Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. HASNA S.K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nichangie Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Kwanza, nimshukuru Mwenyezi Mungu, niwashukuru pia na wapiga kura wangu wa Jimbo la Kigoma Kusini kwa dua na maombi yao yaliyowezesha kesi iliyokuwa na mvuto mkubwa zaidi ya miezi sita hatimaye tarehe 17 Mahakama imeweza kutupilia mbali shauri la Ndugu David Kafulila. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami nijikite kwenye hoja iliyopo mbele yetu. Kwenye Wilaya yangu ya Uvinza tuna matatizo katika baadhi ya maeneo kwa mfano kwenye Kata ya Uvinza kuna Kitongoji cha Tandala. Kile kitongoji kimesajiliwa kwa mujibu wa sheria na wananchi wanaishi pale, lakini tatizo kubwa ambalo liko pale wananchi hawawezi kufanya shughuli yoyote ya maendeleo kwa sababu wanaambiwa pale ni eneo la hifadhi. Sasa unajiuliza inakuwaje eneo la hifadhi ambalo wananchi wanaishi zaidi ya miaka 35.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, nimeona kwenye hotuba yake ameonesha kwamba kwenye Halmashauri za Wilaya ana hekta karibu milioni 3.1, lakini kuna maeneo mengine yapo tayari yanakaliwa na wakaazi, tungeomba maeneo kama hayo yaweze kuachiwa na hatimaye yatumiwe na wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, hicho Kitongoji cha Tandala hawana shule, wanasoma kwenye kibanda. Nimeweza kuwasaidia vitabu, nimewasaidia vifaa mbalimbali vya kujifundishia, kuna mzee mmoja amejitolea pale kufundisha watoto, watoto hawawezi kutembea kutoka pale mpaka kwenye Kijiji cha Chakuru kwenda kutafuta elimu. Kwa hiyo, ningeomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha hapa hoja yake, basi aweze kuangalia maeneo kama hayo, Wizara iweze kuachia tuendelee na masuala ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo vilevile tatizo kama hilo kwenye Kata ya Nguruka, Kitongoji cha Nyangabo. Tunalo eneo la hifadhi linaitwa Rukunda Kachambi, nimeenda kutembelea pale, unakuta nyumba ya mkaazi hii hapa na GN iko nyuma ya choo. Wananchi wamebanwa kabisa, hawawezi kulima na hawawezi kufanya shughuli zozote za maendeleo. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri washirikiane na Wizara ya TAMISEMI kama ikiwezekana zile GN zisogezwe ili wananchi wapate maeneo ya kulima na kufanya shughuli zao za kimaendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye Kata ya Itebula tuna eneo linaitwa Ipuguru. Eneo la Ipuguru ni hifadhi lakini kwa bahati nzuri hakuna wanyama wowote mle kwa zaidi ya miaka 20. Sasa kwenye maeneo kama hayo tungeomba basi hata wakulima waruhusiwe, lakini hata wafugaji pia waruhusiwe kutumia maeneo hayo. Wafugaji wamekuwa wanahangaika, wanaingiza mifugo yao kwenye mashamba, wanaingiza mifugo yao kwenye maeneo mbalimbali kwa sababu hakuna maeneo halisi ya kuchungia mifugo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tuna eneo la Kurora, nadhani Mheshimiwa Waziri analifahamu. Hili eneo lilitengwa kwa ajili ya matumizi bora ya ufugaji, lakini kwa bahati mbaya wakulima wamevamia na kusababisha wafugaji watoe mifugo yao na ianze kuhangaika kwenye mashamba. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha ajaribu kuangalia kwenye Wizara yake kuna maeneo mengi yanaitwa kama hifadhi lakini kwa bahati mbaya wananchi wameshavamia na vijiji vimeshasajiliwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa namsikia Mheshimiwa Magdalena Sakaya hapa anazungumza kwamba Tabora wana zaidi ya vijiji 50 vimesajiliwa kisheria ndani ya hifadhi. Tatizo hilo Mheshimiwa Waziri na sisi pia tunalo. Kwa mfano, sisi tuna ile Hifadhi ya Mahale ambayo ipo kwenye Kijiji cha Kalilani lakini Waziri anafahamu kuna mgogoro wa zaidi ya miaka 20 baina ya wananchi wa Kalilani na watu wa hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, huu mgogoro unapelekea mpaka watu wa hifadhi hata zile shughuli za kijamii za kuwachangia wananchi wa Kijiji cha Kalilani wanakuwa hawatekelezi na badala yake wanakwenda kusaidia vijiji vingine ambavyo havipakani na ile Hifadhi ya Mahale. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri aliangalie suala hili, ni mgogoro ambao uko ofisini kwa Mheshimiwa Waziri akiuliza ataambiwa. Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Kinana alipokuja tulimwambia na tulimkabidhi documents zote kwamba mgogoro baina ya wananchi wa Kijiji cha Kalilani na watu wa Hifadhi ya Mahale, tunaomba Mheshimiwa Waziri auangalie ili utatuliwe waweze kukaa kwa amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba pia nitoe shukrani kwa watu wa TANAPA kwa sababu sisi kwenye ile Hifadhi ya Mahale watalii wanapokuja wanatumia usafiri wa boti kwa sababu barabara hakuna. Tunazo kilometa kama 30 ambazo mtu hawezi kupita kwa gari na tuna mito kama mitatu ambayo inahitajika ijengewe madaraja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru watu wa TANAPA kwenye bajeti hii ya 2016/20167, wameweza kututengea shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kutengeneza barabara ile na tulipitisha kwenye kikao chetu cha barabara cha Mkoa wa Kigoma. Kwa hiyo, nimeona pia nitoe shukrani zangu za dhati maana wangeweza kupeleka sehemu nyingine, lakini wameona waje kusaidia ili watalii nao waweze kupita bila tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia Mheshimiwa Waziri aangalie sana kama inawezekana kuboresha zile speed boat za Mahale kwa sababu kwenye Ziwa Tanganyika tuna kitu kinaitwa Rukuga, ni upepo mkali sana, unapokuwa mkali hata meli ya Liemba haiwezi kupita. Hata kama sikuangalia kwenye bajeti kama wametenga namna yoyote ya kuboresha usafiri maeneo yale, naomba waone umuhimu wa kuwaongezea watu wa Mahale speed boat nyingine kwa ajili ya kubeba watalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichangie kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 32. Asubuhi mdogo wangu Mheshimiwa Doto alichangia kuhusiana na masuala ya unyanyasaji wa wafugaji kwenye hifadhi. Mimi nilikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Mbogwe ilizaliwa kutoka Bukombe, Mkoa mpya wa Geita. Matatizo hayo kwenye Hifadhi ya Kigosi wakati yametokea kwenye ile Operesheni Tokomeza, nilikuwa Mkuu wa Wilaya pale. Kwa kweli kabisa alichosema mdogo wangu ni kweli, unyanyasaji ni mkubwa sana. Wanapowakamata, hawawakamati tu kwamba wafuate sheria, sheria imewekwa kwamba watu wanapokamatwa wameingiza mifugo kwenye hifadhi wachukuliwe hatua gani. Wale maaskari badala ya kufanya hivyo wanawa-harass wale wananchi na wanawapiga risasi ng‟ombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge kwamba tuko hapa leo kuipitisha bajeti ya Wizara hii ya Maliasili na Utalii, tunatambua fika kwamba Mheshimiwa Waziri ndiyo kwanza amepewa dhamana kwenye hii Wizara na hii ndiyo bajeti yake ya kwanza. Kwa hiyo, badala ya kumshambulia au kum-attack moja kwa moja tumpe ushauri ili aweze kupokea, aangalie upungufu uliojitokeza kwenye Wizara yake siku za nyuma na aweze kuyafanyia kazi. Huu ndiyo ushauri ambao napenda kuutoa. Namfahamu Mheshimiwa Maghembe, najua ni mchapakazi na msikivu, yote haya tunayoyasema hapa atayasikia, atayapokea na atayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee tu kumtakia kila la kheri Mheshimiwa Waziri na nimwambie kwamba aangalie sana sekta ya wanyama pori. Wale maaskari wanaolinda hifadhi hizi wamekuwa ni shida kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niombe Mheshimiwa Waziri wa Maliasili kuna mambo mengine wawasiliane pia na Waziri wa Kilimo. Kwa mfano, haya matatizo ya mifugo kuvamia hifadhi na wakati Uvinza tunazo ranch za Serikali kama tatu lakini zile ranch inaonekana siku za nyuma walipewa watu ambao hawako tayari kuzitumia na badala yake wanazikodisha kwa pesa nyingi. Kwa hiyo, kwenye matatizo kama haya wakae chini Wizara na Wizara, kwa mfano Wizara ya TAMISEMI na Wizara hii waone matatizo hayo ya GN ambazo zimeingia mpaka kwa wananchi walikojenga waweze kusogeza ili kutatua migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.