Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana Mtemi wa Kabila la Wasukuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache tu ya kushauri. Pengine nianze na hili la retention ambalo limezungumzwa na Mbunge aliyepita Mheshimiwa Rwamlaza. Retention kwa mapendekezo ya Serikali ni jambo zuri kwa sababu uzoefu unaonesha sisi ambao tumekuwa tukishughulika na mahesabu ya Serikali, ziko taasisi ambazo wanatumia fedha hizi vibaya. Kwa hiyo, Mpango huu wa Serikali ni mzuri, waendelee nao, isipokuwa Halmashauri zote nchini pamoja na Mifuko ya Hifadhi za Jamii, hao wasiwekwe kwenye kundi la kupeleka fedha kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina, waendelee kubaki na makusanyo. Bahati nzuri Mheshimiwa Rwamlaza tuko Kamati moja nadhani kule tutaendelea kushauriana vizuri ili Halmashauri zetu zisije zika-suffocate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la kilimo. Iko mikoa ambayo kila mwaka inakumbwa na njaa na haipungui mikoa 12 lakini kwenye Mipango yetu hapa sijaona mipango mahsusi na ya makusudi ya kuhakikisha kwamba mikoa hii wanaiwekea miundombinu ya umwagiliaji. Mikoa mingi upande wa Kanda ya Ziwa tuna maji ya uhakika, tunahitaji miundombinu ya umwagiliaji, tumechoka kuletewa chakula kila mwaka. Labda tuambizane hapa kwamba mikoa ile ambayo inakuwa na njaa kila mwaka tumeitelekeza na kwamba tutaendelea na Kamati za Maafa ili tuwe tunaendelea kuwapelekea tani za chakula ilhali wao ndiyo wamebahatika kuwa na maji ya uhakika, wanaweza wakamwagilia na tukapata chakula tukajitosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano pale Bunda tayari eneo la EPZ limetengwa zaidi ya hekari 1,350. Naishauri Serikali kwenye Mpango huu, hebu sasa mikoa ile ya Kanda ya Ziwa kwa kuanza na maeneo hayo ya EPZ watuwekee miundombinu ya umwagiliaji ili tusiendelee kuombaomba chakula. Kila mmoja hapa anajua madhara ya njaa, watu wenye njaa hawatawaliki, watu wenye njaa hawatulii na watu wenye njaa hawawezi wakashiriki kwenye maendeleo ya huu Mpango tunaouweka hapa. Utashirikije kwenye maendeleo wakati una njaa? Wakati mwingine hatutulii humu ndani, hakuna amani na utulivu kwa sababu watu wana njaa za aina mbalimbali humu. Wengine wana njaa ya pesa, wengine wana njaa ya kushika madaraka, huwezi kutulia humu ndani, ni mifano ya njaa ukiwa na njaa huwezi kutulia. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la reli. Kwenye Mpango huu nishauri jambo moja na hii itakuwa ni hatari kwa Serikali. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais, ukurasa wa 12 ameelekeza kujenga reli ya kutoka Dar es Salaam - Rwanda na kwa kwenye Mpango Serikali inasema itajenga reli ya kati kwa standard gauge. Sasa kitendo cha kunyamaza au cha kuwa na kigugumizi sijui kimetoka wapi cha kutotaja reli yetu ya kati ya kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma na michepuko yake ya kwenda Kalema kwenda Msongati, michepuko ya kwenda Mwanza na baadaye twende Dutwa kule kwa ajili ya nickel. Serikali inaweza kutumia uchochoro huo na kwa sababu wanamshauri vibaya Mheshimiwa Rais, kama wameweza kutaja michepuko ya kutoka Mtwara kwenda Liganga na Mchuchuma, michepuko ya reli kutoka Tanga kwenda Arusha na Musoma na michepuko ya Minjingu na Engaruka kuna kigugumizi gani cha kutotaja reli ya kati kwamba ndiyo inayoenda kujengwa kwa standard gauge? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mpango huu kuna eneo la kukarabati reli ya kati. Kwa hiyo, tunaweza kukuta ule mtandao wetu wa reli ya kati ukaishiwa kukarabatiwa halafu tusiwe na standard gauge matokeo yake wanampelekea Rais Kagame. Nani asiyejua Kagame anatamani Bandari ya Dar es Salaam? Nani asiyejua Kagame aliwahi kusema akipewa mwezi mmoja atakusanya fedha za Bandari ya Dar es Salaam kuendesha Rwanda kwa mwaka mzima? Nani asiyejua Kagame alianzisha UKAWA ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wakamtenga Rais wetu ili waweze kujenga reli ya Mombasa mpaka Rwanda na sasa wanavuka Naivasha. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye utalii. Tunahitaji kuinua pato la Taifa na ili tuliinue ni lazima tushughulike na ujangili ambao unatishia wanyamapori na ujangili unaotishia watalii kuja Tanzania.
Naomba Mheshimiwa Maghembe haya mambo ya kuandika humu kwamba tunataka kuboresha miundombinu, kununua zana za kupambana na majangili, mpaka sasa zana za kupambana na majangili unazo, tulikuwa na helkopta juzi majangili wameitungua, hizo ndizo zana za kupambana na majangili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama majangili wameanza kutungua ndege ambazo ndizo zana za kupambana na majangili maana yake tukiendelea kukupa hizi zana za kupambana na majangili wataendelea kuzitungua. Idara yako ya Wanyamapori na Hifadhi yako ya Ngorongoro ndiko kwenye wafanyakazi wasiowaaminifu kwenye Idara ya Intelejensia ambao wanaazimisha silaha za kivita, wanawapa majangili halafu wanatungua ndege. Waheshimiwa Wabunge, hizi ndege zinaendelea kuanguka kwenye hifadhi hata ile ya Marehemu Filikunjombe ilianguka kwenye Hifadhi ya Selous. Kwa nini nisiamini kwamba inawezekana kwa sababu walikuwa kwenye Hifadhi ya Selous ambako ujangili wa tembo ni mkubwa, ni majangili hawa hawa waliangusha ndege ya Mheshimiwa Filikunjombe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inakuwaje ninyi katika kuajiri askari wa wanyamapori na kwenye Kikosi cha Intelejensia hamuwa-vet? Watu wengine wamefukuzwa polisi ndiyo hao mnawachukua, mnawachukua kwa sababu ya ubinamu, ujomba na mwingine ameshiriki kuangusha ndege ya Rubani Gower, maskini Mungu aiweke roho yake mahali pema. Mtu huyu ameajiriwa wakati alifukuzwa ni mhalifu, ni jambazi matokeo yake ameshiriki kwenye tukio hili.
Mheshimiwa Maghembe unafanya kazi gani na yule Mhifadhi pale ambaye ndiye anashughulika na ajira za watu wa namna hii? Tutaendelea kuwa na majangili hata ukileta zana za kupambana nao kama wafanyakazi wa Idara yako hautawa-vet na kuwasimamia vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme jambo moja. Mpango huu ni mzuri sana na katika uzuri wake ndiyo maana tunaomba kuendelea na mapendekezo haya ili Serikali ije na rasimu ikiwa inaonesha sasa Mpango huu unatekelezeka. Nakuhakikishia Mpango huu ukirudi jinsi ulivyo mkadharau mapendekezo ya Wabunge hautatekelezeka, zitabaki ni hadithi, zitabaki ni porojo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kutaja maeneo ambayo reli yetu inaenda kujengwa kwa standard gauge kwa kisingizio kwamba hamuwezi kutaja kila kitu, kama hamuwezi kutaja kila kitu mbona maeneo mengine mmetaja? Kama mtakuja hapa bila mwelekeo wa reli ya kati, nitakuwa mtu wa kwanza kusema kwamba rasimu hii hatuikubali, nitakuwa mtu wa kwanza kutokubaliana na bajeti ya kupitisha mpango ambao hauna dhamira nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule pembezoni Kanda ya Ziwa mfuko mmoja wa simenti shilingi 20,000 wakati Dar es Salaam ni shilingi 12,000, Watanzania hawa watajenga lini nyumba? Misumari, nondo, gharama za usafirishaji zinakuwa kubwa lakini tunaendelea kupiga chenga zaidi ya miaka 15. Hayo makelele yenu mliyonayo huko kwenye mambo ya tender, sisi hatutaki vurugu zenu huko, endeleeni kukaa vizuri, tunachotaka ni kujenga reli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo taarifa, reli hii Waheshimiwa Wabunge…
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Ahsante sana Mtemi wa Wasukuma. (Makofi)