Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu katika uchumi wa nchi yetu. Naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye mchango wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) ni miongoni mwa mashirika ya umma yanayotuingizia pesa nyingi sana katika nchi yetu. Utalii katika nchi yetu unachangia 18% ya GDP ya Taifa. Jambo la ajabu na la kusikitisha sana, miaka zaidi ya mitatu TANAPA haina Bodi ya Wakurugenzi. Maamuzi muhimu yamekuwa yakitolewa na viongozi wa Wizara akiwemo Waziri na Makatibu Wakuu walioondoka na hata wa sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka kadhaa kulitokea mvutano juu ya ada zinazotakiwa kulipwa na wenye mahoteli maarufu kama concession fee, walishtakiana wakapelekana Mahakama Kuu na TANAPA walishinda kesi ile lakini mpaka sasa hivi hakuna kinachoendelea kwa sababu hakuna Bodi ambayo ndiyo ilitakiwa wapange jinsi gani ada hizi zitatozwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunapoteza mapato mengi sana kutokana na kukosa hizi fee za kwenye mahoteli. Kwa mwaka TANAPA inapoteza shilingi bilioni 10 kwa kukosa fees hizi. Shilingi bilioni 10 siyo pesa ndogo, ni pesa nyingi sana. Tunaona Rais wetu anavyohangaika kutafuta pesa, anabana matumizi, shilingi bilioni 10 hizi zingeweza kupeleka maji Arusha, Karatu, Longido, Ngorongoro na zingeweza kusaidia watoto wa maskini wakakaa kwenye madawati. Sijui ni kwa nini mpaka sasa hivi pesa hizi hazijaanza kukusanywa na ni kwa nini Bodi ya TANAPA mpaka sasa hivi haijaundwa. Waziri atakapokuja ku-wind up naomba aniambie ni lini Bodi ya TANAPA itaundwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Ndugu Allan Kijazi kwa sababu amekuwa akimsaidia Rais kusaidia maskini. Tumeona juzi wamemkabidhi Mheshimiwa Makamu wa Rais shilingi bilioni moja kwa ajili ya madawati kwa mikoa 16, tunamshukuru sana kwa hilo. Nimeona nikitaja TANAPA bila kumtaja Ndugu Allan Kijazi nitakuwa sijaitendea haki hotuba yangu, nampongeza sana, naomba aendelee hivyo hivyo kum-support Rais wetu kuwa sasa ni kazi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba moja kwa moja niende katika suala zima la ujangili. Ujangili umeshamiri sana, wanyamapori wamekuwa wakiuawa, tembo wapo hatarini kutoweka licha ya Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kufanya jitihada za kutatua tatizo hili. Majangili wana silaha kali sana hasa katika mapori yetu kama Ugala, Loliondo na mapori mengine mengi. Mbaya zaidi sheria haziruhusu walinzi wa makampuni ya vitalu vya uwindaji na YWMA kutumia silaha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naona sasa hivi ni wakati muafaka wa kuleta sheria ili walinzi wa haya makampuni waruhusiwe kutumia silaha kwenye hifadhi zetu ili washirikiane na walinzi wa wanyamapori na wa TANAPA, majangili wamekuwa wakitamba sana kwenye hifadhi zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba iwekwe adhabu kali sana kwa ajii ya majangili siyo kuwa watozwe fine tu hapana, majangili wana pesa nyingi, fine kwao ni kitu kidogo. Tumeona Serikali ya Kenya wameweka sheria atakayekutwa kwenye hifadhi bila kibali anapigwa risasi sisi hata kama hatuwezi kufanya hivyo, lakini ni wakati muafaka wa Serikali kuleta sheria hapa Bungeni ikiwezekana majangili wafungwe kifungo cha maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia inasemekana kuwa baadhi ya Wabunge ni majangili, wamekuwa wanajihusisha na biashara hii ya ujangili.
Nina imani hakuna ambaye yupo juu ya sheria. Hata gazeti la Jamhuri la leo limeandika Mbunge jangili. Huyo Mbunge jangili ni nani, ni Munde Tambwe, Catherine Magiga au Ally Keissy, tunataka tufahamu. Vyombo vya usalama, vyombo vya sheria vipo wafuatiliwe ijulikane Mbunge jangili ni nani. Hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria na akikutwa kiongozi ambaye ni jangili kama Mbunge jangili ,naomba mfano uanze kuoneshwa kwake. Siyo tunalaumu tu watu wengine wakati majangili tuko nao humu humu ndani, tunataka kuwafahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi majuzi gazeti ya Jamhuri liliandika makala ikaonesha jinsi vibanda vinavyokusanya mapato ya watalii kwenye mapori ya Loliondo na Longido, vibanda vile vilikuwa vinasikitisha sana, ni vibanda vya miti tu. Kweli watalii wanatuletea dola wanakuta watu wamekaa kwenye vile vibanda wanapokea mapato tuko serious na utalii wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua Wizara haihusiki zinazohusika ni Halmashauri ya Longido na ya Monduli lakini mtalii anapokuja hazitambui zile Halmashauri bali Wizara ya Maliasili, naomba tuwe serious kwa hili. Tunataka kupokea dola za watalii, tunapokea kwenye vibanda, vibanda vya ajabu, ni aibu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja naomba nielekeze mchango wangu katika misitu. Misitu inamalizwa, biashara za mkaa zimeshamiri sababu kubwa wakisema bei ya gesi au nishati mbadala ni kubwa. Naomba suala hili la mkaa ingawa kwa Wizara ni suala mtambuka lakini bado kuna ukweli misitu yetu ambayo iko chini ya Maliasili watu wanakata mikaa wanaimaliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iliangalie sana suala hili la kukata misitu na iwachukulie hatua ambao wanauza mikaa, maana wanakata miti bila vibali na sasa hivi tumeona magari yanasafirisha mkaa usiku kwenye ma-container. Naweza nikatolea mfano pale kwa Msuguli kuna watu wanakaa pale kwa ajili ya kukagua hizi lumbesa za mazao sasa huoni kama ni wakati muafaka watu wa misitu nao wakawepo pale kwa ajili ya kuhakikisha kuwa miti yetu haikatwi ovyo na kukwepa kodi kupitia misitu? Tunaomba sana Serikali iangalie suala hili zima la mkaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona hapa watu wanaongelea kuhusu ndege, mimi akinamama wa Arusha hawaniulizi kuhusu ndege, wanauliza kuhusu maji na mitaji. Kwa hiyo, naomba tujielekeze sana kuona haya masuala ambayo ni muhimu kwa ajili ya wananchi wetu, siyo tunajiangalia sisi tu maana wale wapiga kura kule hata ndege hawapandi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba TANAPA iendelee kuwasaidia vijana na akinamama kwa kuwapa mitaji. Kuna akinamama na vijana wengi ambao wanafanya biashara ya utalii hasa katika Mkoa wangu wa Arusha iwasaidie kuwapa semina wapate elimu ya ujasiriamali ili waweze kutumia vizuri fursa hii ya utalii. Vilevile wawatafutie masoko, kuna akinamama wanauza shanga na vinyago kwa watalii watusaidie akinamama hao wapate soko ili waweze kujitosheleza na mahitaji yao mbalimbali kama ya kusomesha watoto wao na waweze kufanya biashara za kiutalii na wanufaike na utalii wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ila naomba tu Waziri atakaponijibu aniambie ni lini ataunda Bodi ya TANAPA, la sivyo nitatoa shilingi.