili hii bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Ileje kwa ushirikiano mkubwa ambao wananipatia bila kuisahau familia yangu pia kwa ushirikiano mkubwa wanaonipatia na kunipatia huu utulivu ambao ninao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nitakuwa na mambo machache na ninaamini Mheshimiwa Waziri ataongea zaidi, lakini mimi nitajikita zaidi kuelezea yale mambo ambayo tumeyafanya katika kipindi hiki na yale machache ambayo tunategemea kuyafanya. Kwa sababu ya michango mingi, sitataja majina lakini pia itakuwa ni vigumu sana kugusa kila Mbunge alichochangia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwamba tunaamini moja ya kipimo cha maendeleo yoyote ya nchi pia ni miundombinu ikiwemo barabara. Pia, tunaamini ukiwa na barabara bora maana yake unapunguza gharama, muda, unachochea uchumi, unarahisisha kusafirisha, pia unafanya watu waweze kuwasiliana, na unaimarisha pia huduma mbalimbali za kijamii. Pia, unakuwa na uwezo wa kuunganisha eneo na eneo ikiwa ni pamoja na kusafirisha bidhaa kutoka eneo moja kwenda lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara ya Ujenzi, Ilani ya Chama cha Mapinduzi pia ni sera kwamba tuna wajibu mkubwa wa kuunganisha mikoa na mikoa, miji na miji, na pia kuunganisha nchi na nchi. Sasa, ni kuunganisha Makao Makuu ya Wilaya na Makao Makuu ya Mikoa yetu.

Mheshimiwa Spika, pia, tunahangaika sana na barabara zile za kimkakati ambazo tuna hakika tukizijenga zitainua uchumi bila kusahau barabara za mipakani na barabara za ulinzi. Kwa sababu hiyo, ndiyo maana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, moja ya eneo ambalo amelitilia mkazo sana ni kuhakikisha kwamba anaifungua nchi na kuiunganisha nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaona katika kipindi hiki tumeweza kuunganisha Tanzania na Malawi kupitia Mpemba kwenda Isongole. Sasa hivi tunajenga barabara ya kutoka Mpanda kwenda Kalemie ikiwa ni kuunganisha na DRC. Pia, tunajenga barabara ya kutoka Sumbawanga – Matai kwenda Kasesya kuunganisha na Zambia. Pia, sasa hivi tunafanya ukarabati mkubwa sana wa barabara ET3 ambayo ni ya kutoka Lusahunga kwenda Rusumo ambayo ilkuwa imekufa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lazima niwahakikishie wananchi wa Tanzania na Waheshimiwa Wabunge kwamba, kama Wizara kazi hiyo tunaendelea kuifanya na tunaifanya kwa umakini mkubwa sana. Waheshimiwa Wabunge, wameongelea matatizo mbalimbali kuhusu barabara zao, lakini nataka niwaambie kwamba katika kipindi hiki cha awamu hii tuna barabara nyingi sana ambazo tumezijenga na kwa sababu ukishapata, basi hiyo inakuwa siyo ajenda, ajenda ni kitu ambacho unakihitaji.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi watu hatuongelei tu kupitika kwa barabara, maana yake ni ya lami. Zipo barabara ambazo tumezikamilisha katika kipindi hiki ama tunaendelea kuzijenga. Tuna barabara ya Mnivata – Tandahimba kwenda Masasi ipo inajengwa kilometa 160.

Mheshimiwa Spika, tumekamilisha barabara ya Mbinga kwenda Mbamba Bay katika kipindi hiki ambayo pia inaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Ziwa Nyasa kwenda Malawi. Tumejenga Lusitu – Mawengi, barabara ya zege. Tumejenga Tabora – Koga – Mpanda moja ya barabara ya mfano kabisa kilometa zaidi ya 350. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumejenga Kaliua – Nguruka ikiwa ni pamoja na kuunganisha na Mkoa wa Kigoma, lakini sasa hivi tunakamilisha kipande cha Malagarasi – Uvinza ili tuunganishe 100% kwenda Kigoma. Tumekamilisha Vikonge – Luhafwe kule Mpanda. Sasa hivi kutoka Kigoma hadi Mwanza unatembea kwa lami kilometa 260 ambazo tunazikamilisha na kwa sasa unatembea kwenye lami katika kipindi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, tumekamilisha barabara ya kuunganisha na Daraja la Kitengule ikiwa ni pamoja na Daraja la Kitengule. Tumejenga Barabara ya Chaya – Nyahua, kwa hiyo, kutoka Manyoni kwenda Tabora zile kilometa ambazo zilikuwepo pale sasa hivi vumbi tumeshaliondoa katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Spika, Makutano Sanzate tumejenga. Pia tumejenga Barabara ya Nyamuswa – Bunda – Bulamba katika kipindi hiki. Waso – Sare tumekamilisha, Dumila – Kilosa tumekamilisha, Kidatu – Ifakara tumekamilisha, list ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kazi zimefanyika nyingi hatuwezi tukataja zote. Pia kwa sababu tunajua ili ufanye biashara na shughuli za kijamii hasa kwenye miji lazima upunguze msongamano. Katika miji hasa, nianze na Mji huu wa Dodoma, tunapoongea sasa hivi outer ring road yenye kilometa 112.3 ipo 84%, zaidi ya kilometa 70 au 75 zimeshawekwa lami. Itakuwa ni barabara ya aina yake ambayo tunategemea ifikapo mwezi Agosti, itakuwa imekamilika.

Mheshimiwa Spika, hii ni barabara ambayo itakuwa na taa kote kilometa 112 pia itapandwa miti barabara yote na upana wake ni zaidi ya mita 150, ambapo kutakuwa na maeneo mengi sana ya kufanya shughuli mbalimbali za kibiashara.

Mheshimiwa Spika, kutoka katikati ya Mji ambapo sasa hivi tupo kwenye manunuzi, kutoka katikati ya Mji kutakuwa na njia nne ambazo zinaunga barabara ya kwenda Iringa, barabara ya kwenda Arusha, barabara ya kwenda Dar es Salaam na barabara ya kwenda Singida. Hiyo ni mipango ambayo tunaifanya ili Dodoma hii kusijekutokea changamoto.

Mheshimiwa Spika, unapokwenda Jiji la Mbeya tunaendelea na ujenzi wa njia nne kutoka Nsalaga – Ifisi – Airport, Mkandarasi yuko site. Barabara ile imeelemewa, nguvu kubwa ya Wizara sasa hivi ni kuhakikisha kwamba tunaifungua.

Mheshimiwa Spika, unaposikia changamoto ya Tunduma mabasi, Mbeya inawezekana ikawa ni mara mbili kwa sababu unaweza ukatumia zaidi ya saa mbili. Kwa kweli nguvu zote tumeweka kuhakikisha kwamba zile barabara zinakamilika ili kupunguza changamoto ya usafiri pale Mbeya.

Mheshimiwa Spika, Dar es Salaam tunaendelea na BRT, BRT one na two zimekamilika, three iko mwishoni, four inajengwa, na five ambayo inaanza Ubungo – Buguruni hadi Kurasini; pia Matumbi – Tabata Dampo – Kigogo, Matumbi – Kinyerezi, upande wa Kinyerezi; lakini nyuma hapa Segerea, ziko kwenye hatua za manunuzi. Zote hizo ni kazi kubwa ambazo Mheshimiwa Rais anataka kufungua, kuunganisha na kurahisisha shughuli za kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukienda Jiji la Mwanza, tunavyoongea tuko kwenye hatua za manunuzi kuhakikisha kwamba tunajenga barabara ya njia nne kutoka Mwanza katikati – Mkuyuni – Nyegezi – Mkolani – Buhongwa – Nyashishi – Usagara, itakuwa ni njia nne ambazo hizo zitakuja kuunganisha sasa na Daraja la Kigongo – Busisi, maarufu kama Daraja la Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Daraja la Kigongo – Busisi ama JPM ninadhani limeelezewa na watu wengi na Waziri atalielezea lakini ni daraja la aina yake kama walivyoliongelea, nasi tukiwa kama sehemu ya mafanikio hayo tuna kila sababu ya kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye wakati anapokea hiyo kazi lilikuwa siyo zaidi ya 25%. Tunavyoongea sasa hivi, anasubiriwa yeye akalifugue hilo daraja. Ni kazi ambayo katika Afrika Mashariki na Kati haipo, kwa hiyo ni kati ya vitu ambavyo Watanzania tunasema tunayo miradi ya kielelezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nigusie suala la viwanja vya ndege. Tunajenga kiwanja cha ndege kikubwa sana cha Msalato, ambacho wanasema ni State of the Art. Kitakuwa kama viwanja vyovyote. Plan yake ni kwamba, kadri mji utakavyokuwa unapanuka, wameweka utaratibu kwamba design itakuwa kila Mji unavyopanuka na mahitaji yanaongezeka, ule uwanja utakuwa unaongezeka kadri mahitaji yanavyoongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunavyoongea sasa hivi tuko zaidi ya 85% kwenye runway, 55% kwenye hizi facility nyingine za viwanja. Ule uwanja utaunganishwa na barabara ambayo itatoka Airport Msalato – Ofisi za Mtumba – Chamwino Ikulu. Kwa maana kwamba hakutakuwa tena na sababu ya foleni pale ambapo viongozi wanaokwenda Chamwino Ikulu ama Mtumba kuingiliana na barabara nyingine hizi. Kwa hiyo, unaweza ukaona hiyo mipango ambayo ni mipango ya kisasa kabisa tunayokwenda kuifanya.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kwenye viwanja vya ndege, Uwanja wa Ndege wa Mbeya umekamilika, uwanja ambao sasa hivi ni maarufu sana. Uwanja wa Songea umekamilika, Uwanja wa Mtwara na hivi vimekamilika katika kipindi hiki. Uwanja wa Mtwara umekamilika, tunajenga uwanja wa Sumbawanga, tunajenga Uwanja wa Tabora, tunajenga Uwanja wa Shinyanga, tunajenga Uwanja wa Musoma, na sasa hivi tunahamia Lake Manyara na Tanga. Mheshimiwa Waziri ataelezea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, Wizara tumejipanga na tunategemea kwamba yale yote ambayo tumeahidi kwenye bajeti tutayatekeleza. Yale ambayo tutashindwa kuyajibu kwa mdomo, basi mtegemee kwamba tutawaletea kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga hoja. Ahsante sana. (Makofi)