Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ili na mimi nitoe machache ya kwangu katika Wizara hii ya Maji, Wizara muhimu sana katika maisha yetu ya kibinadamu na ni Wizara ambayo kwa kweli ina mgusa kila mmoja. Jana na juzi tulizungumzia Wizara ya Elimu jinsi gani inagusa maisha ya kila mmoja lakini maji kwanza, usipokuwa na maji hauwezi ukaenda darasani wala hauwezi ukaenda kazini wala hauwezi ukafanya chochote. Kwa hiyo, nitoe mchango wangu katika Wizara hii muhimu sana ambayo inagusa maisha ya kila Mtanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee nisemee yale ambayo wananchi wa Jimbo la Babati Mjini wamenituma kuyasema. Hadi sasa hali ya maji katika nchi yetu siyo nzuri na Mheshimiwa Waziri unazungumza kuhusu kufikia asilimia 80 katika miaka hii mitano maji katika vijiji vyetu katika nchi nzima. Lakini Mheshimiwa Waziri kinachokukwamisha ni bajeti ya Serikali na mimi niombe tu Waheshimiwa Wabunge wenzangu hakuna sababu ya kukaa na kujadili bajeti ya Serikali wakati hazipelekwi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mtu anafanya vizuri ana nia njema lazima umpongeze. Mheshimiwa Waziri, tangu umeingia kwenye Wizara hii walau tumeanza kuona fedha zimeanza kufika katika maeneo yetu, bajeti iliyopitishwa ya Serikali ya mwaka huu inayotekelezwa kwenye shilingi bilioni 400 za maendeleo, zimeletwa tu bilioni 130 na kitu asilimia 28, hivi hata kama ungekuwa na nia njema ungefanyaje hiyo kazi? Ndiyo maana mchango wangu siku ya leo niwaombe Wabunge wote tujadili hii bajeti lakini tukijua adui mkubwa wa Wizara hii ni Wizara ya Fedha. Wizara ya Fedha hawapeleki pesa katika Wizara hii tunatenga bajeti pesa haziendi, na ndio maana miradi yetu haiendi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru pia katika vijiji vyangu vya Nakwa, Malangi, mliniletea pesa yale maji yameanza kutoka Mheshimiwa Waziri, lakini kama ungeletewa pesa zote shilingi bilioni 400 maana yake miradi ingekamilika yote. Kwa hiyo, niiombe Serikali tusiiachie Wizara ya Maji tukawanyima fedha tukajua watu wetu kule wako salama. Kama mpaka sasa nusu ya Watanzania vijijini hawana maji mnategemea tunasongaje mbele na Serikali ya CCM mkae chini mfikirie hili. Watanzania hawana maji, na mkimyima Waziri huyu, siyo kwamba mnaikomoa Wizara hiyo, mnatukomoa sisi na wananchi wetu huko chini, kwa hiyo niiombe Serikali Wizara ya Maji tuipe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie miradi viporo, tulikuwa na vijiji kumi kwa kila Halmashauri na Wilaya, kwenye Halmashauri yangu ya Mji wa Babati, zaidi ya vijiji vitatu sasa tumesubiri kwa muda mrefu sana. Mheshimiwa Waziri nimeona kwenye bajeti hii zaidi ya shilingi milioni 900 mnakwenda kunipatia kwenye kijiji cha Imbilili, kijiji cha Hala na Haraa. Ninaomba bajeti hii ya zaidi ya shilingi bilioni 900 unaoiomba kwenye Bunge hili, basi hivyo vijiji uvipatie kipaumbele kwa sababu tumekaa zaidi ya miaka minne watu hawana maji. Kata nzima kijiji kimoja tu sasa ndiyo naanza kuona kwamba kuna mwelekeo katika hizo shilingi milioni 900 lakini Kata nzima kina mama wanachota maji makorongoni, wanahangaika.(Makofi)
Mheshimiwa Waziri, shilingi bilioni 900 unaomba ni jambo jema, asilimia 75 ya fedha za ndani umetenga kwa mara ya kwanza kwa ajili ya miradi ya maendeleo, haijawahi kutokea, hizo asilimia 75 zikitoka za shilingi bilioni 900, shilingi bilioni 600 fedha za ndani basi zije moja kwa moja kwenye hivyo vijiji, haiwezekani miaka 55 wananchi wanachota maji kwenye makorongo. Kata nzima hawana maji, hawajui hata bomba la maji linafananaje, ndiyo sasa kijiji kimoja walau unaanza kuona mwanga kwa miaka 55 haiwezekani. (Makofi)
Kwa hiyo, ninaiomba Serikali kwa ujumla wake, angalieni suala la maji, suala la maji halisubiri, watu wanateseka. Walimu tuliokuwa tunawasemea juzi kwenye Kata hii Sigino anakuambia Mheshimiwa Mbunge ninakwendaje kufundisha wakati tu hata vyoo mlivyotujengea vya maji hakuna maji tunatoka na maji kwenye madumu. Naongea kwa masikitiko makubwa kwa sababu wananchi hawa wameteseka kwa muda mrefu, ninaomba Mheshimiwa Waziri hivi vijiji vyetu, ambavyo vimesubiri kwa muda mrefu uvipe vipaumbele hizo pesa zije mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la madeni ya taasisi. Wizara hii inadai zaidi ya shilingi bilioni 30 kwa taasisi mbalimbali za Serikali. Mfano, katika Jimbo langu la Babati Mjini, Magereza tu tunawadai shilingi milioni 100, Polisi tunawadai zaidi ya shilingi milioni 30, Halmashauri yangu inadaiwa zaidi ya shilingi milioni 12 katika hospitali, kwa nini taasisi hizi wanashindwa kulipa, sababu ni hizi zifuatazo:-
Kwanza Serikali hampeleki pesa za OC. Kwenye Magereza hampeleki, Polisi hampeleki, hospitali zetu tunaendesha kwa shida hata madaktari na manesi wanashindwa kulipwa, fedha za OC na on call allowances, watalipaje maji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu, naona leo dada yangu Susan Lyimo ndiyo amekaimishwa hongera dada, niombe Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu hebu taasisi na Wizara hizi waweze kulipa fedha hizi, mkiwapa Magereza na Polisi maana yake hizi shilingi bilioni 30 Mheshimiwa Waziri una uwezo kwamba hizi pesa sasa zinafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wezangu wa BAWASA Babati wameshindwa kufanya kazi kwa sababu wana nia njema, waliniambia Mheshimwa Mbunge tunapeleka Maji Gadueti, Managa, kila mahali kwenye vijiji vyako, lakini tunadai zaidi ya shilingi milioni 100 Magereza, Polisi tunawadai Halmashauri mmekata mpaka OC tunashindwa kuendesha, Serikali itupatie hizi pesa tukalipe.
Mheshimiwa Waziri, unasema solution ni prepaid meters, hivi unaweka prepaid meters hizi kwa pesa zipi yaani walipe kabla pesa ziko wapi OC haziko, hili ni la Serikali. Serikali tuleteeni pesa, lipeni hili deni la shilingi bilioni 30 ili tupate maji katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la madeni ya wakandarasi, Mheshimiwa Waziri katika shilingi bilioni 200, shilingi bilioni 100 umeshalipa, ninakuomba hizi shilingi bilioni 105 zilizobaki ulipe ili nikamilishe mradi wangu wa Nakwa, mradi wa Malangi, mradi wa Kiongozi wa maji, kwa sababu kwenye hizi shilingi bilioni 100 naamini pia Wakandarasi wangu ambao wanaendesha mradi wa Nakwa wanadai zaidi ya shilingi milioni 252. Kijiji cha Malangi zaidi ya milioni 280 hizi pesa zikija shilingi bilioni 100 ambazo Wakandarasi wanadai na Serikali mkapeleka Wizara ya Maji, maana yake wananchi hawa wanapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe Serikali bado, wala sina ugomvi na Waziri wa Maji, kwa sababu unagombanaje na mtu ambaye Serikali kwenye shilingi bilioni 400 inampelekea shilingi bilioni 100, nitakuwa mwenda wazumu! Mimi nahitaji Serikali pelekeni pesa Wizara ya Maji ili tuone kama Waziri anatosha au hatoshi. Lakini kwa kile alichokipata naamini kila mmoja hapa alikuwa anauliza walau kuna fedha zinafika kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe haya madeni Waziri wa Fedha naamini Mungu akitujalia tutachangia kwenye Wizara yako, kitu cha kwanza, tuone shilingi bilioni hizi 105 za maji za wakandarasi unalipa lini ili watu wetu waweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uvunaji wa maji, Mheshimiwa Waziri umesema taasisi za Serikali watengeneze matenki ya kuvuna maji. Hivi Halmashauri hazina pesa, OC haipelekwi unategemea hata kwenye fedha zile za miradi ya maendeleo watajenga matenki kwa fedha zipi? Serikali msirushe tu mpira Wizara ya Maji, hampeleki hata fedha za maendeleo, kama hampeleki mnategemea matenki hayo ya kuvuna maji kwenye maeneo ambayo visima haviwezi kujengwa, vinajengwa kwa namna gani? Kwenye package yenu hamuweki ujenzi wa hayo matenki ya kuvunia maji! Hili ni la Serikali, niishauri Serikali tatizo la maji ni kubwa sana, basi pelekeni fedha Wizara ya Maji ya matenki hayo maeneo ambako hakuna visima na maji ya mtiririko ili tuhakikishe kwamba maji hayo yanapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine muhimu sana ni suala la upangaji wa bei za maji. Mheshimiwa Waziri, utaratibu unajulikana kwamba wananchi wanahusishwa, lakini maji yamekuwa yakipanda katika taasisi za maji wananchi hawahusihwi, hata wakitoa maoni yao bado unit ya maji ni pesa nyingi sana. Hivi hawa Watanzania wanawezaje kulipa hizi bili?