Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia Wizara ya Maji, nimshukuru pia Mwenyezi Mungu kwa kuniweka hapa salama na kuweza kuchangia hotuba hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa hotuba yake nzuri iliyosheheni mambo mengi sana hasa kwenye Mkoa wangu wa Tabora, safari hii kwa kweli kama yatatimia yote haya watakuwa wametutendea haki sana. Wametutengea pesa za Halmashauri karibu shilingi bilioni tano na milioni mia nane za maji. Lakini pia kuna miradi tofauti ya skimu za umwagiliaji, hekta nyingi sana zimechukuliwa Nzega, Igunga na Urambo. Ukiangalia ukurasa 134, 65, 154, 166 na 167 nimesoma sana na nimeona kwamba kwa kweli Serikali imejitahidi sana, tunaomba tu kwa Mwenyezi Mungu mambo haya yote yatekelezwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mradi wa Ziwa Victoria. Naipongeze Serikali kwa kutupa mradi mkubwa wa Ziwa Victoria, mradi huu utaanzia Shinyanga - Nzega, Nzega - Tabora, Nzega – Igunga - Tabora kwa baadaye utaenda Sikonge lakini mradi huu utapita kwenye vijiji 100 ambavyo vitafaidika na maji ya Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu tuliahidiwa toka mwaka 2008 mpaka leo mradi huu haujatimia, tumekuwa tukiambiwa upembuzi yakinifu, upembuzi wa kina lakini mchakato wa kuwapata wakandarasi unaendelea. Tulikuja hapa Bungeni mwaka 2011 tukaiomba sana Serikali wakatuahidi mwaka 2013 watakuwa mradi huu umekamilika wa maji wa Ziwa Victoria. Mpaka sasa mradi huu haujakamilika baadaye tukaja kuambiwa utakamilika mwaka wa fedha 2014/2015 haujakamilika tukaambiwa mwaka 2015/2016 Juni mradi huu utakamilika lakini haujakamilika (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nachangia hotuba ya Waziri Mkuu niliongelea suala hili lakini Waziri hakupata nafasi ya kunijibu, nikakutana nae mwenyewe nikamuuliza akaniambia Munde mchakato wa kuwapata wakandarasi unaenda kumalizika na mradi huu utakuwepo.
Mheshimiwa Waziri nikuombe sana tumesubiri kwa muda mrefu kuhusu mradi wa Ziwa Victoria tunaiomba sasa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo tunaiamini sana ije na majibu. Mheshimiwa Waziri ukisimama hapa leo hii uje na majibu ya maji ya Ziwa Victoria nimeona kwenye bajeti yako umeweka, lakini naomba unipe action plan, uniambie huo mchakato wa Wakandarasi unaisha lini, Wakandarasi wanaingia lini site na kazi inaanza lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nahemewa sana kumwambia Waziri kwamba nitatoa shilingi, kwa sababu Serikalini hii ni mpya imeanza kazi ndiyo bajeti yao ya kwanza na wameanza kazi kwa ari mpya, wamefanya kazi kwa nguvu sana na kwa kasi kubwa na hii ndiyo bajeti yao ya kwanza, mimi nasema nawapa muda nikiamini ahadi atakayoitoa hapa Waziri na action plan atakayoitoa hapa Waziri itakuwa ni ya ukweli kwa asilimia mia moja. Tunaiamini sana Serikali ya Awamu ya Tano na tunaamini kwa sababu ni bajeti yao ya kwanza tuwape muda watuambie hizo ahadi zao na tunaamini watazitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee kuhusu bwawa la Igombe, pale Tabora Manispaa tuna Bwawa la Igombe tuna ipongeza sana Serikali, mwaka 2011 wakati nimeingia humu Bungeni tulikuwa tunapata maji lita milioni 15 na sisi tulikuwa tunahitaji maji lita milioni 25. Serikali ya Chama cha Mapinduzi imefanya kazi na sasa hivi tunapata maji lita milioni 30. Napata taabu sana mtu anaposema Serikali hii haifanyi kazi yoyote, sasa tunapata maji lita milioni 30 pale Tabora Manispaa, lakini changamoto tuliyonayo hatuna mtandao wa mabomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ni jambo la aibu ule ni Mkoa wa siku nyingi sana ni mji wa zamani toka tunapata uhuru kukosa mtandao wa mabomba pale katikati ya Mji Manispaa kwa kweli ni jambo ambalo linasikitisha. Niiombe Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi Mheshimiwa Waziri utupe sasa hivi pesa za mtandao wa mabomba, tuliomba mkatuahidi mwaka 2013 mtatupa pesa za mtandao wa mabomba tupate mabomba pale mjini. Pale mjini kuna kata hazina mabomba Kata ya Mtendeni, Kata ya Kibutu, Kata ya Simbachawene, Kata ya Uledi na Kata ya Mawiti. Kata hizi hazina mtandao wa mabomba, tunakuomba sana.
Mheshimiwa Waziri, mliwaahidi TUWASA mwaka 2013 mtawapa hizi pesa kwenye mradi wa pili wa WSDP mpaka sasa pesa hizo TUWASA hawajazipata. Ninaiomba Serikali ijue kwamba TUWASA inajitegemea, inalipa mishahara, inalipa posho lakini kubwa zaidi inanunua madawa kwa ajili ya kutibu maji wanayokunywa wananchi wa Mkoa wa Tabora. Serikali tunaidai pesa nyingi sana, niombe kupitia Bunge lako Tukufu tunadai shilingi bilioni 2.3 TUWASA ili kuhudumia maji ya wananchi wa Tabora hasa kuya-treat ili tuweze kunywa maji safi. Watu hawa wanapokopwa, hawapewi hizi pesa haya maji wataya-treat vipi? Ndiyo maana siku nyingine ukiamka asubuhi ukifungua maji kwenye bomba maji ni meusi hayakuwekwa dawa Serikali inadaiwa pesa nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalidai Jeshi la Wananchi shilingi bilioni 1.9, naomba Jeshi la Wananchi wahusika mpo humu Waziri Mkuu upo unasikia, watulipe kama kupitia Hazina kama ni kupitia kwao shilingi bilioni 1.9 ili TUWASA iweze kujiendesha yenyewe. Tusiwafanye hawa watu wakashindwa kujiendesha, watu watakufa, milipuko ya magonjwa inapotokea kipindupindu Serikali ina gharamia pesa nyingi sana. Sasa wapeni pesa zao ili waweze kufanya kazi, Polisi tuna wadai shilingi milioni 230 na Hospitali ya Mkoa shilingi milioni 136 na Magereza shilingi milioni 76. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu uongozi wa TUWASA ujaribu kuongea na wafanyakazi wake wa chini, wafanyakazi hawa wamekuwa wakibugudhi sana wapiga kura wetu wa Chama cha Mapinduzi. Wamekuwa wakienda kudai pesa kwa kutaka rushwa, wamekuwa wakidai pesa kwa manyanyaso makubwa, niombe sana baadhi ya wafanyakazi wachache wanaichafua TUWASA Tabora. Wanakwenda kumwambia mtu unadaiwa maji ya shilingi ngapi, shilingi 18,000 nakukatika unipe shilingi 10,000, sasa jamani hiyo shilingi 10,000 unayochukua ya huyo bibi kizee ambayo angeongeza 8,000 akalipa maji unataka rushwa wewe nikuombe sana Mkurugenzi wa TUWASA naamini umo humu ndani unanisikia, tunaomba sana ulifanyie kazi hili suala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi wa Inala, Inala tuna bwawa kubwa la shilingi bilioni 1.9 tumepata msada wa JICA lakini bwawa lile limepasuka mbele linamwaga maji, Serikali imetoa pesa nyingi sana zaidi ya shilingi bilioni (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mambo mengi ya kuongea lakini nitaandika mengine kwa maandishi, naomba nipate muda wa kumjibu Waziri Kivuli wa Upinzani, amesema Serikali ya Chama cha Mapinduzi itaingia kwenye kitabu cha maajabu na mimi nakubaliana na yeye tutaingia kwenye kitabu cha maajabu, tumepata Rais jembe anasifika dunia nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukifungua BBC utamsikia Magufuli tutaingia kwenye kitabu cha maajabu, lakini tukishaingia kwenye kitabu cha ajabu mwaka 2020 tutapofuta Upinzani wote, kwa sababu Serikali inafayakazi, Serikali imedhibiti rushwa, inasimamia wafanyakazi wake na miradi hii itaendelea kwa sababu imedhibiti wizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaingia kwenye kitabu cha maajabu CCM sasa hivi haina makapi ya kupeleka mgombea Urais, kwa hiyo, sasa hivi tumejipanga kwa hiyo tutaingia kwenye kitabu cha maajabu kwa sababu tunafanya kazi. Museveni ameomba kura Uganda kwa kutumia Jina la Magufuli anasema nipeni kura ili nifanye kazi kama Magufuli. Kwa hiyo, anavyosema Serikali hii itaingia kwenye kitabu cha maajabu mimi namuunga mkono tutaingia kwenye kitabu cha maajabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda wangu unaendelea naomba nichangie kuhusu bwawa la Manonga, Kule Manonga kuna bwawa kubwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekuja, tunaomba sana Serikali itupe pesa kwa ajili ya kujenga tuta, bwawa lile litatusaidia kilimo cha mboga mboga, lakini litasaidia wakulima wetu kutokuhama hama kwa ajili ya kunywesha mifugo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.