Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia kwenye hoja iliyo mezani kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia nataka nitoe ushauri wa bure kwa Mheshimiwa Waziri. Pamoja na juhudi kubwa za kuweza kutatua maji katika jiji la Dar es Salaam kwa kuongeza uzalishaji kwenye Mto Ruvu na kuchimba Bwawa la Kidunda. Kimbiji ilikuwa ndiyo lango la Mto Rufiji kuingia baharini, pale Kimbiji chini kuna maji takribani cubic kilometre moja ambayo wakazi wa Dar es Salaam pamoja na kukua kwake wanaweza wakatumia kwa zaidi ya miaka 50. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri kwamba anapotafuta vyanzo vingine vya kupeleka maji Dar es Salaam na Kimbiji aifikirie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu alivyoibariki Mwenyezi Mungu pamoja na madini na kila kitu alichotupa ametupa vyanzo vingi vya maji, ukiacha bahari inayoanzia Tanga, Pemba, Zanzibar mpaka Mtwara; mito mingi, maziwa mengi. Lakini pamoja na mito yote tuliyonayo ukiangalia idadi ya watu waliokuwepo wakati wa uhuru na tuliopo sasa hivi tumeongezeka sana, wanyama wameongezeka sana, kilimo kimeongezeka sana, mito inapungua kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi. Ukiuangalia Mto Ruaha ulivyokuwa miaka ya 2006 - 2007 ukaungalia na leo inasikitisha, maji yanakauka ina maana mito yetu yote inakauka. Nashauri hizi Mamlaka za Mabonde ya Mito zote ambazo zimeunda naomba zipewe uwezo zaidi wa kusimamia vyanzo na kuboresha vyanzo vya mito hii vinginevyo vitakauka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa Mbunge miaka mingi sijawahi kuona mara moja ambapo mawazo ya Serikali, mawazo ya Kamati, mawazo ya Kambi ya Upinzani yanafanana, lakini safari hii naomba ninukuu kwa ruhusa yako. Mheshimiwa Waziri kwenye kitabu chake ukurasa wa 8 anasema kuhusu maji vijijini, Waziri anasema; “miradi ya maji vijijini inatekelezwa chini ya Programu Ndogo ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini kwa kuzingatia mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa (BRN), idadi ya watu wanaopata huduma ya maji vijijini imeongezeka kutoka milioni 15 sawa na asilimia 40 ya wananchi waishio vijijini mwezi Julai, 2013 hadi kufikia watu milioni 21.9 sawa na asilimia 72.” Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu anasema; “aidha, Mfuko wa Taifa wa Maji umeonyesha mafanikio makubwa katika kuwezesha upatikanaji wa fedha za kugharamia miradi ya maji vijijini, ambapo kiasi cha shilingi milioni 90 zilizotengwa zimeonyesha kutokidhi mahitaji ya miradi ya maji yaliyopo.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani anasema; “uanzishaji wa Wakala wa Maji Vijijini, katika Bunge la Kumi yalitolewa maoni kadhaa ndani ya Bunge lako Tukufu kuhusu uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini (Rural Water Agency) ikiwa ni lengo la kuongeza utoaji na usimamiaji wa huduma ya maji kwa wananchi katika maeneo ya vijijini.” Wote watatu wamekubaliana kwa hoja hii moja, ina maana Bunge lako lote linasimamia kwamba tuanzishe Wakala wa Maji Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona Wakala wa Barabara ilivyofanikiwa kutengeneza mtandao wa barabara nchini, tumeona mafanikio ya Wakala wa Umeme Vijijini sasa umefika wakati wa kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini. Kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye majumuisho aoneshe dhamira na nia yake kwamba katika Muswada wa Fedha wa Bajeti hii tunayoizungumzia apeleke mapendekezo ya kuanzishwa kwa Wakala wa Maji Vijijini ili vyanzo vya fedha vijulikane na viwekewe uzio ili Wizara ya Fedha isiweze kuvichezea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kwetu Chunya. Katika kitabu chako hiki Mheshimiwa Waziri kuhusu orodha ya Halmashauri zilizotengewa fedha za maendeleo kutekeleza maji vijijini kwa mwaka 2016/2017 sina matatizo, nimeiona Wilaya ya Chunya ipo kuhusu fedha zinazotoka nje kwa ajili ya maendeleo ya maji vijijini na mijini sina matatizo, tatizo langu ni mgawanyo wa fedha ukurasa wa 153 zilizotengwa kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji (Quick wins katika Miji Mikuu ya Wilaya na Miji Midogo kwa mwaka 2016/2017. Nikiangalia pale naona Mbeya kuna Kyela- Mbeya, Mbarali - Mbeya, Tukuyu - Mbeya, Kasumulu - Mbeya – Mbozi, sijaona Chunya, najua ni makosa ya uandishi, kwa hiyo nakuomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja kuleta majumuisho yako hapa na Wilaya ya Chunya uiweke kwenye hizo Quick wins.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mji wa Chunya ni katika miji mikongwe nchini au wilaya kongwe, nitaichukua Bagamoyo, Ujiji na Chunya. Visima vya maji ambavyo viko Chunya pale vilianzishwa mwaka 1938 wakati huo wananchi pale Chunya walikuwa 2000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi pale Chunya wananchi wanaelekea kuwa 20,000. Tunachimba kisima hiki, hakitoshi, tunachimba kisima kingine hakikidhi. Hata Mheshimiwa Rais alipokuja kuomba kura Chunya alikuta shida kubwa ya pale Mjini Chunya ni maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, fedha za quick wins zije ili tuweze kutatua matatizo ya maji Chunya Mjini na kwenye mji mdogo wa Makongorosi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niishukuru sana Serikali kwa kujenga bwawa la maji la Matwiga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.