Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigamboni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa nami nichangie katika bajeti kuu. Nianze kwa kusema kwamba kauli mbiu ya bajeti hii naikubali ambayo imelenga kuongeza uzalishaji viwandani na kupanua fursa kwa ajira. Niseme tu kwamba nasi kama Jimbo la Kigamboni tumeshajipanga vizuri, tayari tumeshapima ekari 1,000 na tumetoa viwanja vipatavyo 461 vya viwanda ambavyo viko tayari kwa uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niseme tu kwamba bajeti hii mwelekeo wake ni mzuri, kutoka asilimia 26 mpaka asilimia 40 ya fedha za ndani kutengwa katika kuelekea katika bajeti ya maendeleo, ni jambo jema. Jambo jema lingine ni kupunguza utegemezi kwa wahisani.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna changamoto ambazo nami naziona. Pamoja na juhudi ambazo zinaendelea za kuongeza ukusanyaji wa kodi za ndani, bado tuna changamoto ya wigo wa kukusanya kodi, kwa maana ya tax base, hilo bado ni tatizo kubwa sana. Bado naona tunaendelea kuvikamua vyanzo vile vile ambavyo tumekuwa tunavitumia siku zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali kwamba sasa hivi inabidi tuangalie na vyanzo vingine. Sekta ya Kilimo, Uvuvi pamoja na Utalii vinaweza vikachangia kwa kiasi kikubwa. Tuweke pesa ili tupate pesa. Kwa hiyo, nataka kuishauri Serikali ijaribu sasa kuangalia vyanzo vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kushauri ni kuhusiana na matumizi makubwa ndani ya Serikali. Tunaziona juhudi ambazo mnazifanya katika kupunguza matumizi ya Serikali. Asilimia 49.5 ya mapato ya ndani yote yanaenda kwenye mishahara. Hii ni gharama kubwa sana. Ni lazima sasa mwangalie upya ndani ya Serikali, kuangalia reforms za kuboresha ufanisi lakini na kupunguza gharama ambazo zinaingia katika masuala ya mshahara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuangalie tena maeneo mengine ambayo tunaweza tukapunguza matumizi makubwa. Katika eneo la ununuzi wa magari, matumizi ya magari ya Serikali bado ni mbovu. Tunayanunua magari kwa gharama kubwa. Ni muda muafaka sasa kuweka sera nzuri ya ununuzi, matumizi na matengenezo ya magari ya Serikali; yanatumia gharama kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka kuchangia ni ushirikishwaji wa sekta binafsi. Tuna Sheria nzuri ya PPP na sera nzuri sana ya PPP; lakini ukiangalia katika hotuba hii ya bajeti kwa kiasi kikubwa sana, miradi yote mikubwa tunategemea sana Serikali kwenda kukopa fedha kwa ajili ya kuendesha hiyo miradi. Kwa nini tusi-engage sekta binafsi tuka-freeup some resources kwa ajili ya huduma nyingine za jamii kama afya, elimu na maji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Serikali ijaribu kuangalia hii, miradi mingine kuna watu wana fedha zao, tuwashirikishe ili hizo fedha nyingine tuweze kuziokoa kwa ajili ya mambo mengine katika huduma za jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nilikuwa nataka kuchangia ni concern. Sisi kama Bunge jukumu letu ni kupitisha bajeti ya Serikali. Nilipokuwa nasoma hotuba ya Kamati ya Bajeti, imenishtusha kidogo kuona kwamba Serikali inatumia fedha kupita kile kiwango ambacho kimeidhinishwa na Bunge, hilo ni kosa. Tuanze sasa kujenga msingi wa Serikali kuheshimu maazimio na zile idhini ambazo zimepitishwa na Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupeleka fedha asilimia 140, 120, 150 zaidi ya zile zilizopitishwa na Bunge bila kuleta maombi hayo Bungeni ni kuvunja sheria na kuvunja Katiba. Kwa hiyo, lazima sasa tufike mahali turudi kwenye ile misingi ya matumizi ya fedha ya Serikali na nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali izingatiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulichangia ni hususan ushirikishwaji wa Kamati ya Bajeti. Kamati ya Bajeti inafanya kazi kwa niaba ya Bunge. Serikali ione kuwa, wanapofanya kazi na Kamati ya Bajeti, wanafanya kazi na Bunge. Ni muhimu sana wakawashirikisha. Bajeti itakuwa nyepesi kama Kamati ya Bajeti itakuwa imeridhia kwa niaba yetu sisi. Sasa Serikali inapokuwa inaleta bajeti na vitu vingine havijapitishwa katika Kamati ya Bajeti mnaifanya kazi ya kujadili na kupitisha bajeti inakuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba sana Serikali, Bunge linaweza likawa rafiki pale mnapokuwa mnatoa ushirikiano kwa Bunge, lakini kazi inaweza ikawa ngumu pale mnapokuwa hamuwashirikishi Wabunge kikamilifu. Sasa nawaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, msiwaone Kamati ya Bajeti kwamba wale ni maadui, wale ni marafiki zenu na wako pale kwa niaba yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema, nami nataka kugusa suala la kiinua mgongo kwa Waheshimiwa Wabunge na nataka Mheshimiwa Waziri wa Fedha naye ajaribu kunisaidia, nini hasa lengo la kuiweka hoja hii katika bajeti yake? Kwa sababu Bunge letu hili ndiyo limeanza 2015 litakwisha 2020; unapoliweka hili suala la kukata kodi katika kiinua mgongo, lengo lake ni nini? Ama ilikuwa kama hivyo alivyokuwa anasema Mheshimiwa Kangi Lugola, kuwa-beep Waheshimiwa Wabunge?
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme, huwezi ukaleta usawa katika kupofua wenzako. Kama kuna watu vipofu nawe ukawapofua wengine ili wote tuwe sawa, nadhani hiyo siyo mantiki sahihi. Suala kubwa la msingi hapa, kama tunaongelea masuala ya kiinua mgongo, lets cut across board. We should not single out a single group. Kwa hiyo, hili nataka niliseme kwa Mheshimiwa Waziri ili liweze kueleweka. Maana yake unapokuwa na single out a single group, inaleta mashaka kuhusu dhamira ya lengo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, nakushukuru sana.