Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon Faida Mohammed Bakar

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia hoja hii ya bajeti yetu kuu. Naunga mkono hoja mia kwa mia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza kupeleka pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri. Mimi namwita Mheshimiwa Waziri wa Mipango; huyu jina lake Mpango, kwa hiyo ana mipango mingi. Mheshimiwa Naibu Waziri, dada yangu au mdogo wangu, huyu ana jina gumu sana huyu! Ashatu, sijui jina la Kichina hili au la wapi, sielewi lakini Ashatu ni jina zuri sana, nafikiri la kihindi. Napenda kumpongeza kwa ushirikiano mzuri wa kazi. Wanashirikiana, wanafanya kazi na inaonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda moja kwa moja kwenye hoja. Suala la maji limezungumzwa sana na kweli Serikali yetu inajitahidi sana katika kusaidia huduma za maji mijini na vijijini; lakini tukiangalia sana vijijini maji yanayotegemewa sana ni ya visima. Sasa maji yaliyoko vijijini hasa ya visima, visima vingi vinakuwa havitoi maji. Tunaomba sana, watu hawa wa vijijini hususan wanawake, sisi wanawake ambao tunahangaika sana, tunatoka usiku wa manane kwenda kutafuta maji masafa marefu na inafikia wengine hata kuachwa na waume zao kutokana na matatizo haya ya maji. Hebu tuwaondolee matatizo haya ya maji wanawake hasa wa vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi katika kutekeleza ilani yake ya 2015 hadi 2020 inatekeleza vizuri sana kujenga zahanati vijijini na mijini, lakini ukiangalia zahanati nyingi hazina vifaa. Akinamama wengi ambao wanakwenda kujifungua wanaambiwa wabebe ndoo, kanga, nyuzi, mikasi na viwembe. Huu ni udhalilishaji wa wanawake. Naomba sana Serikali ilione hilo na ilipe kipaumbele mambo ya zahanati na vifaa, siyo iwe zahanati tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zile zahanati ambazo zimejengwa na ambazo hazijamalizwa, zimalizike, siyo kutenga tena bajeti mpya ya kujenga zahanati nyingine ambapo zile za zamani zilizokuwa zimejengwa hazijamalizwa na vile vile vifaa hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunaishukuru Serikali yetu kutenga shilingi milioni 50 za vijijini, mitaa na kule Zanzibar tunaita shehia. Fedha hizi kwa kifupi ni nyingi sana. Serikali yetu imetenga fedha nyingi sana, lakini je, tujiulize, matumizi yake yatakwenda sawia? Sisi ni mashahidi kuona kwamba fedha za Mheshimiwa Jakaya Kikwete vilivyoteketea na fedha za TASAF zinavyoteketea. Je, hizi fedha shilingi milioni 50 za vijiji, shehia ya mitaa zitakwenda kutekeleza majukumu ya kuondolea wananchi umaskini zinatumika vizuri?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali iangalie sana suala hili ili wanaohusika walisimamie vizuri tukiwemo na sisi Wabunge, maana na sisi tusijitoe, tumo katika utekelezaji wa majukumu ya shilingi milioni 50. Asilimia tano hizi za kwenda Halmashauri za vijana na wanawake ni siku nyingi tu, ni miaka mingi zinatengwa na zinaonekana katika makaratasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kamati ya PAC na zamani nilikuwa LAAC, tulikuwa tunaziona, lakini fedha hizi hazitumiki vizuri kule. Fedha watu wanatumia vibaya, sijui wanazifanyia nini kusema ukweli. Ukitazama hesabu, haziendani na wanawake hawa na vijana huwa hawapatiwi fedha hizi. Naishukuru sana Serikali kutenga hilo lakini tunaomba sana Serikali yetu iwe simamizi sana ya fedha hizi za asilimia tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, wengi wameongelea watoto wetu wa kike. Watoto wetu wa kike ni watoto ambao wanataka hifadhi kubwa sana; hivi ni kwa nini hizi pad siziwe free? Hizi taulo za watoto wa kike! Mtoto wa kike siku zake zikifika anaomba dunia ipasuke aingie; mtoto mama yake maskini, baba yake maskini, fedha ya kununulia taulo hana. Mtoto anabakia haendi shule siku saba au siku nane. Hii hatuioni kama ni muafaka?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana, tuko chini ya miguu yenu Serikali, mwondoe VAT ili watoto hawa wapate kusitirika. Watoto wetu wa kike wanapata shida sana; wakati mwingine wanafeli madarasani kutokana na tatizo hili. Tatizo hili katujalia Mwenyezi Mungu, hatukulitaka wenyewe; watoto wetu hawakulitaka wenyewe. Wanaume hawana hili. Kwa hiyo, tunaomba na Waheshimiwa Wabunge wanaume wakichangia hapa watetee hili ili watoto wetu waweze kuhifadhika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, naomba kuunga mkono hoja.