Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Malinyi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu katika mada iliyopo mbele yetu. Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa uwezo wa afya leo kusimama hapa mbele na mimi nitoe mchango katika mada hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamekupongeza na mimi nitakuwa mchoyo wa fadhila. Pongezi hizo ni kweli unastahili, za haki na za dhati kabisa kwamba nafasi uliyokalia hapa unaiweza. Sisi tuko pamoja nawe, tunakuomba usiyumbe, endelea kurekebisha Bunge hili kama mhimili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu katika bajeti hii nitajikita zaidi kwa mambo yafuatayo na nitaanza na mambo ya mapato. Changamoto kubwa ni kwamba bajeti tunapitisha lakini inafika wakati tunashindwa kutekeleza bajeti hii kwa sababu ya mapato. Kamati ya Bajeti toka kipindi cha Mwenyekiti Chenge wametoa maelekezo, wametoa ushauri lakini Serikali ni muda sasa bado hawatilii maanani vyanzo vipya vya mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika Serikali yetu inaendelea na vile vyanzo vya kawaida na matokeo yake yanatupelekea tunapofika nusu ya mwaka wa kifedha tunarudi tena tunakaa chini tunaanza kupitisha bajeti na matokeo yake tunashindwa kutekeleza miradi mingi ambayo tumeiweka kwenye bajeti. Kwa kuwa kipindi hiki tunaweza tukajifunza, basi muanze kutekeleza angalau yale ambayo Kamati wamependekeza, ndani ya miezi sita pengine mnaweza mkaleta matokeo mapya zaidi mkayafanyia kazi katika bajeti ijayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kingine hapa nimekiona kidogo, natoa angalizo kwamba, wanataka waongeze wigo wa walipa kodi. Angalizo langu wigo huo wanapotaka kuupanua wasije wakagusa hawa wananchi wa kawaidam maana wanasema wanataka wachukue sekta zisizokuwa rasmi, kwa mfano wenye maduka madogo madogo ambao wengi wako vijijini, wenye miradi ya Sh. 70,000 mpaka Sh. 100,000 kama watawaingiza hawa kwamba ndiyo wanaongeza wigo wa walipa kodi, hili ni angalizo, Serikali watakuwa wanawaonea kwa kuwa hawa kwa lugha nyingine ni wajasiriamali ambao wanajitahidi na tunatakiwa Serikali tuwaunge mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii imeleta neema na imeleta matumaini katika kutatua kero za wananchi. Bunge hili toka tunaanza kikao hiki cha bajeti watu wanazungumzia kero mbalimbali kama migogoro ya ardhi, miundombinu, sekta ya afya na sekta ya maji. Nitatoa mfano katika Jimbo la Malinyi, tuna migogoro ya ardhi ambayo inatokana na matumizi ya ardhi ile kati ya watumiaji wake (wafugaji na wakulima).
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro mingine Serikali wenzetu ndiyo wameitengeneza. Kwa mfano, mgogoro ule wa Pori Tengefu la Bonde la Mto Kilombero. Ile hifadhi ya Pori Tengefu la Mto Kilombero ndiyo chanzo kimojawapo cha migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika maeneo ya Wilaya ya Ulanga na Wilaya ya Malinyi. Tumewaomba na wamekubali lakini ni muda mrefu sasa bado hawajaanza kutekeleza ombi letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ombi letu ni rahisi sana kwamba lile Pori Tengefu la Bonde la Kilombero kuna ile buffer zone, eneo lile lina range, linatoka kutoka kilomita moja mpaka 12, eneo lile ni pana sana. Matokeo yake wamekuja kuingiza mpaka vijiji 18 na vitongoji 22, wananchi wale wanaishi kihalali katika maeneo yale, wanashindwa kujiendeleza na matokeo yake kwa sababu ya uhaba wa ardhi tunaingia kwenye migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Kwa kuwa tayari wameshakubali, naomba basi katika bajeti hii na naiona kweli wametekeleza basi migogoro hii ifikie mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, mvua ya mwaka huu imekuwa nyingi na imeathiri sana miundombinu. Mojawapo ya miundombinu ni barabara zetu ambazo wananchi wengi wanazitumia. Nikitolea mfano ni barabara ya kuanzia Ifakara – Lupilo - Malinyi, Kilosa Mpepo - Namtumbo - Songea. Kwa kuwa barabara hii sehemu kubwa ni vumbi au barabara ya kawaida mvua zimeathiri sana. Naomba bajeti hii kama tutaipitisha, najua barabara sehemu nyingi zimeharibika lakini tunaomba kipaumbele kipelekwe kwenye barabara ambazo zimeathirika sana ikiwepo hiyo ambayo nimeitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, angalizo lingine naiomba Serikali kwamba, hii bajeti tunapoipitisha basi fedha hizi zipelekwe katika muda muafaka. Maana tumeshuhudia bajeti zilizopita kwamba tunapitisha bajeti lakini uwasilishwaji au upelekaji wa fedha umekuwa unasuasua. Kama tutapitisha halafu fedha haziendi kwenye bajeti impact yake itakuwa ni ndogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamegusia suala la bajeti finyu au fedha chache zilizotengwa kwa ajili ya Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali. Waheshimiwa Wabunge, sasa tuko kwenye mchakato wa kupitisha bajeti na kazi yetu nyingine inayofuata ni kuangalia ni namna gani fedha hizi za wananchi ambazo tumepitisha zinatumika na taasisi ambayo itatusaidia sana, jicho letu ni hili moja tu, ni jicho la CAG. Kwa bajeti ambayo wameitenga au fedha ambazo zimewekwa hapa ni kidogo sana. Naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati anaomba bajeti yake ya fedha, kitabu chake kile cha hotuba ukurasa wake ule wa 94, naomba ninukuu, alisema:-
“Wizara hii ya Fedha itaendelea kuimarisha uwezo wa kitaalam kwa wakaguzi wake, maana yake hawa CAG, na kuendelea na ujenzi wa majengo ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ili kuimarisha uhuru wa wakaguzi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na tija zaidi ili kukidhi matakwa ya viwango vya kimataifa vya taasisi za ukaguzi pamoja na maazimio ya kimataifa ya Lima na Mexico ambayo Tanzania imeridhia”.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wapi na wapi, walichotenga kinatofautiana na kile walichokisema, hakuna reflection na alichosema Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake. Nitoe mfano, bajeti ya mwaka huu ambayo wametengewa shilingi bilioni 32, ukiangalia mwaka wa fedha uliopita walitengewa shilingi bilioni 63, sasa wapi wanakoelekea wakati taasisi hii CAG wetu ana ithibati katika uwanja wa kimataifa. Kwa mgao huo maana yake tunamrudisha nyuma. Hiyo fedha niliyosema shilingi bilioni 32 ni matumizi ya kawaida lakini matumizi ya maendeleo ukijumlisha na matumizi ya kawaida yanafikia shilingi bilioni 44.7 ambapo mwaka jana wa kifedha CAG alipewa shilingi bilioni 74.2.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali wametoa maelezo hapa kwamba watakapofikia mwisho wa miezi sita (mid year review) mwaaangalia kama CAG fedha haitoshi wataweza kumwongezea. Mimi kwa uzoefu mdogo niliokuwa nao Serikali inaongea kwa maandishi. Tunaomba Serikali ili kweli tumpe nguvu CAG hapa watakapoishia watoe maandishi kama ni kweli wako committed, watakapofanya mid year review watajazia hii fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya CAG ili aweze kukamilisha majukumu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie, wenzangu wamechangia kuhusu kodi…
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.