Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia bajeti. Kwanza kabisa, naomba niipongeze bajeti yetu, bajeti nzuri, naomba niiunge mkono kabla sijaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niipongeze Serikali yangu sikivu kwa kututengenezea barabara ambayo ilikuwa inasumbua sana wananchi wa Mpanda; Mpanda – Tabora kwenye Daraja la Ipole. Lile daraja sasa hivi limekwisha. Nomba tu Serikali yangu basi itoe kauli hilo daraja liweze kufunguliwa ili wananchi wa Mpanda sasa waweze kupata maisha mazuri, waweze kufanya biashara zao na kufanya shughuli zao kwa amani kwa sababu daraja lile la Ipole lilikuwa ni kikwazo, walikuwa hawawezi kusafiri, walikuwa wanazunguka mwendo mrefu. Naomba Kauli ya Serikali kwa ajili ya daraja hilo, kwa kuwa limekwisha ili tuweze kupata manufaa ndani ya maisha ya wananchi wa Mpanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba kuchangia bajeti hii kwa upande wa akinamama. Kwa kuwa mimi ni Mbunge wa akinamama, nianze na akinamama. Asilimia tano ya akinamama mara nyingi tunaitenga lakini akinamama hawaipati kutokana na Halmashauri zetu kwamba hazina uwezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi ukiangalia, makusanyo mengi yameingia Serikali Kuu, ina maana TRA ndiyo watakusanya. Ina maana Halmashauri watakuwa hawana kipato cha kuwapa akinamama pamoja na vijana zile asilimia tano. Sasa sijui Serikali itafanyaje kwa sababu akinamama wengi sasa hivi wameshapata mwamko, ni wajasiriamali. Nanyi wenyewe mnaona sasa hivi hata mkienda vijijini mnakuta akinamama wengi ni wajasiriamali kutokana na juhudi nzuri za Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Sasa tunaomba hii asilimia tano iliyowekwa na hivi vigezo ambavyo viliwekwa, hela nyingi zimechukuliwa Halmashauri, akinamama hawa wajasiriamali watapataje mikopo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata sasa hivi kupata hiyo asilimia tano kwenye Halmashauri zetu ni shida. Sasa naomba Serikali yangu sikivu kwa bajeti hii ione ni jinsi gani ya kuweza kutenga au kutafuta ili hawa akinamama waweze kupata asilimia tano ili waweze kufaidika na Serikali yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye upande wa maji. Hakuna kitu kigumu na shida katika maeneo yetu kama maji. Nikiangalia, Wilaya yangu ya Mpanda kuna vyanzo ambavyo Serikali ilifanya jitihada kubwa, lakini unakuta miradi ile haiishi na ile bajeti inayopangwa haiendi kwa wakati ile miradi ikaisha.
Sasa sijui bajeti hii ambayo imekuja mbele yetu, itaweza kukamilisha miradi ile ya maji na wananchi waweze kupata kwa urahisi na wepesi zaidi. Hususan Wilaya ya Mpanda, kuna mradi wa Ikorongo One; bajeti ya mwaka 2015 mkatupangia kuwa mtatupatia shilingi bilioni nne, lakini zile pesa hazikuweza kupatikana. Matokeo Wilaya ya Mpanda Mjini, Manispaa, maeneo mengi maji ni shida. Yaani maji yale yakipatikana leo, kesho hawapati; au wanaweza wakakaa siku tatu ndiyo wanapata maji. Maeneo mengine kama Makanyagio, Ilembo, hakuna maji kabisa, ni shida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba basi, hii bajeti ya safari hii, miradi ambayo inaelekezwa, iweze kukamilika ili wananchi waweze kupata maji safi na salama. Nafikiri na Waziri alivyotusomea bajeti yake, alisema sasa ni kipindi cha akinamama kufurahi; anawatua ndoo. Sasa naomba basi akinamama hususan wa Mpanda Vijijini, kuna vijiji havina maji kabisa wala havina miradi kabisa. Akinamama wanapata shida sana. Naomba bajeti hii iweze kutimiza yale malengo waliyoyataja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya ardhi ni mikubwa mno. Ukiangalia kama Wilaya yangu ya Mpanda, Kata ya Ilembo ni shida. Naiomba Serikali sasa kupitia bajeti hii, migogoro hii ya ardhi iweze kwisha. Tunaomba bajeti hii ambayo leo tunaisema hapa ifanye kazi kama mlivyoileta mbele yetu, kwa sababu, migogoro ya ardhi haiishi. Kwa nini haiishi? Mimi nashangaa kila siku, kwa nini haiishi? Lazima sasa bajeti hii ambayo tunaichangia hapa, tunaomba migogoro ya ardhi kupitia bajeti hii, iishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vijijini mwetu wanavijiji wanavaa mitumba na ndiyo nguo rahisi walizozizoea, ndiyo maana ukienda sasa hivi vijijini unawakuta akinamama wengi ni wasafi kutokana na mitumba. Leo sisi bado viwanda vya kutengeneza malighafi ya nguo havijafika, lakini leo tumeipandishia mitumba ushuru mkubwa, ina maana wale wananchi wa vijijini washindwe kuvaa kabisa?
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kuhusu mitumba iangalie upya, watoe ushuru wa mitumba kwa sababu wananchi wetu ndiyo mavazi yao wanayayategemea kuliko kitu kingine chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.