Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa jioni hii kuchangia. Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia kusimama ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nawashukuru Wapigakura wa Mkoa wa Pwani kwa kukiwezesha Chama chetu kushinda Majimbo yote ya Mkoa wa Pwani, iliyopelekea kutuingiza Wabunge wa Viti Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Awamu ya Tano pamoja na Baraza lake la Mawaziri. Naona ameanza kazi vizuri na anasema Serikali yake siyo Serikali iliyochoka; Serikali makini ambayo inakusanya trilioni 1.4; Serikali ambayo inatumbua majibu kadiri inavyoweza; Serikali ambayo imechaguliwa na watu takriban milioni nane; Serikali ambayo ndani ya Bunge hili ina 74% ya Wabunge.
Mhesimiwa Mwenyekiti, Serikali hiyo haijachoka na Chama hicho kinaaminiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najielekeza kwenye Mwelekeo wa Mpango 2016/2017. Wakati najielekeza, naomba ninukuu hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati akizindua Bunge hili, ukurasa wa 22 aliposema: “Tunataka tuwatue akina mama ndoo kichwani. Tunatambua umasikini hauwezi kuondoka nchini kama wananchi hawapati maji safi na salama.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Mwelekeo wa Mpango 2016/2017 kwa kuwa umejielekeza kwenye miradi ya maji; Mradi wa Maji wa Ruvu Juu, Mradi wa Maji wa Ruvu Chini, Mradi wa Maji wa Chalinze, Mradi wa Maji wa Visima Virefu vya Kimbiji na Mpera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono nikiwa na matumaini kwamba miradi hii itakapokamilika; Mradi wa Maji wa Ruvu Juu umekamilika kwa 97%, nina imani maeneo ya Bagamoyo, Kibaha, Mlandizi, Kisarawe na Mkuranga yanaenda kupatiwa maji kutokana na kukamilika kwa miradi hii ambayo nimeitaja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono mwelekeo wa Mpango huu wa 2016/2017 kwa sababu, suala la elimu; na naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Elimu Profesa Ndalichako kwa kuanza mpango wa utoaji wa elimu bure. Natambua wapo baadhi ya Wapigakura wangu wa Mkoa wa Pwani walikuwa wanashindwa kulipa ada ya mitihani ya Baraza la Mitihani; walikuwa wanashindwa kulipa ada ya Sh. 20,000/= mpaka Sh. 70,000/= kwa Shule za Sekondari; walikuwa wanashindwa kugharamia baadhi ya gharama ambazo Serikali imezibeba kupitia capitation. (Makofi)
Kwa hiyo, nasema mwanzo wa safari ni moja. Tumeanza vizuri. Naipongeza Serikali, lakini natambua Serikali ipo sasa, inaangalia changamoto zilizojitokeza baada ya kuanza awamu hii ya elimu bure. Naiomba Serikali iangalie sana kwenye baadhi ya maeneo, hasa suala zima la uandaaji wa mitihani, suala zima la gharama, umeme, mlinzi katika shule zetu; nina imani mambo yatakuwa mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, katika suala hili la elimu, natambua Serikali ya Awamu ya Nne kupitia Bunge hili, tulipitisha Sheria ya Kuanzisha Tume ya Walimu. Naiomba Serikali ya Awamu ya Tano iharakishe uandaaji wa Kanuni ili hii Tume iweze kuwatendea haki Walimu, mishahara yao, kupanda kwa madaraja, lakini pia Serikali iendelee na mpango wa kuzipa Halmashauri zetu kila mwaka milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Walimu na ujenzi wa miundombinu mbalimbali.
Vile vile Serikali ikiangalie sana Kitengo cha Ukaguzi wa Elimu. Kitengo hiki mara nyingi hakitengewi fedha na tunakitegemea sana katika kukagua ubora wa elimu. Kwa hiyo, hayo yakifanyika, ninaamini utoaji wa elimu bure utaenda sambamba na elimu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu pia umejielekeza kwenye afya vijijini. Kama ambavyo Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ilivyoahidi, kila Mkoa kuwa na Hospitali ya Rufaa, Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati, naomba Serikali itakapokuja na Mpango ujieleze kinagaubaga, awamu hii itaongeza zahanati ngapi katika vijiji vyetu? Itaongeza Vituo vya Afya vingapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Serikali hii ijielekeze zaidi kwa watoa huduma kwenye Zahanati hizo na Vituo vya Afya. Yapo maeneo katika Mkoa wetu wa Pwani, hasa maeneo kwenye Jimbo la Kibiti, Kiongoroni, Kiechuu, Maparoni; maeneo haya ni maeneo pekee ambayo yanahitaji uangalizi maalum, kwani zipo Zahanati mpaka sasa hazina watoa huduma, hazina Madaktari wala nyumba. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iangalie maeneo yale maalum hasa yale yanayozungukwa na maji, ikiwemo Wilaya ya Rufiji, hususan Jimbo la Kibiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Sera za Serikali za kubana matumizi na katika Sera za Mapato. Hapa najielekeza kwenye utaratibu wa retention. Naipongeza Serikali kwa kuamua ku-retain fedha zake na Sheria ya Fedha (Public Finance Act) ya mwaka 2001, ilisema kinagaubaga, fedha zote zitaingia kwenye Mfuko Mkuu (Consolidated Fund).
Kwa hiyo, hapa nampongeza Dkt. Mpango kwa kuja na hili suala kwamba yapo mashirika ya EWURA, TICRA, walikuwa na pesa nyingi zaidi. Yapo mashirika, hata hizi tunazosema zinasimamia mbuga zetu, lakini tulijionea Taasisi ya Ngorongoro, TANAPA; kuna wakati fedha zilitumika kwa kulingana, siyo na bajeti, lakini matakwa ya viongozi wa wakati huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini fedha hizi zikikusanywa kwenye Mfuko Mkuu, lakini naiomba Serikali ijielekeze kuuondoa urasimu. Hazina mjipange kupunguza urasimu na kuzileta pesa hizi kwa mashirika haya kwa wakati uliokusudiwa. Ila ombi langu, Halmashauri zetu tuendelee kukusanya kwa sababu tunayo Mabaraza ya Madiwani yatasimamia, tutafuata Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Halmashauri, tukusanye na tuweze kufanya maendeleo ambayo yanakusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, najielekeza kwenye suala la kilimo. Tulikuwa na utaratibu wa Kilimo Kwanza, lakini pia tulikuwa na utaratibu wa SAGCOT; vile vile kipindi cha BRN kuna baadhi ya maeneo yalichaguliwa kuongeza uzalishaji wa sukari, mpunga na mahindi. Nina imani kabisa, kupitia Mpango huu, naomba kipaumbele pia kiwekwe kwenye kilimo na mipango iliyowekwa hii, BRN, bado ina nafasi ya kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna maeneo ambayo yalitengwa, kwa mfano Wilaya ya Bagamoyo lilitengwa eneo, watu wapo ECHO Energy, wanataka kufanya kazi kwa haraka, tuzalishe sukari nyingi tupunguze pesa tunazozitumia kwa ajili ya uagizaji wa sukari zifanye shughuli ambazo ni za kutoa huduma ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika ujenzi wa viwanda; Wilaya ya Kisarawe tumetenga eneo la viwanda. Tunalo, tunategemea miundombinu ya maji na miundombinu ya umeme ili eneo lile wadau mbalimbali wanaojitokeza waweze kununua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nina imani sana na Serikali. Serikali inaweza! Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi ina uthubutu. Serikali hii, amani ipo. Waliokuwa na nia ya kuvuruga amani ni waliokwenda kwenye Vituo vya Television na kujitangazia ushindi wamepata kura milioni kumi; hawana fomu za matokeo na walikuwa na Mawakala nchi nzima, wanajitangazia kura wakiwa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuliokuwa site, tuna uhakika, kura tulizihesabu vituoni, tunajua Wagombea Urais walipata kura ngapi, hakukuwa na utata. Matokeo yaliyotangazwa, Rais Dkt. John Pombe Magufuli alishinda, hatukuwaona mlete ushahidi wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna imani Serikali haijachoka, itafanya kazi. Hata hivi karibuni Serikali kupitia utaratibu wa utumbuaji wa majibu, napongeza ilivyotumbua jipu la Hati Fungani. Vipo Vyama vinajidai vinapinga ufisadi, lakini hatukuwaona kwenye majukwaa wakisema kupinga ufisadi. Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alijipambanua, alitoa ahadi kwamba yeye atapambana na ufisadi. Wengine hatukuwasikieni! Mlisemea wapi? Leo mkija ndani ya Bunge, mnasema ninyi ndiyo mnapambana na ufisadi, lakini naomba mtoe boriti zilizopo kwenye macho yenu kisha mtazame Vyama vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, napongeza na Bunge hili, wananchi wa Tanzania msibabaishwe na miongozo na kanuni, zimejaa Kanuni nyingi; lakini ukiangalia hata Taarifa yao hiyo waliyoandaa, Mpango huu umeandaliwa kwenye karatasi mbili tu. Zote hizi wameandaa maoni ya Mpango wa Miaka Mitano ambao haujadiliwi sasa! Maoni ya Mpango huu ni kurasa mbili tu. Kuonekana, mmesituka! Hongereni Watanzania. Ahsanteni sana. (Kicheko/Makofi)