Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Vyuo Vikuu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi katika Bunge lako hili Tukufu. Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama na kuongea, nilikuwa naendelea ku-observe majadiliano yanavyokwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu na kumpongeza sana Mheshimiwa wetu Rais kwa jinsi anavyopambana katika kuondoa umaskini, kupambana na rushwa, mafisadi na kadhalika ili kuona kwamba sasa nchi yetu itafikia mahali ambapo ile keki itagawanywa mpaka kule kwa wanyonge. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza mama yetu Mheshimiwa Samia kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kazi tunaiona, nawapongeza Mawaziri wote kazi zetu tunaziona na mnatosha lakini pia kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa kurudi mjengoni na wengine mara yetu ya kwanza kama hivi. Niwapongeze wapiga kura wangu wa Mkoa wa Morogoro pamoja na wanawake UWT Taifa kwa kuniamini kuweza kuwawakilisha bila kusahau support ninayoipata kutoka kwa familia yangu ikiongozwa na mume wangu mpendwa Profesa Tisekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, napenda sasa niweze kuchangia hii bajeti. Nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na timu yake yote akiwemo Mheshimiwa mdogo wangu Dkt. Ashatu Kijaji, nafahamu uwajibikaji wake na weledi wake, kwa hiyo nawapongeza sana. Bajeti hii inaleta matumaini hasa kwa kutenga asilimia 40 kupeleka kwenye masuala ya miradi ya maendeleo, hongereni sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na wajumbe wote ambao wamejadili suala hili hasa kwa kuwapongeza jinsi walivyopanga mikakati ya kuweza kukusanya kodi na kuongeza wigo wa kodi, nawapongeza sana. Pia nashauri sasa tuangalie zile kero ambazo zinaambatana na kodi na tozo za aina fulani ambazo wananchi bado wanazilalamikia kama Serikali muweze kuangalia kwa undani na kwa macho mawili ili kuondoa misuguano ambayo inaweza ikatokea kati ya Serikali na wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nichangie kwa kusema kwamba sasa hivi Watanzania sera yetu ya maendeleo tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda baadaye kufikia uchumi wa kati. Viwanda peke yake bila ya kuwa-empower wananchi wake hasa wananchi waishio vijijini haviwezi vikawa endelevu. Kwa nini nasema hivyo? Ni lazima tuweze ku-empower maendeleo vijijini na kwa wananchi wa vijijini kwa sababu asilimia 75 ya wananchi wako vijijini, rasilimali nyingi za Taifa zipo kijijini, nguvu kazi ipo vijijini lakini umaskini uliokithiri upo vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna sababu zote za msingi kuhakikisha miradi hii ya maendeleo ambayo imeelekezwa vijijini zile fedha ambazo zimepangwa basi fedha hizi zote zipelekwe ili kuendeleza vijiji vyetu. Tukifanya hivyo tunaweza sasa kuwa-empower hawa wananchi wetu na kuweza kuwa na purchasing power kwa sababu ukiwa na kiwanda parameter mojawapo lazima ku-create soko la ndani na la nje. Kama watu wako ni maskini ina maana hivi viwanda sustainability yake kidogo inaweza ikawa kwenye question mark. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuangalie suala la usawa wa kijinsia. Miradi ambayo imeelekezwa kule vijijini au mijini ile yote ambayo imelenga kupunguza matatizo ya wanawake (reproduction roles zao) mfano maji, afya, elimu na kadhalika ipewe fedha kama ilivyokuwa imepangwa. Kama tunavyoona 51% ya population ya Tanzania ni wanawake, ukiwaacha watumie saa tabi au sita kwenda kuchota maji, kuhangaika kwenda kwenye kituo cha afya hawataweza kushiriki katika uzalishaji. Kwa hiyo, huyu mwanamke ili aweze kuwa productive kwa sababu wako wengi na waweze kujikwamua kiuchumi tufikie ile fifty fifty mwaka 2030, lazima hawa wanawake wapunguziwe ile mizigo ya reproduction roles. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda nizungumzie suala la shilingi milioni 50. Hii shilingi milioni ya kila mtaa naona kwamba imeelekezwa sana kwa wajasiriamali na SACCOS. Mimi naona hii approach tunayoitumia siyo sahihi sana kwa sababu tunasahau hili kundi la maskini wa kipato cha chini watakuwa hawana msaada.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Sh. 5,000 inaweza ika-transform maisha ya huyu maskini ambaye hana kitu. Kwa sababu kule kijijini huyu mtu maskini wa kipato cha chini ambao wanaishi under poverty line kwa mfano anaweza akawa na nguvu, yupo physically fit, ana ardhi lakini hana jembe, hana mbegu. Kwa hiyo, huyu mtu ukamkopesha Sh. 5,000 akanunua mbegu, akanunua jembe that means next season tayari umeshamwezesha lakini sasa tukijikita kwenye wajasiriamali tukawasahau hawa, hatutafika mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine nasema sasa ili kupunguza milolongo ya kodi na tozo kwa wananchi wetu tutumie rasilimali zetu kwa mfano utalii, madini na kadhalika. Sisi kule Morogoro (Kisaki) tuna hot spring eneo kubwa, kilometers and kilometers lakini halitumiwi. Kwa mfano, ukienda Swaziland walikuwa na ka-spot kamoja ka hot spring wamejenga pale hoteli, swimming pool, hela zinatengenezwa. Sisi kwetu ukienda kwenye zile hot spring unakuta vibanda vya waganga wa kienyeji vimejazana pale. Kwa hiyo, tutumie rasilimali zetu ili tuweze kupunguza hizi tozo ambazo mara nyingi ni kero kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Kitengo cha Monitoring and Evaluation lazima kipewe kipaumbele kwa sababu on desk work mtu anakuja anatengeneza mikakati bila research, tathmini, hatutafika mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nizungumzie upande wa environment. Sikubaliani na kusema mifuko ya plastic sijui microns 50 sijui nini, nashauri ipigwe marufuku, inailetea hasara Taifa letu. Mafuriko haya mengi ukiangalia ni kwa sababu ya mifuko ya plastic. Huyu mzalishaji mwenye kiwanda anapata super profit lakini Serikali inapata super loss kwa sababu kila mwaka lazima itengeneze miundombinu ya barabara, umeme na kadhalika. Kwa hiyo, mimi naona hapana, ikatazwe kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho napenda nimalizie kwa kusema kwamba, mimi nashangaa sana, Waheshimiwa Wabunge, wachumi, wasomi na kadhalika kazi yao kusimama kwenye media na kubeza Serikali. Hii bajeti tunayoipitisha ni ya Serikali lakini kila Mtanzania lazima awe na bajeti yake ku-top up kwenye bajeti ya Serikali. Mimi nashangaa kwa mfano ukienda Bangladesh, Profesa Yunus alichukua dola zake 27 kwa kila mwanamke wale waliokuwa wanatengeneza furniture mpaka ikazaa Grameen Bank ambayo na yenyewe ikazaa na vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Profesa mzima aliyebobea anaenda eti kwenye media kuanza kulaumu Serikali, wewe Mbunge unasimama unalaumu Serikali eti mpaka nipewe nafasi ya kwenda Ikulu, wewe role yako ni nini kama Mbunge, kwa sababu wewe ni kiongozi! Wewe role yako ni nini kama Profesa kwa sababu wewe ni kiongozi, wewe role yako ni nini kama mwananchi wa kawaida kwa sababu sasa hivi mpaka Mheshimiwa Rais aende akawafanyie watu usafi kwenye kaya zao, inakuja hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nasema bajeti ya Serikali lazima iwe supported na sisi wananchi kwa umoja wetu. Watu hapa ni mabilionea badala ya kuweka hela benki chukueni hizo pesa wagawieni kama alivyofanya huyu Profesa Yunus wa Bangladesh kwa riba nafuu. Kwa sababu bajeti ya Serikali hata siku moja haiwezi kutosheleza kuleta maendeleo ya nchi yetu, ni sisi. Vita dhidi ya umaskini ni vita na kila mwananchi lazima awe askari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nasema, naomba bajeti hii fedha zipatikane ili kuweza kuleta maendeleo. Naunga mkono hoja, ahsante sana.