Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buhigwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba hii ya bajeti. Kwanza kabisa naomba nimpongeze Waziri na Naibu Waziri na timu yake kwa kuandaa hotuba nzuri ya bajeti yetu ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeisoma bajeti hii, naiona katika mambo yafuatayo:-
Kwanza, bajeti hii inajaribu kutuambia kwamba lazima watu wawajibike. Watu walioomba fedha kwenye Taasisi, Wizara, lazima wawajibike! Hata hivyo, nikiiangalia inajaribu kutuonesha kwamba nidhamu ya matumizi kwa walichopangiwa ni kitu muhimu sana. Pia inanionesha kwamba fedha zilizopangwa zinabadili mwelekeo kwa yale tuliyoyazoea na hatimaye kuwaza mambo mapya. Jambo la mwisho naiona kama inaenda kulenga maskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha nimesoma kitabu chake cha Hali ya Uchumi ukurasa wa 10 pale, kuna kitu amekisema kizuri sana pale. Hali ya umaskini; ametaja mikoa yeye mwenyewe kwamba kuna mikoa ambayo kipato chake ni kidogo. Mikoa mitano yenye umaskini mkubwa wa kipato ni Kigoma, asilimia 48.9, Geita asilimia 43.7, Kagera asilimia 39.3, Singida asilimia 38.2, Mwanza asilimia 35.3. Sasa nataka nimuulize; je, anafurahia kuitaja tu humu au ana mikakati gani aliyoipangia mikoa hii? Hii Mikoa ambayo anafurahia kuiandika kwenye vitabu vyake, kwenye bajeti ili aweze kuikomboa amepanga kitu gani? Hiyo ndiyo, ningependa atuambie.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu naangalia Mkoa wangu wa Kigoma, Mheshimiwa Waziri ameutaja kwamba ni maskini. Jimbo langu lina mgogoro na Serikali yake, vibanda 120 katika Kijiji cha Mnanila walijenga kwa kupewa ramani na Halmashauri yao, lakini TANROADS wakaja wakavunja na mpaka sasa wanawadai, kila kibanda milioni nane, jumla yake ni shilingi milioni 960, wamewafanya maskini, hawataki kuwalipa, lakini kuwaandika kwenye vitabu kwamba ni maskini wanapenda! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina wakulima 435, Waziri wa Kilimo yupo hapa Mwigulu Nchemba nimemwona, wamelima kahawa yao wameuza, wamepeleka kwenye vyama vyao vya ushirika ambavyo wamewapa leseni mpaka sasa wakulima hao tangu msimu uliopita fedha zao hawajalipwa. Bado anapenda awaandike kwamba hao watu wa Obama au watu wa Kigoma ni maskini na watu wanalima hawawapi hela zao! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kigoma katika mipango ya REA, Kigoma ni kati ya mikoa ambayo mpaka sasa hivi performance yake ni ndogo sana, ni Serikali yake hiyo anayoandika kitabu kwamba Kigoma wako nyuma na huku hawataki kuwapelekea fedha. Hivyo hivyo ukienda kwenye data za maji, ukienda kwenye pembejeo, Mkoa wa Kigoma tunapata pembejeo kidogo na zinakuja zimepitwa na wakati, lakini wanapenda watuandike kwamba sisi ni maskini! Kwa hiyo, hayo mambo mengine tunaomba mikakati ya kuokoa mikoa hii sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo hizi fedha milioni 50 ambazo mmesema, najua na nina uhakika, Mkoa wa Kigoma haujapangiwa kuanza na hizi fedha. Mnapeleka kule ambapo ni matajiri. Je, kama mnaionea hii mikoa kwa nini tusianze na hizi fedha zikaenda kwenye mikoa hiyo waliyoitaja? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili sikupendezwa nalo ni kuhusu madhehebu ya dini kwamba wanapoagiza vitu vyao walipie kodi kwanza halafu ndiyo waje wa claim! Tujue kwamba nature ya madhehebu yetu mengine yana shule, mengine yana hospitali na hawana fedha, kwa hiyo, ningeomba hilo mliangalie ili tusije kuwa na matatizo na madhehebu yetu ya dini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye pay as you earn, katika kitabu page 60, Rais alikubali kwamba pay as you earn itakuwa digit kutoka 11 kwenda tisa lakini ukiangalia ile schedule watumishi wa Serikali wanaonufaika na hiyo asilimia tisa ni wachache sana kwa sababu inatakiwa uwe chini ya 170,000. Kwa hiyo, watumishi kule wanafurahia kwamba Serikali imepunguza lakini digit za pale juu ni kuanzia asilimia 20, asilimia 25 mpaka asilimia 30, kwa hiyo kile kilio cha watumishi wengi hata Walimu wanaokuwa wanafurahia hakitaweza kuwafaidisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mengine tumeandika kwenye hotuba yetu ya Kamati ya Bajeti, nami nilikuwa sehemu ya Kamati, sina mengi ya kusema nilitaka nimkumbushe Waziri kuhusu hiyo mikoa maskini anayoisema ana mikakati nayo ipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.