Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Zaynab Matitu Vulu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ZAYNABU M. VULLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Kwa sababu hii ni mara yangu ya kwanza kwa ruksa yako, niwashukuru wapiga kura wote wa Mkoa wa Pwani wakiongozwa na wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli pamoja na Baraza lake la Mawaziri. Mheshimiwa Rais wewe endelea na kuchapa kazi kama kaulimbiu yako ulioitoa ya “Hapa Kazi Tu” haya maneno ya humu ndani ni sawa na wimbi la baharini, Waswahili sisi kule baharini tunasema wimbi la nyuma halimsumbui wala halimkeri mvuvi, kwa hiyo ya nyuma yamepita sisi tusonge mbele, tuchape kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nijikite kwenye mpango ambao tunao mbele yetu. Mpango huu unauzungumzia ujenzi wa uchumi. Nianze kwa kuipongeza Serikali kuwa na uamuzi wa kufanya elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari na chekechea yake lakini nitoe msisitizo tunaposema elimu bure tusaidie kutengeneza mazingira bora. Kwenye Mpango haikugusa maeneo ambayo yatamfanya Mwalimu, yatamsaidia Mwalimu kuweza kufanya kazi zake kwa amani zaidi ya hivi sasa anavyofanya. Majengo, Nyumba za Walimu, miundombinu na mambo mengine yale muhimu kwa ajili ya kuendeleza elimu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ndiyo itakayotusaidia kuinua uchumi wetu na hasa huo uchumi wa viwanda tunaouzungumzia. Kuna masomo ya sanaa na masomo ya sayansi, tunapozungumzia masomo ya sayansi ndipo tutakapopata wataalam wa viwanda, sasa hivi tujikite katika kujenga vyuo vya VETA, kupeleka wanafunzi wengi, ili waweze kuajiriwa maeneo mbalimbali katika viwanda vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi ni vipi Mpango umemuangalia mwanamke katika kuinua uchumi wa viwanda, ni vipi mwanamke atashirikishwa, ni vipi umeme utaweza kusaidia kwenda kijijini ili mwanamke au gesi itakavyoweza kusaidia inayotoka Mtwara ifike mpaka kijijini ili mwanamke yule apungukiwe na mzigo wa kutafuta kuni, apungukiwe na mzigo wa kuhangaika na mambo mengine, aweze kwenda kushiriki katika kazi za kuinua uchumi katika, katika kuajiriwa kwenye viwanda, hata kuweza kuwa na viwanda vyao wenyewe wanawake kama Serikali ilivyotuwezesha kuwa na Benki yetu ya Wanawake kuwa na Benki ya Kilimo. Hayo ndiyo mambo ninayoomba mimi, huu Mpango uangalie na uende ukarekebishe tuone hayo yatafanywaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka kumkomboa mwanamke aweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi, tuangalie na mazingira ya mtoto wa kike toka anasoma chekechea. Watu wamegusia suala la maji humu ndani, maji ni msingi unaoweza kuleta maendeleo katika nyanja zote, lakini maji hayo kama hayatofika kila mahali na kwa wakati, kuna udumazi wa maendeleo utakaotokea na kuwanyima wengine haki ya kuweza kwenda kujiendeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa maana kwamba tunahitaji uvunaji wa maji mashuleni, uwezo wa kuchimba visima kama water table iko chini sana basi itengenezwe miundombinu ya kuvuna maji ya mvua. Mahitaji ya maji ya mtoto wa kike au ya mwanamke ni makubwa zaidi ya wanaume, tunahitaji watoto wa kike wawekewe utaratibu, wanapewa pesa za kuwasaidia lakini wawekewe na utaratibu wa kupewa mataulo ya kike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa wa Jimbo la Ludewa Mjini aliyeguswa na maendeleo na mahitaji makubwa ya mtoto wa kike. Nakushukuru sana na nakupongeza, wanawake wote tunasema tuko pamoja na wewe na tumekutaja leo kwenye vikao vyetu tutakushirikisha ili uone tutasaidiaje watoto wa kike katika kuleta maendeleo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wa Serikali kutoa misaada. Mtoto wa kike anaweza asiende siku saba shule, yuko nyumbani, mama anahitaji maji zaidi ya baba, anahitaji ndoo tatu, nne kwa siku. Leo hii kama mama hapati maji ya kutosha hawezi kwenda kushiriki kwenye uchumi, kwa hiyo suala la maji ni suala la kuwekea msisitizo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye suala la gesi. Naipongeza Serikali kwa juhudi iliyofanya, gesi inatoka Mtwara imefika Dar es Salaam mpango haukueleza, katika Mkoa wetu wa Pwani inapoanzia Rufiji watu watanufaika vipi! Tunahitaji gesi ile ipate manufaa Wilaya ya Rufiji, Wilaya ya Mkuranga, Wilaya ya Kisarawe, Wilaya za Kibaha, Bagamoyo, ambako pia nako kuna uwezekano pamoja na Mkuranga kupata gesi tuone tutafaidika vipi, viwanda vingapi tumeandaliwa kuletewa, gesi imekuja, tunawaambia watu wasikate mkaa, watu wamezoea kukata mkaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam yote inalishwa mkaa unaotoka Pwani, sasa Mpango huu unaelezaje, gesi hii imeandaliwa vipi na Serikali ili wale wakataji wa mkaa waweze kunufaika na biashara yao wakaacha, misitu yetu ikarudi pale pale. Sasa hivi misitu imekuwa kama vipara, eeh unakwenda unakuta pembeni kuna miti lakini ukienda katikati miti hakuna. Mama anahangaika kutafuta kuni asubuhi mpaka jioni. Watani zangu kule Usukumani miti yote imekwisha matokeo yake wanatumia mavi ya ng‟ombe. Kwa hiyo, niwaombe, ufanywe utaratibu Serikali ihakikishe gesi na umeme inafika kwa watu wote ili kuleta maendeleo ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wangu mniwie radhi nasema ukweli wa maisha. Niseme kwamba suala la maendeleo katika Wilaya ya Mkoa wa Pwani, naomba tuliangalie sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Rufiji. Rufiji watu wameanza ujasiriamali, wanachonga vitanda lakini ushuru wa kitanda ni laki moja na ishirini. Huyo muuzaji atanunua hicho kitanda kiasi gani? Ushuru wa mkaa umepanda asilimia moja na kumi na nne, huyo mwananchi anayekata miti na mbao anafanya biashara ya kujisaidia ataendelea vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Nyamwage mpaka Utete na Utete ndiyo kuna hospitali ya Wilaya, tunatarajia watu watolewe Utete wapelekwe kwenye hospitali ya Wilaya Kibaha, barabara mbaya, Wilaya ile ni miongoni mwa Wilaya kongwe katika nchi hii, mpaka leo hii hatujaiona lami. Tunaomba suala hilo liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika twende Mafia. Kuna barabara inaanza Kilindoni hadi Bweni haina lami, lakini pia Mafia kuna utalii, naomba Serikali kupitia Wizara ya Utalii, hebu ijaribu kuangalia ni vipi watainua wilaya ile na kuifanya wilaya ya kiutalii. Watalii wengi sana wanakwenda, tunashukuru, gati limejengwa tunangoja tishari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuu uwanja wa ndege umejengwa tunasubiri taa ziwekwe, watalii waingie asubuhi na jioni hali kadhalika na wananchi waingie asubuhi na jioni. Hata hivyo, bado tuna tatizo la hospitali zetu, Wilaya zetu za Mkoa wa Pwani, zimepakana na Mkoa wa Dar es Salaam, lakini kwenye vituo vya afya na zahanati na hospitali za Wilaya...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge muda wako umekwisha!
MHE. ZAYNAB M. VULLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.