Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Salum Khamis Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Meatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SALUM K. SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza na mimi nianze kwa kushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba hii iliyopo mbele yetu. Kwanza, nianze kwa kuunga mkono hoja iliyopo mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue fursa hii kukupongeza kwa kazi nzuri unayofanya na umahiri mkubwa unaouonesha katika kuongoza Bunge hili. Naomba nikuongezee nguvu kwa kukwambia Watanzania na watu wa Meatu wanakupongeza na wanakuita mwanamke hodari. Endelea kutuongoza hivyo hivyo kwa sababu Bunge hili miaka ya nyuma tulikuwa tukiitwa Bunge Tukufu sasa hivi katika kipindi cha miaka mitatu, minne iliyopita Bunge hili limekuwa Bunge la vurugu. Sababu yake ya msingi ni kwamba sheria ziliwekwa pembeni. Sheria za kuendesha Bunge na taratibu zake unazo mbele yako zishikilie na sisi tupo nyuma yako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nami nitoe shukrani zangu kwa watu wa Meatu na Jimbo la Meatu kwa kunipa imani yao ya kunipa nafasi ya uwakilishi ili nilete mawazo yangu hapa katika Bunge hili. Sisi wana Meatu tuna matatizo mengi na yanayohitaji fedha nyingi, kwa hiyo naunga mkono hoja hii nikiwa na maana ya kwamba Meatu tunahitaji barabara na maji ya Lake Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru kaka yangu Waziri wa Miundombinu kwa kuweka katika bajeti yake barabara za kutoka Shinyanga kuelekea Meatu kwenda Oliani. Hata hivyo, nilishamwambia lakini niseme kusudi wapiga kura wangu wasikie, hizi habari za kuambiwa kwamba fedha imetengwa na mkandarasi anatafutwa ziwe mwisho mwaka huu. Tunahitaji baada ya bajeti hii kuona wakandarasi wako site wakitengeneza barabara hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimshukuru kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mto Sibiti. Pia nimshukuru Waziri wa Maji kwa kutupa fedha na kutuwekea fedha za miradi yetu yote iliyokwama. Nimkumbushe bwawa la Mwanjoro linamhitaji aje Meatu kwa ajili ya kwenda kulikagua na kuona fedha za Serikali zilivyopotea. Pia nimshukuru Waziri wa Nishati na Madini katuahidi wana Meatu neema kubwa ya umeme, kila Kata itapata umeme, namshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maliasili, sisi kule Meatu tuna matatizo yetu ambapo nyie Wabunge wote mmeona mambo mbalimbali yakiandikwa kwenye magazeti lakini hiyo ndiyo sababu ya kuwasemea wapiga kura na athari zake ni za namna hiyo. Nawaomba ndugu zangu Wabunge wapuuzeni, hawana hoja hao watu wanaoleta maneno ya kizushi.
Suala letu tumemkabidhi Waziri Mkuu na Serikali ipo na wana Meatu tusubiri maamuzi ya Serikali. Sisi tupo tayari kuyapokea lakini hatutishwi wala hatutishiki kama walivyozoea. Kumchafua Mbunge wa Meatu hupati faida yoyote ile, unajiharibia mwenyewe tu kwa sababu mimi siyo Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kutoa mchango kidogo kuhusiana na sera yetu ya Rais wetu Magufuli ya viwanda. Kwanza naomba ku-declare interest kwamba mimi ni mjasiriamali wa hivyo viwanda. Tuna matatizo makubwa na nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, mipango yake iendane na fikra za Mheshimiwa Rais wetu Magufuli kwa kwenda kwenye nchi ya viwanda. Hatuwezi kufika kwenye fikra nzuri ya Rais bila kuwa na mipango mizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kutoa ushauri, tunatakiwa tubaini ni viwanda gani tunavyovizungumzia, tunataka kiwanda gani? Kwa sababu nchi yoyote duniani iliyofanikiwa kiviwanda iliweka programu ya viwanda, ni kiwanda gani kinachotakiwa kujengwa kwa wakati huo na ukikijenga utapata nini kama nchi, lakini kama wawekezaji wanatakiwa wafanye nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikiliza hotuba za Mawaziri na Wizara zote, kila Wizara inakinzana na Wizara nyingine kuhusu uwekezaji tena wa viwanda. Sasa niseme tu kwamba tunapitisha bajeti hii lakini nawaomba sasa wahusika bajeti ijayo mje na mpango ambao unawiana. Wizara hii na Wizara hii inasaidiana kwenda kwenye malengo ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii kuna viwanda haviwezekani. Mimi mwenyewe ninayezungumza hapa viwanda vyangu vyenyewe binafsi saba nimevifunga. Kwa maneno haya haya ya siasa tukajenga kiwanda cha nyuzi mnazungumzia Tabotext humu nawasikiliza, Tabotex ile haina mashine!
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina kiwanda cha nyuzi cha kisasa kutoka Ujerumani nimekifunga, thamani yake ni dola milioni 50. Kwa sababu siwezi ku-compete na nyuzi zingine kwa sababu umeme wa nchi yetu ni ghali, lakini siwezi ku-compete na watengenezaji wa nyuzi wengine kwa sababu pesa ninayochukua kwa ajili ya kununulia raw material ni asilimia 18. Hizi nyuzi zote mnakwenda kuuza kwenye soko moja, huyu mtu amepata umeme wa bei ya chini, huyu mtu amepata interest ya chini, labor ipo chini, ni lazima tubadilishe sera zetu kuhusu viwanda kama nchi hii inataka kwenda kwenye viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna usumbufu ambao hujawahi kuuona ukiwa mjasiriamali wa viwanda. Kuna kila aina ya kodi na kila mtu ana maamuzi yake. Wakati mwingine unashindwa kuelewa kama kweli tuna dhamira ya dhati. Kwa hiyo, niiombe Serikali ije na mpango mzuri, iwe na dira na iwe…
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja.