Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi jioni ya leo nami niweze kuchangia. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, ndiye anayeniwezesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina kila sababu ya kuwashukuru wananchi wa Kalambo, tulikubaliana kwamba nuru mpya ya Kalambo, kwa pamoja tunaweza; na hakika wamenirejesha kwa kishindo, nawaahidi sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango ulioletwa unaleta matumaini makubwa sana. Tanzania ya viwanda inawezekana. Viwanda vipi ambavyo tunaenda kuvijenga? Ni hakika Serikali lazima ijenge viwanda vya kimkakati lakini, ni wajibu wa sekta binafsi kushiriki katika viwanda vidogo vidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapotaka kujenga kiwanda maana yake ni lazima rasilimali fedha iwepo ya kutosha. Bila mtaji wa kutosha hakuna viwanda ambavyo tunaweza kujenga. Serikali ikijenga viwanda vya kimkakati, tukaiachia Sekta binafsi, wanaenda kutoa pesa wapi Hawawezi kwenda kukopa katika mabenki ya kibiashara, kwa sababu unapowekeza katika kiwanda hutarajii return ya haraka. Lazima ni mtaji mkubwa ambao return yake utaipata kidogo kidogo.?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali, haiwezekani tuka-plan kwenda kushindwa. Tunapokuwa na Benki ambayo hatujaipa mtaji, kwa maana ya TIB, hakika ni kwamba tume-plan kwenda kushindwa. Tusikubali kufanya kosa hili, tuhakikishe tunaiwezesha Benki yetu ya TIB ili itoe fursa kwa wananchi kwenda kukopa kwa riba ambayo ni rahisi kulipika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni mashuhuda kwamba asilimia 75 ya Watanzania ni wakulima na hasa ambao wako vijijini. Sitafarijika hata kidogo na wala sitaki kuamini kwamba Serikali imesahau mpango mzima wa SAGCOT. Tumesema lazima tuwekeze katika kilimo, ikaja mipango mizuri, naamini na hili litakuja; ni kwa sababu inawezekana bado wanakumbuka, ikija detail report itaainisha masuala yote ya kuhakikisha kwamba tunajitosheleza katika kilimo na tena kilimo cha kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali, kwa utaratibu wake na Mpango waliokuja nao wa kuhakikisha kwamba tunaenda kubana matumizi, kutumia pale tu ambapo itaongeza tija. Ni jambo jema. Serikali imeagiza kwamba kuanzia sasa pesa zake zote ambazo Taasisi zimekuwa zikiweka katika Benki za kibiashara, zipelekwe Benki Kuu maana zote ni mali ya Derikali. Sina ubishi! Ubishi wangu unakuja pale ambapo kama utaratibu tutakaoenda kuufanya utasababisha mashirika yetu ambayo yashaanza kufanya vizuri, tukaya-suffocate. Haitapendeza!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni suala la control, naomba niikumbushe Serikali irejee Sheria ya Bajeti Kifungu cha 17, inaeleza kabisa kazi ya Treasury Registrar kwamba mashirika yote ambayo yako chini ya TR watapeleka bajeti zao kule, ataidhinisha na hata kama kuna suala la kwenda kuwekeza, ni lazima wawe wamepata idhini kutoka kwake. Hiyo ni control ya kutosha kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile ambavyo wananchi na Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tunapata wasiwasi, ni kwamba utaratibu wa kuhamisha pesa zote kupeleka Benki Kuu, inaweza kuziua Halmashauri zetu. Hakika pia inaweza ikaua mashirika yetu. Sisi ni mashahidi kwamba mwaka 2015 tulivyokuja hapa tulisema kwamba ni vizuri Taasisi zetu zikawezeshwa ikiwa ni pamoja na TPDC ili iweze kushiriki katika uchumi wa gesi na mafuta. Sasa kama utaratibu itakuwa hatuwezeshi wakawa na fungu la kutosha, wakaweza kuwekeza, hakika ushiriki wa Watanzania kwa kupitia shirika letu hautaweza kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nyie ndugu zangu nyote ni mashahidi kwa jinsi ambavyo Shirika letu la Nyumba la Taifa lilivyokuwa na hali mbovu, leo hii limekuwa ni miongini mwa mashirika machache ambayo yanapigiwa mfano kwa namna ambavyo wanawekeza na naamini na Kalambo watakuja. Sasa zile taratibu kwa wale watu wanaofanya kazi vizuri tusianze kuwa-frustrate. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesoma katika Mpango kuna suala zima la kununua ndege. Ni jambo jema sana, lakini haitapendeza tunaposema tunataka kufufua Shirika letu la Ndege, zinanunuliwa ndege mbili, lakini kwa utaratibu ambao utakuwa umewekwa kwa makusudi, wakashindwa hata kununua mafuta kwa sababu OC haijawafikia. Itakuwa hatutendi haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala zima la Wakandarasi wa ndani. Wakandarasi wa ndani wamekuwa wakiidai Serikali kwa muda mrefu. Kutowalipa Wakandarasi tafsiri yake ni nini? Barabara zetu hazijengwi zikakamilika kwa kiwango kwa wakati unaotakiwa. Tafsiri yake ni kwamba, miradi mingi inajengwa kwa gharama kubwa, kwa sababu kwa kutowalipa, wanalazimika kuidai Serikali riba, lakini hali kadhalika wanashindwa kulipa kodi kwa sababu wao wanaidai Serikali na Serikali haijalipa. Nasi tunataka kuwe na mzunguko wa kutosha; walipwe na Serikali, walipe kodi, lakini pia waweze kutoa ajira kwa Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kipekee, Serikali ihakikishe kwamba miradi ile ya barabara ambayo imeshaanza, ikiwa ni pamoja na mradi wa barabara kutoka Sumbawanga kwenda Mpanda; Mradi wa barabara kutoka Sumbawanga kwenda Kalambo Port, unakamilika kwa wakati ili tuhakikishe kwamba kasi ya Tanzania ya kwenda kuwa nchi ya kipato cha uchumi wa kati, inawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Watanzania tukubaliane, kupanga ni kuchagua. Haiwezekani tukatekeleza yote, ndiyo maana tukubaliane kwamba bila kujenga reli kwa standard gauge, hakika uchumi ambao tunataka upae na kufika uchumi wa kipato cha kati hatutaweza. Niwasihi ndugu zangu wote bila kujali unatoka eneo gani la Tanzania, tukubaliane mkakati wa kuhakikisha kwamba reli inajengwa. Bahati nzuri nyie ni mashahidi, kuna fungu ambalo lilitengwa kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa reli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwekeza lazima utarajie kupata kule ulikowekeza. Tujiulize, kutokana na bomba la gesi, ni kiasi gani kinapatikana kama return kwa Serikali na hicho ambacho kinapatikana kipo kwenye mfuko upi? Kama siyo hapo tu, mkongo wa Taifa, pesa nyingi sana imewekwa, tunataka tujue, baada ya kuwekeza return yake iko wapi? Iko mfuko upi kwa manufa ya Watanzania? (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.