Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Rashid Mohamed Chuachua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MOHAMED R. CHUACHUA: Microphone yangu haiwaki hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Serikali kwa mwaka 2016/2017. Kabla sijaanza kuchangia, kwa heshima kubwa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika katika Bunge hili, lakini pia nawashukuru Watanzania wote kwa kukichagua Chama cha Mapinduzi kwa kishindo kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa namna ya kipekee ninawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Masasi kwa kazi kubwa waliyofanya ya kampeni takribani miezi mitatu, minne hivi katika uchaguzi mdogo. Hawakukata tamaa walifanya kazi usiku na mchana hatimaye CCM imeshinda kwa kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa namna ya kipekee, naomba nitumie fursa hii kuwaambia wananchi wa Masasi chaguo walilolifanya ni chaguo sahihi kukichagua Chama cha Mapinduzi, lakini kunichagua mimi mtoto wao ili niwapiganie na tutatekeleza tuliyo waahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishauri Serikali iendelee kuweka nguvu kubwa katika kukusanya mapato. Iendelee kuweka nguvu kubwa katika kuhakikisha kwamba wanakusanya kodi na kuwachukulia hatua wakwepa kodi wote pamoja na kuongeza juhudi zake za kupambana na ufisadi. Haya ni mambo ambayo tukiyafanya kwa nguvu kubwa tunaimani kwamba tunaweza tukasonga mbele kiuchumi.
Vile vile niwashukuru sana wale walioandaa mapendekezo haya na niseme tu mapendekezo haya yameakisi kwa kiasi kikubwa Hotuba ya Mheshimiwa Rais, lakini pia yameakisi kwa kiasi kikubwa ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kutoa mchango wangu katika sekta ya kilimo, kila mmoja wetu hapa anafahamu umuhimu wa sekta hii, namna ambavyo sekta hii ina uhusiano mkubwa sana na Sekta ya Viwanda. Hata hivyo, niseme tu Serikali ina mzigo mkubwa sana kuhakikisha kwamba sekta ya kilimo inasonga mbele na lazima tuelezane wazi kwamba hatuwezi kusonga mbele katika viwanda kama sekta ya kilimo haitapewa uzito mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa naomba niishauri Serikali lakini pia nimshauri Waziri mwenye dhamana kuwa ana kazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba kilimo kinasonga mbele. Tunapozungumzia kilimo tunazungumzia sekta tofauti tofauti, lakini pia tunazungumzia suala la mazao ya biashara. Kwa kweli hali ya manunuzi na mauzo ya mazao yetu ya biashara haijafikia kwenye kiwango cha kutembea kifua mbele. Nasema hivi nikiwa naakisi Jimbo langu la Masasi ambapo mchakato mzima wa ununuzi wa zao la korosho kama zao kuu la biashara umegubikwa na mambo mengi ambayo yanamkandamiza mkulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Serikali ihakikishe kwamba kama tunataka kusonga mbele katika viwanda basi ni lazima kuhakikisha kwamba tunaondoa kero zote zinazomkandamiza mkulima wa zao la korosho. Zipo kero nyingi, kuna makato yasiyo na sababu za msingi, kuna sheria ambazo kimsingi zinapaswa zifanyiwe marekebisho ili kusudi korosho imnufaishe mkulima na iwe ni zao lenye tija. Pia mchakato mzima wa pembejeo na usambazaji wake nao umegubikwa na mambo ambayo kimsingi yanamkandamiza mkulima. Wapo wanaopata pembejeo ambao hawakustahili pembejeo. Namwomba Waziri mwenye dhamana aliangalie sana eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo deni kubwa kwa Watanzania na tusingependa kusikia tena Watanzania wakiendelea kulalamika kuhusu mazao yao ya biashara. Kero hizi namwomba Waziri mwenye dhamana na Serikali ihakikishe kwamba inaziondoa na tutaisaidia Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanakiona kilimo chao kikiwa kina tija. Pamoja na mambo mengine wakati wote wakulima wetu wamekuwa hawana dhamana ya kuweza kupata mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali itoe nguvu kubwa kuhakikisha Benki ya Kilimo inawafikia wakulima, lakini tuhakikishe kwamba rasilimali zao zinarasimishwa ili waweze kupata mikopo, waweze kupata hati miliki na waweze kukopesheka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo katika Jimbo la Masasi tunacho Kiwanda cha Korosho, kiwanda hiki ni cha muda mrefu tungependa pia kiwanda hiki kiweze kufanya kazi ili wananchi waweze kubangua korosho zao na kuzisafirisha zikiwa zimebanguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo mengine ya msingi nitazungumzia kuhusu barabara, tunapozungumzia Kusini na mchango wake katika uchumi ni lazima tukumbuke kwamba wakulima wanaweza kurahisishiwa shughuli zao za kusafirisha mazao kama barabara zetu zinapitika. Tunalo tatizo kubwa tumeona katika mpango kuna kilomita kadhaa zilizotengwa kwa ajili ya barabara zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ningeomba Serikali safari hii iangalie Mikoa ya Kusini ambayo imekuwa ikisahaulika sana kwa ujenzi wa barabara zetu. Zipo barabara zina umuhimu mkubwa kama waliotangulia kusema wenzangu kama vile barabara ya Ulinzi inayotokea Mtwara inakwenda Tandahimba na Nanyamba - Newala inakuja kutokea Nanyumbu, hii ni barabara muhimu sana. Ipo barabara nyingine ya kutokea Mtwara unakwenda unatokea mpaka Jimbo la Lulindi unaingia Jimbo la Masasi hii ni barabara muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa namna ya kipekee tunaiomba Serikali itutengenezee barabara ya Masasi kwenda Nachingwea, tunaomba Serikali itutengenezee barabara inayotoka Jimbo la Masasi inaelekea Jimbo la Ndanda na inakwenda kukutana na Jimbo la Nanyumbu kupitia katika Kata za Mwengemtapika Kata za Mlingula, Kata zote hizo mpaka tunafika katika hayo Majimbo mawili. Hizi ni barabara muhimu kwa ajili ya usafirishaji wa mazao ya wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mchango mwingine kwa upande wa elimu, tunalo tatizo kubwa. Katika elimu tunazo changamoto lakini pia tunakila wajibu wa kuishukuru Serikali kwa kazi kubwa iliyofanya. Sisi ambao tumeishi katika Ualimu takribani miaka 15, 16; tunajua namna ambavyo Wananchi wameguswa na suala la Serikali kufanya elimu bila malipo. Hili ni jambo la msingi sana na sote tunapasa kuipongeza Serikali kwa kazi yake kubwa iliyofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba Waziri mwenye dhamana pamoja na Serikali iangalie namna ambavyo tunataka kuboresha elimu isisahau elimu nje ya mfumo rasmi. Tunapotaka kuboresha elimu, tusifikirie tu kuboresha elimu kwa upande elimu iliyo rasmi, tuangalie pia elimu nje ya mfumo rasmi. Ningeiomba Serikali ifanyekazi pamoja na Wizara husika, kukaa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, ione namna ambavyo inaweza, ikatoa mchango mkubwa katika kuelimisha watu nje ya mfumo ulio rasmi wa elimu. Ni lazima tukubali kwa sasa kwamba tunao Watanzania wengi wasiojua kusoma na kuandika, tunao Watanzania wengi wenye hitaji la elimu lakini wako nje ya mfumo rasmi wa elimu; hawa wanahitaji msaada mkubwa tusije tukawasahau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo la maji, Mapendekezo ya Mpango yameonesha namna ambavyo Serikali inakwenda kulitatua tatizo la maji. Niseme tu, niishukuru Serikali kwa namna ya kipekee kwa kujumuisha mradi mkubwa wa maji wa Mbwinji na kutaka kutengeneza mipango ya kuuendeleza kwa sababu mradi huu ni muhimu sana, kwa wananchi wa Jimbo la Masasi, lakini pia ni muhimu sana kwa Watanzania. Nawashukuru sana Serikali kwa kuweka mpango huu ili kusudi maji sasa yafike katika vijiji vyote vya Jimbo la Masasi, ambavyo havina maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza kuhusu suala la barabara, lakini ni muhimu kuelewa kabisa, tunapoizungumza Mtwara na miundombinu yake lazima tuzungumzie pia uwanja wa ndege. Uwanja huu umekuwa ukiimbiwa mara nyingi kwamba unahitaji marekebisho ya kina, lakini marekebisho haya yamekuwa hayafanywi. Si jambo zuri mpaka leo tukiwa tunazungumzia uwanja ambao ni uwanja wenye sifa za kuweza pengine kuwa wa Kimataifa, lakini hauna taa. Uwanja huu haujafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu. Tunaiomba Serikali yetu sikivu ifanye kazi katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo changamoto kubwa katika huduma zetu za afya, katika Jimbo la Masasi zipo zahanati saba tu. Tunajua Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha kwamba kila Kijiji, kila Kata kinakuwa na zahanati, lakini lengo hili halijafikiwa ipasavyo katika baadhi ya maeneo. Tunaiomba Serikali wakati inataka kupiga hatua mbele kuelekea katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda, tuangalie pia jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Chuachua.