Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Allan Joseph Kiula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia hotuba hii. Nashukuru sana kwa kunipa hizo dakika tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Waziri kwa Hotuba yenye data nyingi ambazo data hizo ukizipitia kila mtu anajua yuko katika nafasi ipi, lakini kwa ujumla napenda kusema kwamba, pesa za maji zinakuja nyingi, wafadhili wako wengi, lakini mgawanyo wake unaleta mashaka kwa sababu, nguvu kubwa inaelekezwa mijini. Ndiyo maana watu wanasema kuwe na Wakala wa Maji Vijijini. Vile vile asilimia za maji ambazo zinatolewa vijijini haziko sahihi! Niko tayari tufuatane na Waziri, tufanye kwenye Jimbo langu kama liwe Jimbo la Mfano, tuone asilimia ya wananchi wangapi wanapata maji, asilimia 72 haijafika hiyo na haitafikia kwa uharaka wa kiasi hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, suala la maji tuangalie vyanzo vya maji. Mkoa wa Singida ni mkoa kame, kama ni mkoa kame vyanzo vyake ni vya visima, hatuna mito, ingawaje lazima tufikirie mbali; wenzetu wanakunywa maji ya Mto Nile, bomba la mafuta linatoka Uganda mpaka linafika Tanga, gesi imesafirishwa kutoka Mtwara mpaka kwenda Dar-es-Salaam, equally maji ya Ziwa Viktoria yanaweza kusafirishwa yakafika Singida na yakafika Mkalama. Kwa hiyo, ni jambo ambalo linatakiwa tukae chini tuweze kulitafakari tuone tutafanya vipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 134 kuna pesa zimetengwa. Ukiangalia pesa za Mkoa wa Singida ni asilimia mbili nukta mbili katika bajeti yote; ukiangalia zile column unasikitika kuna bilioni tatu, bilioni nne, unakwenda wengine milioni 600, kigezo kipi kilitumika? Ukiangalia Mkalama milioni 600 watu 188,000, vijiji 80! Hayo maji yanatosha? Hayo maji hayawezi kutosha! Naamini kabisa, hakuna Mtaalam aliyefika kule! Katika hilo naondoka hapa nikiwa nimeshawishika hivyo!
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini iko miradi ya maji ambayo ilikuwa imeanza kutekelezwa, Iguguno, kuna wakazi 10,000! Mradi huo umeshindikana kukamilika! Mtamba, mradi huo umeshindwa kukamilika! Kidarafa umeshindikana! Kikonda umeshindikana! Watu wamechoka kusikia maneno, watu wanataka kunywa maji, hilo ndiyo jambo la muhimu! Wanaosimamia wanafanya kazi gani? Mheshimiwa Waziri naomba atakapojibu hapa, watu hao awafahamishe kwamba, hiyo miradi itakamilika lini? Tumezungumza huko kwenye ma-corridor nikamweleza, kuna mafundi wanazungukazunguka, lakini hakuna kinachoendelea!
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna maeneo kame kama vile Mpambala, Nyahaa, Endasaki, Mwangeza, Iguguno, tulitarajia kuwe na mabwawa. Hata kama bwawa moja kwa mwaka kwa miaka mitano tutapata mabwawa matano, lakini hatupo, tumeachwa watoto yatima. Jambo hilo liangaliwe na maeneo mengine kame ya Dodoma yaangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini scheme za umwagiliaji, imezungumzwa scheme ya msingi, huu ushirikishwaji mimi sielewi unaanzia wapi? Ziko scheme ambazo zimekuwa abandoned, kama Mwangeza iko scheme ya umwagiliaji na kulikuwa na miundombinu pale, lakini haijatokea humu! Kwa hiyo, inaonekana hawa Wataalam wanakwenda kwa maslahi yao binafsi.
Ndugu zangu ni vema tukawa tunafundishana humu ndani kwa ndani tuangalie mifano ya Wizara nyingine zinafanyaje? Ukichukua mwenzako amefanya nini inaweza ikaleta tija, tumeona Nishati mambo ya REA! Tumeona REA inasonga mbele! Kwa nini na sisi tusiwe na mfumo kama wa REA kuhusu maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweka hivyo na tukaweka muda kwamba, kwa miaka mitano au miaka 10, tutakuwa tumepiga hatua na jambo la maji litakuwa historia ikiwepo watu kupata maji salama. Hata hivyo, ukisoma ukurasa wa 109 kuna deni la shilingi bilioni 212; lazima tuone pesa zimetumika wapi? Ifanyike auditing, kama hiyo miradi inayozungumzwa ya Iguguno watu wanadai madeni na kwenye majimbo mengine ina maana hizi pesa hazikutumika! Hizi pesa tunashawishika kuwa watu wamegawana! Wametengeneza vitu ambavyo ni sub-standard miradi imeshindwa kukamilika, ifanyike auditing tuweze kujua kabla hamjalipa hizo pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nizungumzie maji mijini, pale Dar-es-Salaam; hawa DAWASCO wanafanya biashara wanawaonea wateja! Mimi kama Mbunge wamenikatia maji nyumbani kwangu wananiambia nilipe laki tisa, nalipa kwa sababu mimi Mbunge! Mtu wa kawaida atapata wapi laki tisa? Wanafunga maji watapata wapi? Pale DAWASCO Kimara yale ni majipu matupu yale! Sasa wananchi wa Dar-es-Salaam mlaji nae aweze kulindwa. Mheshimiwa Waziri naomba jambo hili alichukulie kwa umakini na kwenye mamlaka nyingine za maji ili watu waweze kupata maji kwa wanachotumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji ni suala la muhimu. Tunaomba sisi ambao hatuna mito inayotiririka kwa mwaka mzima, tupewe kipaumbele kwa maana hiyo, hata bajeti iweze kuongezeka. Unategemea viwanda vitajengwaje katika wilaya kama hizo ambako maji hayapo? Unategemea wananchi watarudi vipi vijijini kama hawapati huduma ya maji? Unajua watu mijini wanafuata umeme, wanafuata maji, wanafuata barabara na vitu vya namna hiyo! Kama tunataka wananchi wetu, miji yetu ipumue, watu warudi vijijini, lazima miundombinu na huduma hizo muhimu ziweze kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi hiyo. Nafikiri ujumbe wangu umefika vizuri kabisa kwa Waziri. Naunga mkono hoja.