Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuunga mkono hoja ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuhusiana na Makadirio na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imejaaliwa kwa wingi wa vivutio vya utalii ulimwenguni, vivutio ambavyo kwa bahati mbaya hatujavitumia ipasavyo kutuwezesha kuwa na fursa kubwa ya kiushindani katika sekta ya utalii. Wakati ambapo taarifa mbalimbali zimekuwa zikiisifu Tanzania kwa uwepo wa vivutio hivi, ikizidiwa tu na nchi kama Brazil, kama Taifa tumekuwa na changamoto kubwa ya udhaifu katika mikakati yetu ya kuvitangaza vivutio tulivyonavyo. Ni ukweli uliowazi kuwa endapo vivutio hivi vingetangazwa na kutumika vizuri, mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa nchi yetu ungekuwa mkubwa zaidi kuliko ilivyo sasa. Ni lazima tuwe na mkakati mahsusi wa kutangaza vivutio tulivyonavyo na mkakati huo lazima utengewe fedha za kutosha zitakazowezesha kutumika kwa mashirika makubwa ya utangazaji duniani kutangaza vivutio tulivyonavyo na fursa za uwekezaji katika sekta hii zilizopo hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kusuasua kwa ukuaji wa Dodoma kunasemakana kwa kiasi fulani kunachangiwa na mji huu kukosa bahari na maziwa ambayo husababisha utalii. Kwa kiasi cha maji tunachoona kinapotea kwa wingi kila msimu wa mvua unapofika hapa Dodoma, nani anasema hatuwezi kuanzisha state of the art artificial lake kama walivyofanya Malaysia kwenye mji wao mpya? Nani anasema hatuwezi kuwa na zoo ya kisasa kwenye viunga vya Dodoma? Nani anasema hatuwezi kuanzisha utalii wa zao la zabibiu hasa ikizingatiwa kwama Dodoma inasifika kuwa sehemu pekee ulimwenguni ambapo uzalishaji wa zabibu unafanyika kwa misimu miwili katika mwaka? Au nani anasema hatuwezi kunufaika kwa kuanzisha utalii wa tamaduni za Wagogo na nyumba zao za tembe? Hii ni mifano michache tu ya fursa za uwekezaji na vyanzo vipya vya sekta yetu ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Waziri inaonesha kuwa idadi ya watalii waliotembelea nchini imeshuka kidogo ikilinganishwa na mwaka uliopita. Hali hii inashabihiana na taarifa zilizomo kwenye ripoti ya World Tourism Organisation inayoonesha kumekuwa na kushuka kwa idadi ya watalii waliotembelea Bara la Afrika wakati hali kwa Mabara mengine kama Amerika, Asia na Ulaya ni tofauti kwani Mabara hayo yameshuhudia ongezeko la idadi ya watalii katika maeneo yao. Funzo tunalopata hapa ni kuwa lazima tuwekeze katika ubora wa vivutio tulivyonavyo na huduma tunazotoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kama Taifa lazima tuhakikishe kiwango tulichofikia cha idadi ya watalii wanaotembelea nchi kinalindwa kisishuke na wakati huo huo kuja na mikakati mipya ya kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini. Ripoti ya World Tourism Oraganisation inaonyesha kuwa kwa mwaka 2015 safari za kiutalii zinazofanywa na Wachina zimeongezeka kufikia safari milioni 120, ukuaji ambao umeizidi Marekani na mataifa mengine ya Ulaya. Ukuaji huu wa safari za kiutalii zinazofanywa na Wachina unamaanisha kuwa kwa kila safari kumi za kiutalii zilizofanyika ulimwenguni, safari moja ilihusisha raia wa China. Ukuaji huu wa safari za kiutalii zinazofanywa na Wachina ni fursa muhimu sana kwetu katika kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania. Nashauri Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje kuchukua hatua za haraka kuweka mikakati ya pamoja itakayotuwezesha kulikamata soko hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu sasa wadau muhimu katika sekta ya utalii nchini wamelalamikia mfumo mbovu wa utoaji leseni kwa kampuni za wazawa na masharti magumu ya uanzishaji kampuni za kusafirisha watalii ikilinganishwa na zile za kigeni. Lazima tuondokane na urasimu usio wa lazima ili kuwezesha Watanzania wengi zaidi kuwekeza katika sekta ya utalii. Ieleweke kuwa urasimu katika utoaji wa leseni na masharti magumu kuhusiana na viwango vikubwa vya mitaji si tu unazuia uanzishwaji wa makampuni ya utalii bali pia unadumaza ukuaji wa huduma zinazotolewa na sekta nyingine za uchumi kama uzalishaji wa chakula, usafiri, hoteli, wapagazi na watu wengine wanaotegemewa kutoa huduma kwa watalii wawe wa ndani au nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa mbalimbali zinaifananisha Tanzania na nchi kama Australia kwa kuwa na mfumo mbovu wa utoaji leseni, mfumo ambao hautoi mwanya kwa ukuaji wa sekta ya utalii. Aidha, utafiti wa IFC unabainisha kuwepo kwa urasimu mkubwa katika udhibiti wa leseni za utalii na upatikanaji wa mtaji hali ambayo inasababisha ugumu kwa wanaotaka kuingia katika sekta ya utalii hususani wazawa. Kwa kuwa kama Taifa tunakubaliana kimsingi kuwa sekta binafsi ni injini ya kukuza uchumi wa nchi yetu, lazima tuhakikishe tunatoa fursa pana kwa wazawa hususan wale wenye mitaji midogo ili nao waweze kushiriki katika kuwekeza. Lazima tuwaondolee vikwazo vinavyowanyima haki ya kujituma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya utalii ina nafasi kubwa ya kuendelea kuwa mhimili muhimu wa kukuza uchumi wa nchi yetu. Hata hivyo, kufanikiwa kwa hili kunategemea sana kufanyika mambo kadhaa muhimu kama vile kuongeza jitihada katika kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika kila kona ya nchi yetu, kuboresha miundombinu muhimu, kuboresha taaluma ya utalii ili kuwa na watu wenye elimu na taaluma stahiki na hali kadhalika kuondoa urasimu katika maeneo mbalimbali yahusuyo sekta ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na jitihada hizo ni muhimu vilevile kuelekeza nguvu zetu katika kukuza utalii wa ndani. Kuna umuhimu sasa wa kuja na mkakati mahsusi wa kukuza utalii wa ndani. Lazima mkakati huo uweke bayana jinsi ambavyo tutaweza kutumia makundi yenye ushawishi hapa nchini kama Wabunge, wasanii na hata timu zetu za mpira wa miguu kwenye ligi kuu kushiriki kwenye kuanzisha utamaduni wa utalii wa ndani hapa nchini. Jambo hili ni muhimu kutokana na ukweli kuwa utalii wa ndani ni uti wa mgongo katika ukuzaji wa sekta ya utalii katika nchi yoyote ile. Ni kutokana na ukweli huu hatuna budi kama Taifa kuelekeza nguvu zetu katika kujenga utamaduni wa wananchi kutembelea vivutio vilivyopo nchini na kuwa na mikakati ya kuhamasisha wanafunzi na vijana kwa ujumla kutembelea mbuga zetu na maeneo ya vivutio katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuwe na mkakati kabambe wa kuongeza jitihada zetu katika kutangaza vivutio tulivyonavyo ikibidi suala la utalii wa ndani liwe sehemu ya mitaala yetu ya kufundishia katika shule zetu, tufanye hivyo. Aidha, wakati umefika wa kuanzisha wiki maalum ya uzinduzi wa utalii wa ndani kila msimu wa utalii unapoanza nchini. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa jitihada zetu za kukuza na kutangaza utalii zinalenga makundi mbalimali ya watu nchini kwa kuzingatia umri, jinsia na uwezo wa kipato ili kumuwezesha kila Mtanzania kushiriki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ninalotaka kulizungumzia ni eneo la migogoro ya ardhi iliyopo katika Wilaya yangu ya Mkinga, migogoro ambayo kimsingi inaigusa Wizara hii. Migogoro hii imechukua muda mrefu kupatiwa ufumbuzi licha ya jitihada kubwa zilizofanyika kuishauri Serikali kuipatia ufumbuzi. Jambo hili limekuwa chanzo cha manung‟uniko makubwa na wananchi kupoteza imani kwa Serikali yao. Migogoro hii ni kama ifuatavyo hapa chini:-
(i) Mgogoro wa wananchi wa Segoma na TFS. Msitu wa Segoma wenye ekari 2,311 upo ndani ya shamba la Sigi Segoma lenye ukubwa wa ekari 2,829. Shamba hili lilimilikishwa kwa Shirika la Uchumi la Wilaya ya Muheza (SHUWIMU) kwa hati Na. 7675 ya tarehe 01 Aprili, 1990 ya miaka 33. Kutokana na kukosa mtaji na kuzorota kwa SHUWIMU, hati hii ilibadilishwa umiliki kuwa Muheza District Council kuanzia tarehe 16 Februari, 2007.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1992 SHUWIMU kwa kukosa mtaji na utaalam iliingia ubia na M/S Sigi Agricultural Co. Ltd. na SHUWIMU ilipovunjwa shamba lilimilikiwa na Muheza District Council ambayo ilifuta ubia uliokuwepo na kuingia ubia na SWIFTCOM ya Tanga. Hii ilisababisha M/S Sigi Agricultural Co. Ltd. kufungua kesi Na. 18 ya 1996 kupinga kufutwa kwa ubia wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 hukumu ya kesi hii ilitolewa na Halmashauri ya Muheza kupewa ushindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2007 Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga ilianzishwa kwa kumegwa toka Muheza. Katika zoezi la kugawana mali, shamba hili lilikuwa sehemu ya mali zilizogawiwa kwa Halmashauri ya Mkinga. Hivyo basi, kufuatia kutolewa kwa hukumu iliyohusisha shamba hili, Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga kwa ufadhili wa Tanzania Forest Conservation Group (TFCG) ilifanya ukaguzi wa uhalisia wa shamba kwa wakati huo na kutoa taarifa katika kikao kilichofanyika tarehe 08 Oktoba, 2012 kikihusisha viongozi wa kijiji cha Segoma, Kata, wataalam wa Halmashauri, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – Kanda ya Kaskazini na wataalam wa Mkoa. Kikao kilitoka na mapendekezo kuwa kwa kuwa kijiji cha Segoma kina tatizo kubwa la uhaba wa ardhi, ekari 518 za shamba zigawanywe kwa wananchi kwa shughuli za kilimo na makazi na ekari 2,311 zitengwe kuwa eneo la hifadhi ya msitu. Mnamo tarehe 05 Disemba, 2012 kikao cha Baraza la Madiwani kama wamiliki halali wa rasilimali hii kiliridhia mapendekezo haya na kuagiza ekari 518 zigawiwe kwa wananchi wa kijiji cha Segoma kwa shughuli za makazi na kilimo na ekari 2,311 zimilikishwe kwa kijiji cha Segoma kuwa msitu wa kijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Meneja wa Kanda wa Wakala wa Huduma za Misitu aliomba kuonana na uongozi wa Halmashauri kwa majadiliano juu ya kijiji kumilikishwa msitu. Taarifa ya ombi hilo ilipofikishwa kwenye kikao cha Baraza cha tarehe 16 – 17 Julai, 2014, Baraza liliagiza kuwa wataalam wa ardhi na misitu wa Wilaya watekeleze Azimio la Baraza la tarehe 05 Disemba, 2012 bila mabadiliko yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Menejimenti kutekeleza agizo hilo, tarehe 28 Novemba, 2014 kwa mshangao mkubwa Halmashauri ilipokea barua kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ikiamuru kusitishwa kugawa ardhi kwa wananchi kwa ajili ya kilimo na makazi na halikadhalika kukabidhi msitu kuwa wa kijiji cha Segoma. Jambo hili limeleta taharuki kubwa kwa wananchi kiasi kwamba walikuja Dodoma wakati wa vikao vya bajeti kuwasilisha malalamiko yao. Aidha, wakati wa kuhitimisha mjadala wa bajeti nililazimika kuomba ufafanuzi kuhusiana na jambo hili na Naibu Waziri alikiri kuwa wananchi wa Segoma wanayo haki ya kupatiwa ardhi tajwa na kwamba atatembelea Mkinga ili kulipatia ufumbuzi jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tukiendelea kusubiri utekelezwaji wa ahadi ya Naibu Waziri kutembelea Mkinga kuja kuupatia ufumbuzi mgogoro huu, Halmashauri ilipokea barua toka kwa Katibu Tawala wa Mkoa yenye Kumb. Na. BF 174/314/02/35 ya tarehe 02 Disemba, 2015 ikiagiza eneo la ekari 518 likabidhiwe rasmi kwa kijiji na eneo la msitu lenye ukubwa wa ekari 2,311 kuwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Huduma za Misitu hadi hapo uamuzi mwingine utakapotolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi haya ya kuinyang‟anya Halmashauri ya Mkinga rasilimali yake siyo tu kuwa ni ya uonevu mkubwa bali pia yanakinzana na Sheria ya Misitu ya mwaka 2002 ambayo inabainisha wazi kuwa jamii inaweza kulinda, kuhifadhi, kusimamia na kutumia kiendelevu misitu katika ardhi ya kijiji ili kukidhi mahitaji yao ya kimaendeleo ya muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kuwa zaidi ya hekta milioni 21.7 sawa na asilimia 45.7 za misitu hapa nchini zinasimamiwa na Serikali za Vijiji zaidi ya 1,000. Aidha, hekta milioni 3.5 sawa na asilimia 7.3 za msitu nchini zinasimamiwa na watu binafsi au vikundi. Hivyo, Kijiji cha Segoma kukabidhiwa kusimamia msitu wao wa asili haitakuwa kioja wala mara ya kwanza kwa kijiji kumiliki msitu. Ni kwa msingi huu tungependa kuona busara iliyotumika kuruhusu vijiji zaidi ya 1,000 hapa nchini kusimamia misitu yao ikitumika hata kwa msitu wa Segoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kutokana na ukweli kuwa wananchi hawa ndiyo wameutunza msitu wa Segoma na kuwajibika kuhakikisha msitu unabaki salama pasipo kuombwa wala kukabidhiwa na Serikali. Inasikitisha kuona leo wananchi hawa wakiporwa rasilimali hii kwa mabavu, kejeli na udhalilishwaji kuwa wao ni wavamizi.
Halmashauri ya Mkinga na wanakijiji wa Segoma wanataka kunufaika na umiliki wa rasilimali yao kupitia mapato yatokanayo na mavuno ya msitu huu ili kuboresha huduma za kijamii na kuleta maendeleo ya kijiji.
(ii) Kwamtili Estate - shamba hili lina ukubwa wa hekta 1,150 na linamilikiwa na Kwamtili Estate Ltd.yenye Certificate of Incorporation Na. 2649 iliyosajiliwa tarehe 09 Januari, 1961 ikiwa na wanahisa wafuatao:
S/N JINA LA MWENYE HISA ANAPOISHI MAELEZO
1. Dennis Martin Fielder 4 Market Square Tenbury, Wells Worcestershire - UK Amerudi Uingereza
2. National Agriculture & Food Corporation (NAFCO) Box 903 DSM Shirika limefutwa
3. Handrik Tjails Scheen C1/30 Algamines Bank, Amsterdam, Netherland Amefariki
4. Louis Van Wagenburg Laycisan Ag Vaghel, Holland Amefariki
5. Schoonmarkers Bart Vanderburg De Congabsen, 163 Schlkher, Holland Amefariki
6. Tracey Elan Allison The Willos Terrigton, Herefordenshire, UK Amefariki
7. Juvent Magoggo 42 Block S. Mikanjuni Box 5855 Tanga Anaishi Tanga
8. W. J. Tame Ltd Box 118 Tanga Amefariki
9. Jacobus Cornelius Josephus Moris Logtanburg Vaghel, Holland Amefariki
Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba hili lililopo katika eneo la Kwamtili, Kata ya Bosha, Wilaya ya Mkinga lilitumika kwa kilimo cha kibiashara cha zao la kakau. Hata hivyo, kwa muda wa miaka takribani 26 sasa shughuli za kilimo cha zao la kakau zimesimama baada ya iliyokuwa Menejimenti ya Kampuni chini ya Ndugu Dennis Fielder kutelekeza shamba hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, baada ya shamba kutelekezwa, mmoja wa wanahisa Ndugu Juvent Magoggo amekuwa akifanya shughuli ndogo ndogo ikiwemo kuvuna miti ndani ya shamba hili kwa lengo la kupata fedha za kufanyia uzalishaji mdogo mdogo na hali kadhalika kuruhusu wananchi wanaozunguka shamba hilo kulima mazao ambayo si ya kudumu. Hata hivyo, kwa sasa Ndugu Magoggo ameshindwa kuendelea kufanya shughuli hizo baada ya kunyimwa vibali vya kuvuna miti na kusafirisha magogo.
Kutokana na kuwepo kwa ombi la umiliki wa shamba hili, yamezuka makundi ya watu yanayodai kuwa na haki ya kumiliki shamba hili na hivyo kuwakodisha wananchi wanaozunguka shamba hili maeneo ya kulima kwa kuwalipisha sehemu ya mavuno yatokanayo na matumizi ya ardhi hiyo. Aidha, kumekuwa na wimbi la kujitokeza raia wa kigeni kwa kutumia kivuli cha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shamba na kulitelekeza Ndugu Dennis Fielder kufanya uharibifu wa mali za kampuni, ikiwemo upasuaji wa mbao na kuanzisha michakato ya kujimilikisha ardhi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, wananchi wanainyooshea kidole Ofisi ya Wakala wa Hifadhi ya Misitu Wilaya ya Mkinga kutaka kujiingiza katika kufanya udalali wa ardhi hii. Wananchi bado wana kumbukumbu nzuri ya jinsi watumishi hawa wa TFS Wilayani Mkinga walivyotumika kuwezesha mwekezaji wa Kiitaliano aliyejaribu kupatiwa ardhi ya Mkinga takribani hekta 25,000 kinyume na taratibu ili kulima jatropher.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali haijaweza kulipatia ufumbuzi tatizo lingine ambalo kimsingi limeanzishwa na TFS kutaka kupora ardhi ya wananchi katika shamba la Segoma, TFS hiyo hiyo inataka kuzalisha mgogoro mwingine wa kupora ardhi nyingine katika Wilaya ya Mkinga. Hatupo tayari kuona hili likitokea hasa ikizingatiwa kuwa Kwamtili inakabiliwa na tatizo kubwa la ardhi. Tunaiomba Serikali kutumia busara kuacha jambo hili na kuirejesha ardhi hii kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kwamtili na Kata ya Bosha kwa ujumla wamebaki katika umaskini wa kutupwa baada ya shughuli za kilimo cha kakau katika shamba la Kwamtili ambacho ndicho kilitoa ajira kwao kusitishwa. Nusura pekee kwa wananchi hawa ni kupatiwa maeneo katika shamba hili ili kwa kutumia utaratibu wa wakulima wadogo waweze kufanya shughuli ya kilimo na hivyo kujikimu kimaisha. Naiomba Serikali ifanye uamuzi wa kufuta hati ya shamba la Kwamtili na kisha kuligawa kwa wananchi kwa ajili ya kilimo na sehemu nyingine kutengwa kuwa hifadhi ya msitu wa kijiji.
(iii) Mgogoro wa Kijiji cha Mkota na Hifadhi ya Taifa Mkomazi; wananchi wa Kitongoji cha Kimuuni katika Kijiji cha Mkota, Kata ya Mwakijembe wamekuwa wakiishi katika eneo hilo kabla ya uhuru. Kitongoji hiki kina takribani kaya 170 na wakazi wapato 530. Wananchi hawa kwa muda wote wamekuwa msaada mkubwa kwa ulinzi na rasilimali za nchi yetu hasa ikizingatiwa kuwa eneo hili linapakana na nchi jirani ya Kenya. Wananchi hawa wanalalamika kuwa eneo lao ambalo ni sehemu ya kijiji cha Mkota kwa mujibu wa ramani ya kijiji iliyosajiliwa, eneo lao limechukuliwa na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi na pori tengefu la Umba na kwamba sasa wanatakiwa kuondoka kwenye eneo hilo licha ya kufanya uwekezaji mkubwa kwa kutumia nguvu zao kuchimba mabwawa makubwa ya kunywesha mifugo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro huu nimeufikisha Serikalini na nimelizungumzia jambo hili mara nyingi sana katika Bunge la Kumi lakini hadi sasa halijapatiwa ufumbuzi. Mheshimiwa Profesa Anna Tibaijuka wakati akiwa Waziri wa Ardhi akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa alifanya ziara katika Wilaya ya Mkinga na kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji hiki. Katika mkutano ule, Mheshimiwa Waziri aliwaahidi wananchi kuushughulikia mgogoro huu. Aidha, aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utaliii Mheshimiwa Mahmoud Mgimwa akiandamana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa naye alifanya ziara katika eneo la mgogoro (Kimuuni) na kufanya mkutano wa hadhara ambapo alipokea ombi la wananchi kwa eneo hili kupewa hadhi ya kuwa Wildlife Management Area (WMA) na kuahidi Wizara kuanzisha mchakato wa kulitangaza eneo ili kuwa WMA. Tunaamini kuwa suluhisho la mgogoro huu ni Serikali kukamilisha mchakato huu ili wananchi waweze kuishi kwa amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kuwa sasa changamoto za muda mrefu za uwepo wa migogoro ya mipaka ya vijiji, umiliki wa ardhi na uwepo wa mashamba yaliyotelekezwa kwa muda mrefu katika Wilaya ya Mkinga yatapatiwa ufumbuzi. Namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha hoja ya bajeti hii atueleze nini kauli ya Serikali kuhusiana na changamoto hizi na tunamuomba atoe kipaumbele cha kuitembelea Mkinga ili kuja kutatua migogoro hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja nikiamini kuwa Wizara itachukua hatua stahiki katika kutatua changamoto nilizoelezea na kuzielekeza taasisi zilizo chini yake kuacha kuwa chanzo cha migogoro na kuwanyima haki wananchi wetu.