Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Madaba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nakushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi. Pili, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa uwasilishi wake mzuri. Pamoja na kazi nzuri aliyoifanya Mheshimiwa Waziri nina mambo mawili, matatu ya kuishauri hii Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, unajua habari ya viwanda Tanzania siyo habari ngeni. Tumekuwa na viwanda miaka ya 80 kuelekea miaka ya 90 na viwanda vingi vimekufa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri, sehemu pekee au mkakati pekee ambao ameuweka ambao umeonekana wa namna ya kulinda viwanda vya ndani ni kuongeza kodi kwenye bidhaa zinazotoka nje, zile bidhaa ambazo tunaweza kuzizalisha ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maoni yangu huo ni mkakati mzuri, lakini mkakati huu pekee hautatosha kulinda viwanda vya mafuta ya kula, hautatosha kulinda viwanda vya sukari nchini, hautatosha kulinda viwanda vya nguo nchini. kwa sababu kikwazo cha viwanda vya Tanzania siyo tu ushindani wa bei za bidhaa zinazoingia, bali pia mikataba ambayo tunaingia na nchi marafiki ambao tunafanya nao biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vyovyote vile, mikataba ile bado inatubana. Pengine hata kuweka hizo kodi kwenye hizo bidhaa huenda tukagomewa na wadau marafiki tunaofanya nao biashara kwa sababu na wao wanataka kulinda viwanda vyao. Kwa hiyo, naishauri Wizara ya Fedha ifanye kazi ya kina. Mwezi wa Pili nilitoa ushauri huu na sasa narudia tena kwa sababu mpaka sasa sijaona assessment ya kutosha ya ku-assess kwa nini tulifeli miaka ya 1980 na 1990 na kwa nini tunadhani tutafaulu katika kipindi hiki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, ni suala zima la maji. Sera ya Taifa inatutaka Watanzania wote popote walipo waweze kupata maji katika umbali usiozidi mita 400. Ukiiangalia sera hii na mpango mkakati uliowekwa na Wizara ya Fedha, havifanani kabisa. Kukata sh. 50/= kwenye mafuta ya petrol na diesel pekee, havitoshi. Kamati ya Bajeti imeshauri tuweke angalau sh. 100/= na baadhi ya Wabunge wameshauri tuweke angalau sh. 100/=. Nami naomba tuweke angalau sh. 100/= ili tuweze kusogea mbele kwa haraka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Madaba ni moja katika Majimbo ambayo yana tabu sana ya maji. Hivi ninavyoongea, Kijiji cha Lilondo na Maweso toka miradi imeanza mwaka 2015, haijakamilika na Wakandarasi bado wanahangaika kulipwa. Naishukuru Wizara ya Maji, tunawasiliana kwa jambo hili, lakini huu ni ushahidi kwamba kuna matatizo ya kutosha kwenye hili eneo, tulitengee bajeti ya kutosha kwa kuzingatia ushauri wa Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ni ombi kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango avae viatu vya Walimu wa Sekondari na Shule za Msingi ambao katika uhai wao wote wanalitumikia Taifa hili, mishahara yao inakatwa kodi na wanapomaliza kipindi cha utumishi wanalipwa kiinua mgongo na kinakatwa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri avae viatu vya watumishi wengine wa Serikali na Sekta ya Umma ambao mishahara yao ni ya chini, wanakatwa kodi, wanafanya kazi, lakini wanapomaliza utumishi wao, bado kiinua mgogo kinakatwa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lililopita lilienda hatua mbele, likaiomba Serikali iondoe kodi kwenye hivi viinua mgongo, yaani kwenye mafao ya wafanyakazi. Nilitegemea Wizara ya Fedha ije na mkakati huo sasa wa kuondoa hizo kodi kwenye mafao ya wafanyakazi na kupendekeza njia mbadala ya kupata fedha kwa ajili ya kuendeshea Serikali, kwa sababu hawa wafanyakazi wameendelea kukatwa kodi wakati wote. Kilichonishangaza, tunazidi kurudi nyuma. Tulishapiga hatua mbili mbele, tunarudi hatua nne nyuma, tunaanza sasa kufikiria kukata kodi kwenye mafao ya Wabunge. Tunakwenda wapi? Tutafika lini tunakotaka kwenda kuwatengenezea Watanzania maisha bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri avae viatu vya Wabunge wanaotoka katika Majimbo yenye changamoto kama Jimbo la Madaba. Mbunge wa Madaba akishapata posho humu Bungeni, anakwenda kununua solar kuweka kwenye Vituo vya Afya. Anakwenda kuchangia maji Matetereka ili wananchi wapate maji kwa sababu Serikali bado haijaweza kufikia wananchi hao.…
Nasikitika sana ninapoambiwa kwamba...
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja.