Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon Munira Mustafa Khatib

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia bajeti hii. Naomba kwanza nimshukuru Waziri wa Fedha na timu yake yote kwa kutuletea bajeti ambayo inaweza kwenda kumkomboa maskini wa chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Serikali ina nia njema ya kumkomboa mwanamke mwenye kipato cha chini. Hata hivyo, cha kusikitisha vijana ambao ni zaidi ya asilimia 60 wamepatiwa shilingi bilioni tano kwa ajili ya kuendeleza ujuzi. Hii fedha ni kidogo sana kwa sababu vijana wanao-graduate kila mwaka ni zaidi ya 8,000. Kwa hiyo, naiomba Serikali iongeze pesa hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli tunaka kwenda kwenye nchi ya uchumi wa viwanda basi naomba Serikali iwe tayari kwenda kwenye nchi ya viwanda. Kivipi iwe tayari kwenda kwenye nchi ya viwanda? Ni kwa kuvilinda viwanda vyetu vya ndani kwani bado viwanda vyetu vya ndani Serikali haiko tayari kuvilinda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Kiwanda hiki cha Urafiki ambacho Serikali inamiliki asilimia 49 lakini hawa wenzetu Wachina wana asilimia 50. Kiwanda hiki kinamilikiwa na Wachina si Serikali. Ukiangalia hapa kuna tofauti ya asilimia mbili tu ili Serikali kuweza kukimiliki lakini ndani ya bajeti hii ya 2016/2017 bado Serikali haijatenga fedha hii kwa ajili ya kukikwamua kiwanda hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Meneja ni kutoka China hajui vision wala mission ya Kiwanda hiki cha Urafiki. Hivi kweli tunatengenezaje ajira kupitia viwanda? Hivi ni vipi tunaweza kuwakomboa vijana wa Tanzania kwa kupata ajira? Kama hatuko tayari tungetafuta njia nyingine ya kusaidia vijana lakini si kwa njia hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna Kiwanda cha TANELEC ambacho kiko Jijini Arusha kinazalisha jenereta. Jambo la kusikitisha Serikali inaagiza transformer nje badala ya kununua kutoka kwenye kiwanda hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli tungekuwa tayari kununua transformer katika kiwanda hiki basi tungepata ajira nyingi kwa vijana na tungeweza kupata fedha kwa ajili ya Serikali yetu. Leo wanatoka watu nje ya nchi kuja kununua jenereta katika kiwanda hiki cha TANELEC lakini sisi Watanzania tunaagiza bidhaa kutoka nje ya nchi. Nina imani bado Serikali haijaamua kuinua uchumi wa viwanda Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la asilimia 5 ambazo kila Halmashauri inatakiwa itoe kwa ajili ya kusaidia wanawake na vijana. Kama kweli tuko tayari kumsaidia kijana, kama kweli tuko tayari kumsaidia mwanamke basi naiomba Serikali iweze kuleta fedha hizi kwa wakati. Naiomba Serikali iweze kusimamia fedha hizi kuona zinapatikana ndani ya halmashauri kwa sababu halmashauri nyingi fedha hii wanasema hizifiki na vijana wengi hawapati fedha hii. Je, kijana huyu unataka kumsaidia kwa njia gani wakati fedha hii haimfikii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuzungumzia suala la kiinua mgongo cha Wabunge. Wabunge wengi wameliongelea suala hili la kiinua mgongo cha Wabunge lakini niiombe Serikali yangu, naamini ni sikivu, Serikali ya CCM inavyoambiwa inasikia. Mbunge huyu katika jimbo lake anafanya harusi, maziko, matibabu na kila kitu. Leo hii unasema Mbunge huyu huyu katika kiinua mgongo chake cha mwisho ambacho anakwenda kujipanga kimaisha, umkate kodi, kweli Mbunge huyu unamtaka baadaye afanye kitu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali yangu kwa nia njema, naamini Serikali yangu ina nia njema, iweze kukaa na kulifikiria suala hili la kuwakata Wabunge kodi. Naamini Serikali yangu ni sikivu na suala hili Wabunge wengi wamelizungumza, watalifanyia kazi.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, naunga mkono hoja.