Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa fursa hii. Kwanza, niombe tu Mheshimiwa Waziri anisikilize kwa makini kwenye suala hili ambalo nataka nilizungumze sasa hivi. Niunge mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwenye kipengele cha mabaki ya mjusi ambayo yapo Ujerumani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo hapa, kuna mabaki ya mjusi ambayo yalichukuliwa katika eneo la Tendenguru, Jimbo la Mchinga ambako mimi ndiyo Mbunge wao, Halmashauri ya Wilaya ya Lindi kupelekwa Ujerumani. Dinosaur huyu ndiyo mjusi mkubwa kuwahi kuishi katika dunia hii tuliyonayo, anatengeneza historia kubwa kwa nchi yetu. Mungu hakufanya makosa mjusi huyu kupatikana katika ardhi ya Tanzania, unfortunately alichukuliwa akapelekwa Ujerumani. Hivi sasa ninavyowaambia mabaki yake yapo pale Ujerumani, watalii maelfu kwa maelfu wanakwenda kuangalia pale Serikali ya Ujerumani inapata pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi kifupi nilichokuwa Mbunge wa Jimbo la Mchinga nimekwenda Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambako nilielekezwa kwamba wao ndiyo wanalishughulikia suala hilo. Mheshimiwa Waziri jioni nitamletea barua niliyojibiwa na Katibu wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, majibu yake yanasikitisha Mheshimiwa Waziri. Hapa kwa sababu Mnadhimu alikuwa amesema kwamba nichangie jioni ningekuwa nayo hapa lakini jioni nitaileta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira ya kusikitisha na ambayo sikutarajia Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ananijibu kwamba mpaka sasa Serikali inafanya calculation kujua huyu mjusi anaingiza kiasi gani kwa mwaka, this is very shameful. Mwaka 1907 alipochukuliwa, Tanzania imepata uhuru mwaka 1961 mpaka hivi sasa hatujui mjusi huyu anaingiza kiasi gani Ujerumani, this is very shameful. Ananijibu kwamba Wizara inaendelea kuhakikisha inafanya calculation kujua kwa mwaka inapata shilingi ngapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira mengine ya kusikitisha wiki mbili mbele wananitumia tena barua nyingine ya majibu wakijibu barua yangu hiyo moja, imepata barua mbili za majibu kwamba sasa Serikali ya Tanzania imeshirikiana na Serikali ya Ujerumani kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo ndiyo Wizara hii kwamba waanzishe ushirikiano na mahusiano ya utunzaji wa mambo ya kale. Hii ina maana kwamba mahusiano yatatengenezwa kati ya Ujerumani na Tanzania ili kuhakikisha kwamba Tanzania inanufaika kutokana na mjusi yule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili la aibu. Alikuwepo Mbunge wa Jimbo la Mchinga Mheshimiwa Mudhihir Mohamed Mudhihir, alizungumza sana juu ya suala la mjusi mpaka amemaliza kipindi chake hakuna majibu. Haya mama Fatma Mikidadi akapewa jina kabisa kwamba mama mjusi, Mbunge wa Viti Maalum amezungumza mpaka mkambatiza jina la mama mjusi, chwee majibu hakuna. Bi. Riziki Lulida miaka kumi huu sasa mwaka wa 11 anazungumzia suala hilo la mjusi majibu hakuna. Mimi Mbunge wa Jimbo la Mchinga leo nazungumza suala la mjusi na nitatoka hivi miaka mitano chwee majibu hakuna. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Waziri jambo moja, kama kuna suala ambalo lilinipa Ubunge na mkimuuliza Mbunge niliyemtoa Mtanda atawaambia wananchi hawataki kusikia juu ya suala lolote kuhusu mjusi, wananchi wa Jimbo la Mchinga hawaitaki CCM kwa sababu ya suala la mjusi, nawaambia kabisa. Mheshimiwa Magufuli Rais wetu wakati yupo kwenye kampeni alivyofika Mchinga aliwekewa mabango bring back our dinosaur.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Magufuli kwenye mkutano pale Nangalu, waliokuwa wanatembea na mgombea wa Urais watawaambia, Mheshimiwa Nape angekuwepo angesema hapa, alisema pale Nangalu kwamba najua tunapoteza fedha za mjusi huyu hatutaweza kumrejesha lakini nitahakikisha kwamba fedha za mjusi zinarudi katika Serikali ya Tanzania na kuletwa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi kuja kutatua kero ndogondogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa mgombea wa Urais ambaye sasa ndiye Rais kwa hii ahadi yake aliyowaahidi wana Mchinga wanaisemaje? Ahadi aliyowaahidi Watanzania kwamba pesa za mjusi zitapatikana inakuwaje? Inakuwaje sisi Tanzania hatuthamini mali zetu kwa nini? Kwani Mungu mwenyewe alivyoamua huyu mjusi apatikane Tanzania unadhani alifanya makosa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Waziri atakapokuja kufanya majumuisho ya hoja suala la mjusi alizungumzie. Namwambia kabisa Waziri asipozungumza juu ya suala hili nakamata mshahara wake, tunahitaji majibu ya kutosha juu ya masuala ya mjusi. Kwanza atakuwa anatunasua sisi kutokana na aibu, wenzetu watu wa Kenya wakitangaza Mlima Kilimanjaro, mnalalamika leo watu wa Kenya wala hawasemi kwamba mjusi anatoka kwao wamekubali kwamba mjusi anatoka Tanzania, anatoka huko huko kwetu lakini wao kuchukua kwamba huyu ni wa kwetu hawataki, tatizo nini? Kama kuna mtu anapata maslahi ndiyo anatukwamisha wamtaje kwamba labda kuna mtu anapata maslahi juu ya hili ili watu tujue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu suala la ndovu kuvamia kwenye Jimbo langu la Mchinga. Kwanza Mheshimiwa Waziri nimpongeze sana mzee wangu ametusaidia vya kutosha, Serikali yake imehakikisha kwamba kila ndovu wanapovamia mashamba ya wakulima wangu wanakuja kuwafukuza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Mchinga wastaarabu sana, ndovu wanatembea kwenye vijiji vyangu vile yaani kama mbuzi tu na wanakotoka mbali. Kutoka Selou kuja Mchinga ni zaidi ya kilometa 180, wanakuja wanakaa kule siku 20 - 30 lakini hakuna tembo amepigwa au hawaendi, wale wananchi wakichukua hasira baadaye wakaamua kuwapiga watawalaumu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amenisaidia sana kila walipokuwa wanakuja alikuwa anapeleka askari kwa hili namshukuru na kumpongeza lakini isiishie pale. Yale mashamba ekari 183 za wananchi wale ambazo wamelima kipindi chote cha miezi sita (6), akinamama maskini wale, watu maskini wale, mtu amelima shamba lake la mihogo lote limeliwa na tembo, leo wanakuja kuniuliza Mheshimiwa Mbunge unatusaidiaje? Siyo mimi ni ninyi Serikali mnawasaidiaje wananchi wa Jimbo la Mchinga kutokana na chakula chao kuliwa? Naomba ifanyike tathmini haraka ili wananchi wa Jimbo la Mchinga walipwe fidia kutokana na mazao yaliyoliwa na tembo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Mnadhimu kwamba ilikuwa nichangie jioni, lakini nakushukuru hayo ndiyo maamuzi ya Kiti. Ahsante sana.