Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Suleiman Ahmed Saddiq

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Mvomero ni moja ya Wilaya ambazo zimekumbwa na tatizo kubwa sana la migogoro ya wakulima na wafugaji. Zipo juhudi mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ikiwemo Halmashauri ya Wilaya Mvomero, uongozi wa Mkoa na Serikali Kuu kupitia Wizara mbalimbali. Nia na madhumuni ni kuondoa au kupunguza migogoro hii, zipo changamoto nyingi sana tunazokabiliana nazo ikiwemo uhaba wa ardhi kwa wafugaji na kwa wakulima. Mbali na hilo, lipo tatizo la bajeti, fedha hazifiki kwa wakati katika mipango yetu kama Halmashauri ikiwemo kutenga maeneo ya malisho, majosho, kupima ardhi, barabara na maeneo ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lipo tatizo la watendaji wetu wa ngazi ya kijiji na kata, baadhi yao kupokea rushwa na kuongeza mgogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleze kuhusu hifadhi iliyopo Wilayani Mvomero ya Wami Mbiki. Hifadhi hii inaunganisha Wilaya za Morogoro Vijijini, Bagamoyo na Mvomero. Kwa upande wa Mvomero baadhi ya vijiji vimetoa ardhi yao kwa lengo la kuboresha hifadhi na pia kuongeza Pato la Taifa. Tatizo lililopo sasa ni uhaba wa ardhi kwa ajili ya ufugaji na kilimo. Ombi la wananchi, baadhi ya vijiji virudishwe kwa wananchi. Vijiji hivi vikirudi vitapunguza sana tatizo la migogoro hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa ndani ya hifadhi yapo makundi ya mifugo, wapo wakulima humo, yapo na makazi hewa. Tatizo kubwa ni kudorora kwa mipango ya uanzishaji wa hifadhi hii. Awali Serikali ilikuwa na nia ya dhati lakini hata wafadhili nao wamejitoa katika hifadhi na kukosa mwelekeo wa hifadhi hii. Ombi la wananchi ni kupewa maeneo yao ili wayaendeleze kwa kilimo na ufugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata makubaliano ya awali kati ya vijiji na hifadhi hayatekelezwi na hakuna faida inayoonekana. Watu wa maeneo ya hifadhi wanafaidika na makubaliano ya kuanzisha hifadhi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shamba la mitiki Mtibwa, lipo Wilaya ya Mvomero, Tarafa ya Turiani. Ni shamba ambalo Serikali inapata mapato mengi licha ya wananchi kuwa walinzi wa amani wa shamba hili. Vijiji vina miradi ya maendeleo ya elimu, afya, maji, barabara na kadhalika. Tatizo hakuna mrabaha wanaopata wanakijiji wa maeneo ya jirani. Tunaomba Wizara kupitia idara yake, sasa itenge fungu la ujirani mwema ili kusaidia huduma za kijamii; hili litaleta na kudumisha mahusiano mema na pia kuongeza tija ya shamba. Pia tuna hitaji kubwa la madawati, Wizara iangalie uwezekano wa kutumia mabaki ya miti hii ya Mtibwa Teak kusaidia mabaki vijiji hivi vinavyozunguka shamba ili tupunguze tatizo la madawati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikumi National Park, inapatikana na Wilaya ya Mvomero, Kata ya Doma na Msongozi. Lipo tatizo kubwa sana la wanyama hususan tembo kuingia katika makazi na mashamba ya wananchi na kuleta athari kubwa sana ya mali na maisha ya wananchi wa Doma na Msongozi. Changamoto ni kubwa sana katika eneo hili. Wapo wananchi waliopoteza maisha yao, hadi sasa hakuna fidia iliyotolewa na TANAPA. Yapo mashamba na mali zilizoharibiwa hadi leo, hakuna fidia iliyolipwa na wanyama hawa wanatoka karika maeneo ya wananchi. Naomba kujua hatma ya malipo ya fidia za waathirika hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wananchi wa Doma na Msongozi ambao wapo mpakani na mbuga hii ya Mikumi wanahitaji madawati na kusaidia miradi ya maendeleo. Naomba TANAPA iwatupie jicho wananchi hawa katika mipango yao ya ujirani mwema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, Bodi ya Utalii iundwe na ije Mvomero, tunazo fursa nyingi za utalii kama vile milima ya Mgeta, maporomoko ya maji Bunduki ili maeneo haya yaingizwe katika sekta hii na yaweze kuchangia Pato la Taifa.