Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Awali ya yote nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha jioni ya leo kusimama hapa. Jioni ya leo nataka kumshauri tu Mheshimiwa Waziri na kuishauri Serikali. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri awe makini, atulie bardan wasalaman, laa takhaf wa laa tahzan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hadithi ndogo wakati nasoma miaka ya 70, darasa la tatu kulikuwa na kitabu kidogo cha Kiswahili maarufu tukikiita Haji na Selele, kilikuwa na hadithi nyingi ndogondogo. Sasa tukisoma tukimaliza mwisho wake tunaulizwa hiyo hadithi imekufunza nini? Moja kati ya hadithi iliyokuwemo ni ile ya mtu aliyekuwa na kuku wake kila siku akitaga yai moja la dhahabu. Siku hiyo akaamua kumchinja ili apate mayai mengi ya dhahabu matokeo yake akakosa yote. Hadithi hii inatufunza nini? Tamaa nyingi mbaya. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza na-declare interest kwamba ni Mjumbe wa Kamati ya Wizara hii, lakini pia nimeshawahi kutumikia Idara ya Misitu na Utalii, kwa hiyo nazungumza kitu ambacho kinaelea katika kichwa changu, nakifahamu. Binafsi wakati nilipoteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati hii na nikakutana na viongozi wa Wizara nilieleza waziwazi baada ya taarifa kwamba sifurahishwi na TFS na nikawa na mashaka nayo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefarijika zaidi baada ya kupata semina na ile hofu yangu ikathibitishwa na mtaalam aliyebobea katika masuala ya misitu kwa utafiti wake alioufanya kwa muda wa miaka mitatu juu ya TFS. Nakushauri nini Mheshimiwa Waziri? Kwa sababu ameyakuta haya lakini kwa sasa yeye ndiye mwenye dhamana na Wizara hii, kwa hiyo, mwaka huu namshauri tu ila mwakani nitambadilikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, TFS ni nzuri katika ukusanyaji wa kodi lakini namwomba Mheshimiwa Waziri alinganishe sasa tunachokipata na athari tunayoipata, vinalingana? Misitu ya asili inapotea na itazidi kupotea na kwa mujibu wa mtaalam baada ya miaka 10 Tanzania hii itakuwa jangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niwakumbushe wale wanaokumbuka mwishoni mwa miaka ya 80, kazi kubwa tuliyoipata Watanzania na dunia kwa suala la HASHI na HADO kwa Mikoa ya Dodoma na Shinyanga ilivyokumbwa na janga la ukame, kazi iliyofanyika ndani na nje ya nchi. Binafsi nilifika Dodoma hapa kwa ajili ya kupanda miti kutokana na hali iliyokuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri aichambue TFS, aone udhaifu wake. Udhaifu wa TFS ni menejimenti, ni lazima ahakikishe kwamba anabadilisha, wanakusanya vizuri, wanapanda vizuri, lakini katika misitu ya asili suala la kuelekeza nguvu tu kwamba wakusanye kodi wanatumalizia misitu kitu ambacho kitakuja kuwa ni hatari kubwa kwa Taifa hili. Badala ya rehema hii misitu itakuja kuwa nakama kwetu, Mheshimiwa Waziri namshauri hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo hatuwezi kuwa na misitu endelevu, hatuwezi kuwa na misitu yenye tija, hatuwezi kuwa na misitu ambayo itatuletea faida sisi na kizazi chetu kama hatuna wataalam katika fani hiyo ya misitu. Leo nchi hii ina Chuo kimoja tu cha Misitu Olmotonyi, lakini Serikali imekitelekeza. Chuo kile kimekuwa kama yatima, hakina ruzuku yoyote kutoka Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri kile chuo kiangaliwe, kipewe ruzuku, kisimamiwe, kisomeshe wataalam wengi zaidi ili warudi katika misitu yetu ambayo iko chini ya Wizara, Halmashauri na Vijiji ili iwe ni misitu endelevu kwa faida yetu na faida ya kizazi kijacho. Huo ndiyo ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri kwa siku ya leo katika upande wa misitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye utalii. Amezungumza na kutoa ufafanuzi mkubwa juu ya nia yake ya kutoka kwenye watalii milioni moja na zaidi kwenda milioni tatu. Ni wazo zuri, tunaliunga mkono kwa sababu tunafahamu ongezeko la watalii litaleta faida gani kwenye nchi yetu, lakini lazima tujue tunataka aina gani ya watalii katika nchi yetu? Kwanza iwe ni kwa ajili ya kukuza mila na desturi zetu lakini wawe ni watalii wenye faida siyo watalii vishuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri, ili kupata watalii wazuri lakini kuwa na wawekezaji wazuri katika sekta ya utalii na kuondoa tofauti baina ya watalii, wawekezaji na jamii inayozunguka hivi vituo vya kitalii lazima kuwa na triangle ambayo itahusisha investors, Serikali na community.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutakapokuwa na triangle hiyo na wakawa pamoja na kujua mwekezaji anahitaji nini, Serikali inahitaji nini na jamii inahitaji nini, mkawa mnasimama katika kitu kimoja, mwekezaji akija hapa katika muda mfupi atakuwa amepata idhini ya kuwekeza lakini pia itakuwa uwekezaji huo una faida kwa sababu kila mmoja atakuwa anajua majukumu yake na yamepangwa yapo. Kwa hiyo, hilo namshauri Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa zaidi mtalii anachohitaji ni huduma. Inasikitisha unapokwenda katika hoteli zetu au katika vivutio vyetu vya kitalii kwa zile huduma zinazopatikana pale. Mtalii hahitaji jengo zuri ambalo labda lina ma-AC na kadhalika, anachohitaji hata kama ni kibanda cha nyasi lakini kiko katika kiwango gani? Je, tumeviweka katika viwango vile ambavyo wao wanavifurahia?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli watalii wanafurahia sana tradition yetu lakini je, watendaji wetu ambao wanafanya kazi hiyo, wanafanya kazi wakiwa na uweledi huo? Ndiyo maana katika Kamati nikakikamata sana Chuo kile cha Utalii, je, mnafundisha kulingana na mahitaji tunayoyahitaji ndani ya nchi yetu? Kwa hiyo, chuo kile kitoe wataalam ambao watakuwa ni wale wanaohitajika kulingana na mazingira yetu na matakwa yetu na lengo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ana mwaka mmoja wa kuondoa yale yote mabaya ambayo leo tunamwambia ambayo ameyakuta na mwakani hapa atakapokuja katika bajeti tuje tuone improvement. Kama ipo mimi tutakuwa pamoja, kama haipo Mheshimiwa Waziri kwa kweli mimi nitakuwa adui namba moja katika hili. Kwa sababu ninayoyazungumza nayazungumza nikiwa nayajua na najua kuna nini. Leo nazungumza tu hapa vizuri lakini siku nyingine nikiamua kuzungumza vibaya atakuja kuelewa kwamba kweli hiki kitu ninachokizungumza nakifahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunataka kile chuo kinachotoa vijana…
MWENYEKITI: Ahsante.