Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbagala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie bajeti hii ya Serikali. Mchango wangu ningeomba niondolewe mashaka na namtaka Mheshimiwa Waziri anijibu mashaka haya kwa sababu tuna-experience na jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la property tax Halmashari zote tatu za Jiji la Dar es Salaam tuliwahi kukusanya mapato kwa mfumo huu lakini TRA walichukua chanzo hiki cha mapato, kukawa na ugumu mkubwa sana wa Serikali kurejesha au TRA kurejesha zile pesa kwa Halmashauri. Kama wakituthibitishia kwamba sasa hivi wamejipanga na wanaweza kuzirejesha pesa hizi kadri wanavyokusanya sisi tutaunga mkono hoja, hatuna hoja na hilo. Suala la kuchukua chanzo hiki na kuanza kuomba misaada mtakuwa mnatuonea, yaani itakuwa kama tunaomba na hii ipo katika maeneo mengi siyo kwenye property tax tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nina mfano wa barua ambayo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke inaomba gawio la asilimia 30 kutoka Wizara ya Ardhi ya kodi ya ardhi karibu shilingi bilioni moja tangu mwaka jana mwezi wa nne mpaka leo, hata majibu ya kusema tumepokea barua wameshindwa kutoa. Siyo kwamba tunaomba msaada ni haki yetu, Halmshauri ina majukumu mengi inashindwa kutekeleza wajibu wake hatuna barabara, hatuna maji, hatuna hospitali lakini Wizara imekuwa si sikivu. Kwa hiyo, sisi tunachomba kama TRA wanapewa jukumu hili basi hizi pesa zirudi kwa wakati ili zilete maendeleo kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile kuna tatizo kubwa sana ambalo nimeliona la Serikali Kuu kutopeleka pesa za maendeleo kwenye Halmashauri zote nchini. Unakuta Accounting Officer pale, Mkurugenzi anasubiri disbursement kutoka Hazina miezi sita mpaka nane, matokeo yake inaiba vifungu vingine baadaye inaleta query kwa CAG. Kama Serikali imejipanga kutatua kero za wananchi basi pesa zipelekwe katika maeneo husika kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Mbagala ni jpya lakini kongwe kutoka Jimbo la Kigamboni. Jimbo letu tuna tatizo kubwa sana la barabara ambazo zimekuwa hazipitiki, maeneo mengine yamejifunga. Ukitoka pale Zakhem kwenga Kingugi lazima uzunguke, ni eneo la kwenda kama mita 500 unatumia kilometa tatu, barabara mbovu haipitiki na tumekuwa tukiomba lakini haijashughulikiwa. Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi imeizungumzia na Mheshimiwa Rais alivyokuja wakati wa kampeni pale Zakhem alituahidi, naomba Serikali itenge fedha kwa ajili ya kutimiza ahadi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile barabara ya kutoka Mtoni Kijichi kwenda Zakhem eneo la Mbagala Kuu imeharibika kabisa na hii ilikuwa ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwamba barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami. Cha kusikitisha ni barabara ya kilometa mbili tu lakini mwaka huu imetengewa robo kilometa itengenezwa na TANROADS, huu ni utani. Rais alishaahidi, Serikali ilishasema itatekeleza, naomba Waziri mhusika atilie mkazo mwaka huu barabara ile iweze kuisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni la Hospitali ya Zakhem. Hospitali hii ina mkusanyiko mkubwa wa wagonjwa na inahudumia watu wengi lakini Serikali ilisema italipa fidia ili iweze kuchukua lile eneo lakini mpaka leo imekuwa ni hadithi. Naomba Serikali ije na majibu ya jinsi gani ya kuweza kupanua hospitali ile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, lilitoka tangazo la Serikali kusema kwamba Wizara sasa imepandisha hadhi hospitali zile tatu za Mkoa wa Dar es Salaam za Amana, Temeke na Mwananyamala kuwa hospitali za Mkoa.
Huu mwaka wa saba sasa hivi Halmashauri bado zinazihudumia, Serikali imekwepa jukumu lake la kuchukua zile hospitali na kuzihudumia. Sasa tunaomba Serikali Kuu ichukue zile hospitali ili Halmashauri hizi ziweze kujipanga na kupeleka huduma mpaka chini. Wananchi wanapata taabu, tunazungumzia zahanati kila kijiji sisi hatuhitaji zahanati kila kijiji tunataka tuwe na hospitali inayohudumiwa na Halmashauri ipasavyo ili wananchi wetu waweze kupata huduma stahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, katika maboresho ya afya, eneo la Mbande hospitali ile sasa hivi imeelemewa. Tunaomba Serikali iongeze ruzuku kwenye hospitali ile ili ule upanuzi tulioahidiwa uweze kufanyika wananchi waweze kupata huduma za afya safi na za uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo ambalo ningependa sana kulizungumzia kwenye Jimbo langu la Mbagala nalo ni suala la ulinzi na usalama. Serikali ilianzisha Mkoa wa Kipolisi wa Temeke lakini huu sasa ni mwaka wa saba hakuna kituo cha polisi hata kimoja ambacho Serikali imesema sasa baada ya kuanzisha Mkoa wa Kipolisi Wilaya ya Mbagala ina kituo cha polisi, ina kituo cha OCD na huduma zingine zinazostahili. Vile vituo ambavyo wananchi walivijenga ndiyo vinaitwa police post lakini vinafungwa saa tisa, mwanzo wa uhalifu vituo vinafungwa na unakuta kuna askari mmoja. Mbagala kuna tatizo kubwa sana la uhalifu wote mnafahamu, naomba Serikali ilitazame kwa jicho la huruma eneo la Mbagala.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kuzungumzia maboresho ya Mahakama. Tunasema tutoe haki lakini leo Mbagala ina Mahakama ya Mwanzo moja inayohudumia wananchi karibu 800,000 haki inapatikana vipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile ili uweze kupata haki Mahakama ya Wilaya mpaka uende Temeke. Temeke yenyewe ina Jimbo la Temeke, Kigamboni inategemea Temeke, hatuna Mahakama. Leo tungekuwa na Mahakama Tuangoma, Mbande na maeneo mengine ingetusaidia kuharakisha kesi kumalizika kwa haraka. Kwa hiyo, naomba Serikali Kuu nayo ilitazame suala hili na kutusaidia kupata haki katika eneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende haraka haraka kwenye huduma za nishati ya umeme. Kuna mradi wa REA ambao ulikwenda katika maeneo ya Chamazi, Kwamzala, Mbande, Kwa Masista lakini wale wakandarasi wametupa nguzo wameondoka mpaka leo wameingia mitini. Sijui Waziri anatujibu nini kuhusiana na jambo hili kwani limekuwa kero kubwa maana Mbagala tupo Dar es Salaam lakini umeme hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna suala la low voltage. Jimboni kwangu ikifika saa 12 huwezi kuangalia televisheni, huwezi kuwasha friji kwa sababu umeme ni mdogo mno. Tunasema sasa tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda tunakwendaje nao ikiwa tuna low voltage Mbagala? Mbagala tuna eneo la viwanda lakini bila tatizo hili kushughulikiwa suala la viwanda litashindikana.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kuna kero kubwa ambayo wananchi wa Mbande wanailalamikia ni suala la Kilwa Energy. Huu sasa mwaka wa saba au wa nane hawajalipwa fidia na wameambiwa wasifanye shughuli zozote katika eneo unapopita ule mradi, hawa wananchi wanakwenda wapi na mbona hawalipwi?
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nimeongea na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati ananiambia wanategemea kupata pesa kutoka TIB. Kila siku wananchi wanaahidiwa kama hakuna pesa waambieni hakuna waendelee na shughuli zao za maendeleo. Kama pesa zipo walipeni waondoke pale kuliko kuendelea kuwanyanyasa na kuwasumbua pasipo na sababu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi kero zingine zinawezekana kumalizika. Maana ile Kilwa Energy inaanzia Somanga inakuja mpaka Mkuranga pale kwa Mheshimiwa Ulega, inakuja mpaka Mbagala, imekwenda mpaka Ilala ni tatizo. Mpaka watu washike mabango na waandamane ndiyo muelewe kama watu wanakerwa? Naomba Serikali kidogo ijirekebishe na iweze kutekeleza kwa wakati lile inaloahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la nishati kumekuwa na tatizo na Mheshimiwa Waziri katusomea bajeti yake kwamba gesi imepanda. Hata hivyo, gesi hii tunayoitegemea inatoka nje ile gesi ya Mtwara na maeneo mengine tunayoambiwa kila siku inakuja inakamilika lini ili Mtanzania wa kawaida aweze kutumia gesi maana maeneo yetu yale ukikamatwa na mkaa ni kesi. Sasa basi kama ni hivyo tupate nishati mbadala ya gesi, gesi yenyewe haipatikani na mnazidi kuipandisha bei. Naomba kama gesi ya Mtwara na Lindi bado haijapatikana, tupunguze tozo katika gesi wananchi waweze kupikia gesi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa vilevile kuzungumzia suala dogo tu maana najua kengele inaweza kugonga, kuna suala la mradi wa njia sita kutoka Bendera Tatu au pale BP mpaka Mbagala. Hii barabara ni muhimu sana kwa sababu wakazi wa Mbagala tunategemea na tunatarajia DART Phase II ije lakini ije kwa haraka na njia zile ziweze kupitika. Kumekuwa na msongamano na kumekuwa na matatizo makubwa, jioni kuna foleni, asubuhi kuna foleni. Kwa hiyo, kama mchakato huu upo uanze haraka ili wananchi na wao waweze kwenda na mwendo kasi kama ilivyo katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naona kuna tatizo kidogo la ufundi, katika mradi huu feasibility study ilifanyika miaka 10 iliyopita ndiyo maana ule mradi uliishia Kimara pale lakini mahitaji kwa Kimara pale siyo peke yake, Mbezi Kiluvya, Kibamba wote walikuwa wanahitaji. Kwa kule Mbagala mradi huu ulikuwa unaishia Rangitatu, DART wanataka kulipa fidia mpaka viwanda, kwa nini tuondoe viwanda ikiwa tuna uwezo wa kuusogeza mradi huu? Ileile fedha ya fidia ingetumika wangekwenda mpaka Kongowe eneo la Mwandege pale kwa Mheshimiwa Ulega, lile pori sisi kwetu ni kero, wahalifu wanajificha pale. Ondoeni lile pori wekeni kituo cha mabasi ya kisasa, wanaotoka mikoani wataishia pale, wanapanda mabasi ya mwendokasi wanakwenda katikakti ya mji na maeneo mengine. Ni suala la kukubaliana tu, si lazima kwamba feasibility study iliishia Rangitatu basi lazima tuishie Rangitatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile barabara ya kutoka Charambe kwenda Mbande iliwahi kuleta kashfa tangu Serikali ya Awamu ya Tatu na kuna baadhi ya Mawaziri walipelekwa Mahakamani. Barabara ile haina vituo, haina mifereji ya kuweza kuwafanya watu wakapita vizuri na haipitiki wakati wa masika…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.