Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kushukuru kwa kupata nafasi hii ili niweze kuungana na wenzangu katika kuchangia bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango. Lakini kabla ya yote nikupongeze wewe kwa umahiri wako na msimamo, umeonesha umahiri wa hali ya juu na kiti kimeku-fit, hongera sana mama, hongera sana jembe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nichukue fursa hii kumpongeza Waziri wa Fedha, Naibu wake na watendaji wote walioko ndani ya ofisi yake, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu. Mheshimiwa Waziri tunamfahamu umahiri wake hata kabla hajaingia ndani ya Bunge, uwezo wake tunaujua, isipokuwa michango yetu ni ya kumsaidia tu ili aweze kufunga goli vizuri kama ataitumia vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuchangia nianze kwa kusema kwamba mapato yote, uchumi wote ili kuboresha uchumi, kuongeza mapato huwezi ukatenga vitu viifuatavyo katika kuviboresha, ikiwemo barabara, reli, umeme, maji, afya, elimu, kilimo, tena kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Mheshimiwa Waziri katika kitabu chake ameeleza mikakati ya ujenzi wa reli ya kati na mambo mengine, lakini katika hili nataka nitoe ushauri kwa upande wa barabara. Yapo maeneo katika nchi hii ambayo hayawezi kupitiwa na reli, ama kwa sababu ya jiografia au ukanda wenyewe kwa jinsi ulivyokaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni vyema kabisa maeneo haya na yenyewe yakatazamwa kwa upekee kwa maana ya kuwajengea barabara za lami. Kama unapitisha reli upande huu, upande huu hawana reli ni vizuri basi tukatenda haki na upande wa pili ukapeleka nguvu ya barabara za lami, kwa sababu reli haiwezi ikapita pande zote katika nchi hii. Kwa hiyo, mgawanyo mzuri ni kuweza na wenyewe kuwapelekea barabara ya lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapozungumzia suala hili nizungumzie upande wa jimbo langu, Ukanda wa Ziwa Rukwa kutoka Kibaoni, unakuja Kilyamatundu unakwenda Kamsamba hadi Mlowo, ukanda ule huwezi ukapitisha reli lakini ni ukanda mkubwa tena wa uchumi wa hali ya juu. Nasikitika sana Serikali haijaangalia ukanda ule, una uchumi mkubwa, barabara yake ni kilometa zaidi ya mia mbili na kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu Serikali imeazimia kujenga Daraja la Mto Mumba ambalo wameshatangaza tenda yake, ili kuimarisha barabara hii ni vyema wakajenga sasa lami ili iweze kutoka Kibaoni mpaka Kamsamba ikatokee Mlowo ili kuunganisha watu wa ukanda ule na mikoa mingine. Bila kufanya hivyo wale watu utakuwa umewaacha kisiwani, ile barabara ya lami unayoona Sumbawanga kwa wale watu haiwafai wala hawana matumizi nayo kabisa kwa sababu ni ukanda ambao umejitenga, kwa hiyo, nailitaka nisisitize hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la CAG, wenzangu wamelizungumza kwa utaalam mkubwa sana, na kwa utafiti wangu karibu asilimia 90 ya Waheshimiwa Wabunge wamegusa jambo hili. Nina imani amesikiliza na mimi nimeona nigusie kwa sababu CAG ndiyo jicho, ndiyo dira ambayo inatuonesha kitu gani kimefanyika. Unapomtenga mtu huyu ni kama unataka kuficha uovu wako na sipendi Serikali hii ambayo Rais wetu amedhamiria kuondoa mafisadi halafu na mtu ambaye anaweza akawa jicho lake akapata kifungu kidogo. Kwa hiyo, nashauri kama wenzangu walivyoshauri, ofisi hii iweze kuangaliwa kwa kipaumbele cha hali ya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la migogoro ya ardhi, Serikali imetenga bilioni tano kwa ajili ya fidia ya migogoro ya ardhi, lakini kiwango hiki ni kidogo sana, karibu nchi yote imetapakaa migogoro ya ardhi. Bilioni tano haitoshi kuweza kufidia maeneo mbalimbali katika nchi nzima ya Tanzania, ni kitu ambacho hakiwezekani. Kama tuna azma kabisa ya kuondokana na migogoro hii ningeomba Serikali iweze kuangalia ni namna gani inaweza kufanya katika suala zima la kuongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la mapato kutokana na wananchi kudai risiti wakishapata huduma na namshukuru Mheshimiwa Rais amepiga kauli mbiu sana kwenye TV tunamsikiliza. Sasa kauli mbiu hii ya Mheshimiwa Rais isiishie kwenye TV maana yake ni indicator kutuambia sisi viongozi wote, Waheshimiwa Wabunge, Wenyeviti na raia wote wenye nia njema, huko tunakofanya mikutano kipaumbele iwe ni kuwaelimisha wananchi wetu kudai risiti anapopata huduma na hasa huko vijijini. Tumuunge Mheshimiwa Rais, anazungumza kwenye TV, sisi twende nayo kwenye mikutano ya hadhara kutoa elimu kwa wananchi wetu ili waweze kudai risiti pindi wanapopata huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie mashine za kutoa risiti. Ili tuweze kuleta ufanisi vizuri ni vyema kabisa mashine hizi zikatolewa bure na si bure, kwa sababu mtu akitoa mashine atakapokuwa anazitumia ndiyo nia njema ya kuleta mapato kwenye Serikali. Kwa hiyo, nashauri, ni vyema kabisa mashine hizi zikatolewa bure. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo limezungumzwa na karibu Waheshimiwa Wabunge asilimia 90, ni kuondoa msamaha wa kiinua mgongo kwa Waheshimiwa Wabunge. Suala hili ukiliangalia, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ni kama limechomekwa, halijaja kwa muundo rasmi, limechomekwa. Sasa kama limechomekwa ni kazi rahisi, lichomoe tu, hakuna sababu ya kuhangaika nalo. Lichomoe, kwa sababu lingekuwa limekaa kwa mpangilio lingegusa viongozi wote wa kisheria ambao wanatakiwa kusamehewa na msamaha huo, lakini kwa sababu limepachikwa basi wewe usipate kazi ngumu, lichomoe, wala halina hata uzito wowote, lichomoe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, watu wengine wanaweza wakadhani sisi Waheshimiwa Wabunge tunajisemea, sisi siyo Wabunge wa maisha, tupo leo, kesho watakuja Wabunge wengine, kwa hiyo hatujizungumzii sisi, tunazungumzia hata watakaokuja. Maana mtu mwingine anaweza kusema hawa Waheshimiwa Wabunge wanajitetea, hapana, sisi siyo Wabunge wa milele, wangapi walikuwepo hapa hawapo, hata Mawaziri hawapo. Kwa hiyo, tunazungumza kwa niaba ya Watanzania na kwa nia njema. Kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri aweze kuliangalia jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani kwa haya machache yametosha. Naunga mkono hoja.