Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema na Mwingi wa Ukarimu.

Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru pia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kwangu na kwa timu yangu yote ambayo amenikabidhi nishirikiane nayo katika Wizara ya Ujenzi katika kulijenga Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, pia, naiomba nikushukuru wewe, Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge na Kamati yetu ya Bunge kwa namna ambavyo mmekuwa mkitushauri na kutusimamia kwenye utekelezaji wa kazi mbalimbali za ujenzi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, pia, naomba nitumie fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa mdomo na wale ambao wamechangia kwa maandishi. Jumla ya Wabunge 81 wamechangia hoja yetu. Ahsanteni sana kwa namna ambavyo mmetupa changamoto kubwa sana, na mmetushukuru mkatupongeza, vilevile mmetupa ushauri mbalimbali wa namna ya kuyaendea mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishatangulia kusema, hoja ni nyingi sana za Waheshimiwa Wabunge na ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri Engineer Godfrey Kasekenya Msongwe kwa namna ya utangulizi aliyoanza nayo. Amesema vema kwamba, wale ambao tutakuwa tumewajibu hapa na wale ambao hawatakuwa wameyasikia majina yao wajue tu hoja zao tutazijibu zote hata kwa maandishi. Kwa hiyo, tutahakikisha kila hoja ya kila Mbunge iliyozungumzwa katika Bunge hili tunaipa uzito wake unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mazungumzo yaliyopita leo na jana hapa Bungeni, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia pia juu ya kuomba kupandishwa hadhi kwa barabara. Hapa wapo Wabunge wengi waliosema, lakini naomba niwataje wachache na niwaelekeze wataalam wangu na kwa sababu utaratibu wa upandishaji hadhi barabara unajumuisha kufanya tathmini na ipo Kamati ya Kiserikali ambayo yenyewe hushughulika na kuangalia vile vigezo.

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, nawaagiza wataalam wangu hapa ya kwamba wazichukue hizi barabara zote zilizosemwa na Waheshimiwa Wabunge hapa ndani. Mfano barabara zimesemwa kuanzia jana na Mheshimiwa Njalu Silanga, Mbunge wa Itilima, Mheshimiwa Edwin Swalle, Mheshimwia Emmanuel Cherehani Mbunge wa Ushetu, Mheshimiwa Boniventura Kiswaga wa Magu, Mheshimiwa Flatei Massay, Mheshimiwa Phillipo Mulugo na Mheshimiwa Dkt. Ritta E. Kabati.

Mheshimiwa Spika, wote hawa katika jumla ya Waheshimiwa Wabunge waliosema juu ya barabara katika maeneo mbalimbali nchini, Ninataka niwahakikishie, tunakwenda kulifanyia kazi jambo hili na tutayapata majibu ikiwezekana kabla Bunge hili halijafika mwisho wake. Nina imani kwamba tutakuwa tumepata majawabu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baadhi ya Wabunge pia wamezungumzia juu ya jambo linalohusu advance payments (malipo ya awali) kwa wakandarasi. Hapa wako wa namna mbili, wako wakandarasi wamelipwa fedha, lakini hazijafika kiwango cha 15% na wako wakandarasi hawajalipwa kabisa. Naomba nitoe mfano wa baadhi ya maeneo na ninaomba, katika kesi hii wako Wabunge wawili ambao wameniambia kuwa watashika Shilingi. Nawaomba kwa heshima kubwa na taadhima wasishike Shilingi.

Mheshimiwa Spika, rafiki yangu Comrade Mheshimiwa Kunambi, Mbunge wa Mlimba, yeye anazungumzia barabara ya kutoka Ifakara – Chita – Mlimba – Madeke, kwa sababu barabara hii, mmoja katika wakandarasi amelipwa kiwango, lakini hakijafika kile ambacho anapaswa kulipwa cha advance payment, na mwingine hajalipwa kabisa. Kwa hiyo, hakuna kinachoendelea katika eneo lile, shughuli zote zimesimama.

Mheshimiwa Spika, vilevile amezungumzia juu ya mambo yanayoendelea, ukweli ni kwamba eneo la Morogoro hasa Wilaya ya Malinyi ambako jana Mheshimiwa Antipas alichangia, Ifakara na Ulanga ni maeneo ambao yamepigika sana hasa na hizi mvua.

Mheshimiwa Spika, namhakikishia tu Mheshimiwa Kunambi, eneo la Mpanga ambalo umetolea mfano wa msiba uliotokea pale ni kwamba hizi tunavyozungumza tayari wataalam wetu wamerejesha mawasilino. Tayari tumejenga eneo lile la dharura, tumeweka ma-culvert 15 ya chuma ambayo yatatosheleza kupitisha maji, tayari tumeshatengeneza tuta na kwa hiyo, sasa hivi watu wanaweza kupita.

Mheshimiwa Spika, mpango wa kuendelea pale ni kwamba tunajenga box culverts ambazo zina jumla ya midomo sita. Kwa hiyo, tatu mara mbili tutakuwa tumejenga pale na itatosheleza kwa study tuliyoifanya na tunaifanya hiyo mara tu baada ya kutokushika shilingi na kuturuhusu bajeti hii ipite na tunakwenda kuifanya hiyo kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana na hili suala la Ifakara – Chita – Mlimba – Madeke, miongoni mwa fedha zitakazopatikana za advance payment, tumeshaandika barua tumeipeleka upande wa wenzetu wa Wizara ya Fedha nao wanatupa ushirikiano mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni imani yangu hapa Mlimba kwa maana ya Ifakara – Chita, vilevile na barabara ya kutoka Bigwa – Kisaki kule ambako Mheshimiwa Tale na Mheshimiwa Innocent Kalogeris wamepazungumza kwa uzito sana ndani ya Mkoa wa Morogoro na zenyewe tunakwenda kuzipa kipaumbele haraka sana baara ya kuwa tumeipata fedha ya advance payment. Tutakwenda kuwaondolea shida hii.

Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie kwamba tuliposema juu ya kwamba bajeti hii ni bajeti ya kazi na utu, ni kwa sababu tunatazama zaidi namna ya kutatua kero na changamoto hasa zinazowakabili wananchi.

Mheshimiwa Spika, pia naomba vilevile niwape hongera sana na pongezi Waheshimiwa Wabunge hawa kwa sababu ya namna ambavyo wamekuwa wakiziwasilisha hizi hoja na namna ambavyo wamekuwa wakizisimamia, kwa kusema ukweli wakati wote hawapungui katika jambo hili, wakipiga simu, wakiandika message, ama wakisema humu Bungeni. Hongereni sana kwa kuwawakilisha vema wananchi katika Majimbo yetu kote nchini.

Mheshimiwa Spika, vilevile wapo ambao wamezungumzia juu ya taa za barabarani, Wabunge wengi sana wameonesha kwamba jambo hili ni jambo muhimu na wamelipa kipaumbele sana. Nimeshakueleza katika bajeti kwamba, jumla ya taa 5,200 tunakwenda kuzinunua, ni wastani wa taa 200 kwa kila Mkoa.

Mheshimiwa Spika, wako hapa Wabunge ambao wamesema, mfano mtani wangu mmoja Mbunge wa Mbogwe, Mheshimiwa Maganga, anasema hana cha kunishukuru kwa sababu hajapata jambo. Nataka nimhakikishie kwamba atapata taa hizi 200 na zitakwenda kumulika pale Mbogwe ili kusudi yale mambo mbalimbali ya kuweza kufanya biashara katika maeneo yale yapatikane.

Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa Massare wa pale Itigi ameomba hizi taa, tutazingatia. Mheshimiwa Olelekaita, yuko Mama Sitta, Mheshimiwa Kyombo, Mheshimiwa Cherehani, vilevile yuko na Mheshimiwa Saashisha wa pale Hai, wote hawa wameomba taa. Nataka niwahakikishie kwamba tunayo maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, taa zinaleta nuru na taa zinapunguza ajali vilevile, na taa zinapendezesha sana miji yetu. Kwa hiyo, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, tutalifanya hili jambo mapema ili kusudi kama alivyosema Mheshimiwa Maganga, kabla ya mwezi wa 10 wakati tunaingia kwenye iyena iyena mambo yawe yameshapendeza ili kusudi tuendelee kuaminiwa na kupata kura za kutosha kutoka kwa wananchi wetu, vilevile kupeleka maendeleo kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge kadhaa wamezungumza juu ya barabara ya Chalinze – Segera. Ni kweli barabara hii ilijengwa miaka ya 1990. Wabunge kadhaa wa Mkoa wa Tanga wamezungumza, Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo na Katibu wa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi humu Bungeni, huyu amezungumza kwa mapana sana juu ya barabara hii, na ni kweli barabara hii ni finyu.

Mheshimiwa Spika, yuko Mheshimiwa Mnzava, vilevile Mheshimiwa Omari Kigua, Mheshimiwa Ummy, Mheshimiwa Eng. Mwanaisha Ulenge, yeye aliendelea na akaongeza na ile bypass ya Kiomoni kwa maana ya pale Mkinga – Mlingano. Hii ninataka nimhakikishie tumeshafanya Usanifu wa Kina na baada ya kuwa tumekamilisha Usanifu wa Kina tunaipeleka sasa iweze kuwa ni katika barabara mbadala. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi maana jana alizugumza kwa hisia kubwa ya kwamba ni kwa nini barabara hii haipewi kipaumbele? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa wote niliowataja juu ya barabara hii ya Chalinze – Segera, sasa hivi tunakamilisha detail design, tumekamilisha hatua ya kwanza, tunataka tupate usanifu wa kina wa hii barabara. Ni kweli ni finyu, imejengwa miaka mingi, sasa hivi haikidhi tena haja, kwa hiyo tukimaliza usanifu wa kina, hatua inayofuata tunaitafutia fedha ya uhakika ili kusudi barabara hii iweze kutanuliwa. Hii ni barabara kubwa ni barabara ya kiuchumi nami nimekubaliana nanyi na sisi tunakwenda kuipa kipaumbele pia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine lililochukua nafasi kubwa sana humu ndani, pamoja na pongezi nyingi ambazo Waheshimiwa Wabunge takribani wote mmetupongeza, na sisi tunashukuru sana kwa kutupa matumaini na kututia moyo kwa kazi kubwa inayofanyika, tunashukuru zaidi namna ambavyo Waheshimiwa Wabunge wote mmetambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niseme mbele ya Bunge hili, ukweli Mheshimiwa Rais ameifanya kazi kubwa na ninyi mna haki pale mliposema sasa kazi iliyobaki ni mimi na timu yangu ya Mheshimiwa Eng. Godfrey Kasekenya Msongwe na wasaidizi wetu. Hatuna tunachomdai Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli kazi ameifanya kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hapa limesemwa jambo linalohusu malipo ya wakandarasi. Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia wamesema juu ya jambo hili. Nataka niwape takwimu kiasi na nitasema kwa kiwango fulani juu hata ya hoja ya dada yangu Mheshimiwa Halima Mdee alipozungumzia juu ya performance namna alivyoisoma kwa ufasaha sana kutoka katika vitabu vya CAG. Nami ninamheshimu, sina tatizo na ninamshukuru kwa ufuatiliaji wake, lakini ninataka niwakumbushe tu kwamba, kuanzia mwaka mwaka 2021/2022 Mheshimiwa Rais ameingia, mpaka hivi leo, jumla ya fedha shilingi trilioni 2.5 zimelipwa kwa wakandarasi hapa kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kazi inaendelea na sisi sote ni mashahidi. Kazi kubwa ya ujenzi katika nchi yetu inafanyika. Unajua niseme, kwa mfano kila mmoja hapa amepongeza juu ya Daraja la Kigongo – Busisi. Daraja la Kigongo – Busisi limejengwa kwa viwango vikubwa na ni daraja la mfano. Sasa, ninawahakikishia, Wakandarasi pale wataendelea kulipwa na wale walichokibakiza ni kidogo.

Mheshimiwa Spika, hata hawa wakandarasi wetu wa ndani, ukitazama figures ambazo walikuwa wakidai wakati huo na figures ambazo zinadaiwa hii leo, kila wakati na kila mwezi Wizara ya Fedha imekuwa ikiendelea kutupa fedha, na tunalipa kiwango kwa kiwango.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba bado kuna madeni yanayodaiwa. Wakandarasi wandani wanatudai na wakandarasi wa nje wanatudai lakini jitihada za kulipa zinafanyika. Yapo makubaliano tuliyoyafanya, sisi Wizara ya Ujenzi na wenzetu Wizara ya Fedha, kadri fedha zinavyokusanywa na wao wanatuletea zile fedha sisi tunawalipa wakandarasi wetu na madeni mapya yanazaliwa kwa sababu hatujasimama, kazi ya kujenga nchi yetu inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukumbushane hapa pia, hata tulipojenga SGR ni fedha hizi hizi ambazo zinakusanywa, kikapu ni hicho hicho na zinakwenda kujenga katika SGR. SGR ambayo Watanzania wote leo tunajivunia, Watanzania wote leo tunaona kuwa ni ufahari mkubwa sana, na hiyo ni kazi ambayo imefanywa na Serikali, ni kazi ambayo imefanywa na Bunge hili na ni kazi ambayo imefanywa na Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumesema juu ya hata Bwawa la Mwalimu Nyerere. Tumeambiwa hapa juzi na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, ambaye pia ni Waziri wetu wa Nishati, kazi imefanyika kule. Miongoni mwa watu wanaofanya ile kazi inayofanyika kule contractors, wasimamizi wanatoka huku huku Wizara ya Ujenzi. Ni katika performance hiyo hiyo, kwa hiyo, wametawanyika nchi nzima wanasimamia mambo haya kwa sababu, fedha hizo ni za kwetu wenyewe, zinalipwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumefanya kazi hiyo kama Watanzania wote, na kwa hiyo, tukisema juu ya performance, sikatai imesemwa katika vitabu, lakini ni performance. Ukiitazama kwa mapana maana yake ni kwamba kazi imefanywa na sisi wote katika nchi. Ndiyo maana tunapongezana kwa miradi hii mikubwa na mizuri iliyofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa heshima kubwa sana nimemwelewa sana dada yangu, Mheshimiwa Halima Mdee. Najua kiu yake ya kutaka kuona kazi kubwa na nzuri ikiendelea kufanywa. Ni mpenda maendeleo, na sina shaka hatashika Shilingi kwa sababu na yeye huwa anapanda SGR kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma na kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam na tutamwalika akaone performance kubwa ya Daraja la Kigongo – Busisi. Nitatamani sana atembee kwa miguu kilometa 3.2; hakuna Afrika ya Mashariki, ni jambo la mfano.

Mheshimiwa Spika, hapa niwaunge mkono Mheshimiwa Tabasam, Mheshimiwa Musukuma na Wabunge wengine wengi wa Kanda ya Ziwa waliposema kwamba, wanamsubiri kwa hamu Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aende akalifungue lile daraja ambalo linakwenda kuwa ni mfano katika Afrika ya Mashariki na Kati, ambalo ni tunu sasa.

Mheshimiwa Spika, yaani lile ni jambo ambalo sijui tuliweke katika alama zetu za Taifa hivi, maana ni kazi kubwa sana. Ni jambo kubwa sana limefanywa. Kwa hiyo, naona tuyatazame mambo haya kwa upana sana na tusiyatazame haya madogo madogo ambayo yatatufanya tunyong’onyee na tusitembee kifua mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi kubwa inaendelea kufanywa na kupitia hili ndiyo hapa sasa nataka nimwombe vilevile mtani wangu Mheshimiwa Kasalali Mageni, bwana, usiwe na wasiwasi mimi nimekusikia. Hawa waliokwambia huko mwanzo, umetumia lugha ya kusema wamekudanganya, nawe sasa mtani, Mheshimiwa Ulega umeingia katika uwongo huo huo; usiwe na wasiwasi.

Mheshimiwa Spika, jambo lipo katika vitabu na ninataka nikuhakikishie nina safari ya Mwanza, tutakwenda mimi na yeye kule kwake Sumve, nitakwenda kulisimamia jambo hili na ninajua hivi sasa watani mnapenda sana maendeleo, mmechoka kufanya ile biashara. Huwa nawatania wakati mwingine na uniruhusu, katika nchi yetu utani upo, maana wameomba taa nyingi sana, wanakusudia kuwakimbiza fisi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana Mheshimiwa Kasalali amekuwa mkali sana juu ya jambo hili. Ndiyo maana Mheshimiwa Cherehani na Mheshimiwa Kiswaga wamezungumzia sana juu ya taa za barabarani. Najua shida yenu ni kuwafukuza wale jamaa. Mimi nataka asikasirike, sisi tunamhakikishia hataharibikiwa kwa sababu ya barabara hii.

Mheshimiwa Spika, tukimaliza tu hii bajeti, tunafanya procurement ya haraka, advance payment watapata na tutakwenda kusukuma kwa pamoja watu wa kule Sumve, ili kama tatizo ni hilo tujitahidi kwenda kukutetea. Labda kama wana matatizo yao mengine, hilo sasa ni yeye na wao, lakini mimi nataka nimhakikishie, kwa jambo hili limpe comfort mtani wangu, mambo yake yatakuwa mazuri sana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naomba vilevile niseme hapa. Nilimsikia ndugu yangu, Mheshimiwa Mnzava, amesema vizuri sana, amesema juu ya Barabara ya kutoka Old Korogwe kwenda kwa Mndolwa na tena akagusia mpaka viongozi wa dini.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali ya Awamu ya Sita inaheshimu na kuwapenda sana viongozi wa dini. Naomba nianzie hapo. Inaheshimu na kupenda sana viongozi wa dini katika Taifa letu, na ndiyo maana ile barabara aliyoisema ya kutoka Old Korogwe mpaka Kwa Mndolwa, amesema Wabunge wameiomba, lakini ikasisitizwa zaidi na kiongozi wa kiroho, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Bin Zubeir Bin Ally.

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunakwenda kutengeneza hiyo barabara kilometa zile 10 kwa kuonesha msisitizo namna Serikali hii inavyoheshimu dini na inavyoheshimu viongozi wa dini. Pale Kilimanjaro tuna Barabara ya Askofu Shoo, maarufu kabisa, tumeitengea fedha na yenyewe tunakwenda kuweka lami pia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule Tabora tuna Kituo cha Hija cha RC, Kanisa Katoliki, na kwenyewe tumetengea fedha, tunakwenda kuweka lami pia. Hii ni mifano michache ya namna ambavyo Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaheshimu na kuthamini sana viongozi wa dini.

Mheshimiwa Spika, ningependa sana tukubaliane, tutapitisha maombi katika Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, barabara zile zinazoombwa na kusisitizwa sana na viongozi wa dini, ikiwa ni pamoja na ile ya Kituo cha Hija kinaitwa Inafa, pale Tabora, tuzipe majina ya hawa viongozi wetu wa dini ndio, itapendeza sana na itaonesha heshima kubwa namna sisi Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambavyo inathamini sana dini na viongozi wa dini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa lipo jambo pia, limezungumzwa juu ya wakandarasi wa ndani. Namshukuru sana kaka yangu, Mheshimiwa Getere, amelisema vizuri sana jambo hili kwamba, tuwathamini wakandarasi wa ndani na tuwawezeshe. Akasema, kwa nini hatutengenezi sheria na kanuni?

Mheshimiwa Spika, Bunge tayari lilishatengeneza Sheria na tayari tumeshapitisha Kanuni, ipo Kanuni ya 39, Kanuni Ndogo ya Tatu na ya 10, ambapo hii Kanuni ya Manunuzi ni ya Mwaka 2024. Inasisitiza juu ya kuwapa kipaumbele wakandarasi wake wa ndani, lakini inasisitiza vilevile juu ya kuhakikisha miradi. Wale wanaotoka nje kuja hapa ndani tunafanya nao JV.

Mheshimiwa Spika, kazi tunayoisubiri hivi sasa ni kuhakikisha kwamba, documents za mifumo ya manunuzi, ambayo hii sasa ipo chini ya Wizara ya Fedha na sisi tayari tunafanyanao mazungumzo, ili kusudi wazibadilishe, maana zile kanuni zetu mpya hazijaingia bado katika mfumo ule wa manunuzi.

Mheshimiwa Spika, nataka nikuhakikishie, katika mwaka wa fedha 2024/2025 kwa kuwa, sisi upande wa kanuni tumeshakamilisha, ina maana na wenzetu wa Wizara ya Fedha PPRA watakamilisha na sasa tutakwenda kuwapeleka wakandarasi wetu waweze kufanya JV na kampuni yoyote itakayokuja kupata kazi hapa nyumbani Tanzania. Hiyo itawajengea uwezo wa kitaaluma, uwezo wa kifedha na vilevile uwezo wa kivifaa.

Mheshimiwa Spika, hili tumelitengenezea mpaka formula kwamba, tutakapofanya hiyo JV, mzawa kampuni yake iwe na asilimia ngapi na mgeni kampuni yake iwe na asilimia ngapi, lakini wakati huo huo kwa kuanzia, Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nimesema na sasa narudia kusema kwamba, katika ile miradi ya dharura iliyofanywa mwaka 2025 uliokwisha, baada ya mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya, jumla ya miradi 81 yenye thamani ya shilingi bilioni 566.9 ilisainiwa.

Mheshimiwa Spika, katika miradi hiyo 81 makandarasi wa ndani wamechukua miradi 70 yenye jumla ya fedha shilingi bilioni 414 na hizi fedha wameshalipwa, advance payment, zaidi ya shilingi bilioni 80. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, fedha hizi zipo kadiri ya wanavyofanya kazi, wanaleta certificate, tunawalipa.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana jana hapa katika mimbari hii nilizungumza juu ya kwamba, tunawapongeza sana makandarasi wetu wa ndani, na nikatolea mfano wakandarasi kadhaa, akiwemo yule ambaye amezungumzwa vizuri hapa, anaitwa Makapo Contractors. Yule nilipofanya ziara ya kwenda kukagua fedha hizi, nilikuta kabla hajapewa hata advance payment, ameshafika asilimia 25 ya utekelezaji wa ule mradi.

Mheshimiwa Spika, huu ni uthibitisho ya kwamba, wapo wakandarasi wazawa wazalendo, wapo serious, wanafanya kazi yao kizalendo na sisi tutaendelea kuwazingatia na tutahakikisha kwamba, tunawaunga mkono.

Mheshimiwa Spika, leo katika kikao, kwa sababu, ipo hoja hapa ilizungumzwa na Mheshimiwa Getere pia, ya kwamba, kwa nini tusitengeneze mfuko? Mfuko upo, tena upo kwa mujibu wa sheria. Mfuko ule unategemea tozo za Bodi yetu ya Wakandarasi, ambayo mpaka sasa hivi ina shilingi bilioni 4.2, ndiyo ile uliyoiona katika kitabu na Bodi ya Wakandarasi imeingia katika makubaliano na Benki ya CRDB kwamba, wao wanaweka shilingi bilioni nne na CRDB inaweka shilingi bilioni nne.

Mheshimiwa Spika, baada ya kupata taarifa hiyo, nimewaambia wataalamu wangu, tunaanzisha hili jambo mchakamchaka wa kuhakikisha kwamba, tunatafuta fedha za kuongeza kwa sababu, CRDB Bank ipo tayari, sisi tukiwa na shilingi bilioni 100 na wao wanaweka shilingi bilioni 100. Maana yake ni nini?

Mheshimiwa Spika, hiyo itasaidia wakandarasi wetu wa ndani kupata fedha za uhakika za advance, hiyo itasaidia wakandarasi wetu wa ndani. Kuna kitu kinaitwa big security, watakuwanayo ya uhakika na kwa hiyo, hata tunapowapeleka katika JV na wao watakuwa comfortable kwa sababu, wana uwezo. Hili jambo tunakwenda kulifanya tukishirikiana na wenzetu wa Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza humu juu ya ukarabati wa Barabara Kuu ya Dar es Salaam – Kibiti – Lindi. Waheshimiwa Wabunge nataka niwahakikishieni kwamba, jambo hili ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na hata Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuwa ametumwa na Mheshimiwa Rais kwenda kukagua barabara ilipokatika, naye akasisitiza maelekezo yale ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, tunakwenda kuifanya kazi hii kwa ufasaha. Pia niwaondoe hofu ndugu zetu wa Mikoa ya Kusini, kazi kubwa kule inaendelea. Hivi leo nataka niwaambie, tuna jumla ya shilingi bilioni 400. Zaidi ya shilingi bilioni 400 zinakwenda kujenga Barabara ya kutoka Mtwara mpaka Mnazi Mmoja, pale Mingoyo na inayotoka Mnazi Mmoja, Mingoyo, inakwenda mpaka Masasi.

Mheshimiwa Spika, hiki ni kitu cha uhakika, kutoka Mtwara mpaka Mnazi Mmoja tumeshasaini na Mkandarasi tumeshampa pesa zake za awali. Baada ya wiki mbili tatu zijazo tunamlipa na mkandarasi wa kutoka Mingoyo, kwa maana ya Mnazi Mmoja, mpaka kule Masasi. Barabara hii ina fedha za uhakika, tunakwenda kuijenga.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niwape uhakika ya kwamba, kazi nzuri na kubwa Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaitekeleza katika maeneo yale. Vilevile namshukuru sana Naibu Waziri, Mheshimiwa Eng. Kasekenya, pale alipoeleza juu ya Barabara ya Newala – Mnevata na yenyewe ipo na inajengwa. Kwa hiyo, hakuna mahali ambapo hapajaguswa, hakuna mahali ambapo pataachwa bila ya kufanyiwa kazi. Nchi nzima inajengwa na tutaendelea kuijenga nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile ipo Barabara ya kutoka Dodoma mpaka Iringa. Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati amezungumzia juu ya suala la kutengenezwa kwa bypass, ametoa ushauri, kwa nini Kitonga haipati suluhu?

Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na takribani watu wote sisi ambao tunatumia barabara hii, pale Kitonga, sasa tunakwenda kutafuta bypass na tunaiweka katika bajeti ya mwaka 2025/2026, zitaongezeka kilometa 32, lakini hata zikiongezeka kilometa 32 ni bora zaidi kuliko kwamba, barabara inakatika na baadaye hatuna pa kupita. Kwa hiyo, hili tunakwenda kulitekeleza haraka iwezekanavyo katika mwaka huu wa fedha wa 2025/2026. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile imezungumzwa hapa Barabara ya kutoka Babati – Singida. Waheshimiwa Wabunge wote wa Mkoa wa Manyara wameizungumza. Mheshimiwa Asia Halamga kataja majina hapa, Dareda, Katesh mpaka Gehandu. Nataka niwahakikishie, na yenyewe yote tumekubaliana tunakwenda kuifanyia ukarabati.

Mheshimiwa Spika, jana Mheshimiwa Issaay na Mheshimiwa Flatei waliniomba, kwamba nifanye ziara kule Mbulu, kwa ajili ya kwenda kumsukuma yule mkandarasi. Tunakwenda haraka iwezekanavyo. Tutakwenda kusimamia ile Barabara, kwenda kumsukuma yule mkandarasi ambaye, anasimamia eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile Barabara ya kutoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam, kwa maana ya Morogoro, na yenyewe imeelezwa hapa. Tutaendelea kuifanyia maintenance kadiri tunavyopata fedha.

Mheshimiwa Spika, naomba pia, nijelekeze katika baadhi ya Waheshimiwa Wabunge ambao wameonesha nia hapa ya kusema watakwenda kushika shilingi. Yupo Mheshimiwa Jacqueline Msongozi, namwomba asishike Shilingi kwa sababu, barabara ile aliyoizungumza, ya Litukila – Songea, ile barabara ina pesa za uhakika. Tupo katika hatua ya mwisho ya kupata mkandarasi na baada ya kumpata mkandarasi, basi hata ile bypass ya pale Songea na yenyewe ni sehemu ya Mradi ule mkubwa wa Lutikila – Songea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile naomba pia, nimtoe hofu Mheshimiwa Gulamali, ambaye amezungumza hapa akisema kwamba, watangulizi wangu waliahidi barabara kilometa kadhaa. Cha ajabu, mimi naonekana nimekuja kuifuta kabisa barabara yenyewe. Namwomba Mheshmiwa Mbunge sasa atembelee ukurasa wa 278 na 210 atakuta hizi barabara zipo mle. Kwa kuwa, ameisema hapa na sisi tutasisitiza juu ya kuweza kupata, kuanza kuwekwa vipande vya lami ile barabara.

Mheshimiwa Spika, vilevile Waheshimiwa Wabunge kadhaa, yupo mama yangu leo asubuhi amezungumza kusema, Serikali inafanya usanii. Hatufanyi usanii. Kusema ukweli, ipo barabara kule Same, na nilikwenda Same. Niliombwa na Mheshimiwa Mama Malecela Anne Kilango kwamba, twende kule barabara, imekatika, na kweli tulikwenda, tukaikagua ile Barabara ya Ndungu – Mkomazi, pale Same, na tukarudishia ile njia.

Mheshimiwa Spika, sasa barabara ikianza, imeanza, ikiandikwa katika vitabu vya Serikali ni vizuri kuendelea kuisimamia ijengwe, lakini tukizungumza lugha ya kusema tuitoe kabisa kwa sababu, kinachofanyika ni kama usanii, hii siyo kweli.

Mheshimiwa Spika, nadhani jambo la msingi ni Serikali kuendelea kuisimamia. Namshukuru Mheshimiwa Mama Anne Kilango kwa sababu, ameendelea kusimamia juu ya jambo hili. Yeye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati, amenieleza, amenikumbusha tukiwa katika Kamati kwamba hebu isimamie hii barabara, nami nitaendelea kuisimamia na tutapata hizo tano, 10, 15, 20 mpaka kuendelea na hatimaye barabara ile ya wananchi itawaondolea watu kero. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge, Serikali inapoanza maana yake imeanza, na itaendelea kuifanyia kazi hiyo ahadi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa viwanja vya ndege. Tayari Mheshimiwa Naibu Waziri ameelezea baadhi ya viwanja vya ndege ambavyo vilikuwa vimekwama kabisa, lakini niseme tu kwamba, Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya kazi nzuri. Vipo viwanja vya ndege watu walikuwa wameshaanza kukata tamaa, lakini ukweli ni kwamba, vimefufuka. Hata wale wa Tanga, ambao wenyewe wanasema waja leo kuondoka majaaliwa, sasa wamesisitiza wanataka kiwanja cha ndege.

Mheshimiwa Spika, Kiwanja cha Ndege cha Tanga tumeshafanya manunuzi na tumeshapata mkandarasi na kwa hivyo, mkandarasi, tunakwenda kumpa advance payment kwa sababu, hela zake ni za uhakika na tunakwenda kuanza kujenga kile kiwanja. Kwa hiyo, Uwanja wa Ndege wa Tanga unakwenda kujengwa vizuri na ndiyo maana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia, alipofanya ziara pale Tanga alisisitiza na kusema anaifungua Tanga kibiashara.

Mheshimiwa Spika, sasa Tanga itapitika kwa njia zote, itapitika upande wa kutoka Bagamoyo mpaka Pangani, Tanga, lakini vilevile itapitika kupitia barabara kubwa ambayo leo mmeizungumza hapa Waheshimiwa Wabunge karibu wote wa mkoa huu wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kiwanja cha ndege kitakuwa kimepatikana. Kwa hiyo kuna wengine walitaka kuchukua Shilingi yangu, akina Mheshimiwa Eng. Mwanaisha Ulenge, na alisisitiza sana, anaogopa akichukua hii Shilingi mdogo wake kule nyumbani atakuwa hana cha kupika. Basi usichukue, nakuomba kwa heshima kubwa na taadhima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kuendelea kuwaambia Waheshimiwa Wabunge kwamba hoja zote tumezichukue. Ni wengi sana wamechangia, ambao ni 81, na hili ni jambo kubwa sana. Tumelichukua jambo hili na wengi hapa tumekubaliana kwamba tutakwenda kufanya ziara katika maeneo yao mbalimbali waliyoyasema. Nimeyachukua yote yale ambayo wameyasisitiza na tutakwenda kuyafanyia kazi na ziara tutazifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutaendelea kujenga barabara katika nchi yetu bila ya kuchoka, bila ya kusimama. Naomba kwa heshima kubwa na taadhima Waheshimiwa Wabunge watuunge mkono, watupitishie bajeti hii. Imepanda kwa viwango vizuri, shilingi trilioni 2.2 kutoka shilingi trilioni 1.6, ni ongezeko la zaidi ya 28%.

Mheshimiwa Spika, tutafanya kazi usiku na mchana, hatutachoka na utakwenda kila kona ya nchi yetu. Hapa hapa katika hii miezi miwili iliyosalia tutahakikisha tunafika kadri iwezekanavyo mimi na mwenzagu na wataalamu wetu kuhakikisha kwamba tunakwenda kusaidia kutatua changamoto mbalimbali walizonazo Waheshimiwa Wabunge kwenye majimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe hoja, na ninaomba kwa heshima kubwa na taadhima Waheshimiwa Wabunge watuunge mkono katika hoja hii. Naomba kutoa hoja. (Makofi)