Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika bajeti hii. Kwanza kabisa napenda kukupongeza kwa jinsi unavyoliendesha Bunge hili kwa umahiri na kwa weledi.
Naomba muda wangu ulindwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakupongeza kwa jinsi unavyoendesha Bunge kwa umahiri mkubwa na kuonesha uwezo wako ni jinsi gani unavyojua kuzitumia kanuni. Wembamba wa reli lakini inabebe mizigo mizito ni sawa na wewe. Hongera sana na sisi tunakwambia kazi buti, wanawake tupo nyuma yako, umethibitisha ni jinsi gani unavyoweza, wanawake wa Bunge hili na wanawake wa Tanzania tunakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kaka yangu Philip Mpango, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa hotuba yao ambayo kwa kweli imesheheni mambo mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu sana nimekuwa nikisimama kuililia barabara ya Kigoma-Nyakanazi, huu mwaka wangu wa kumi na moja sasa, lakini siku hii ya leo nina furaha kubwa sana. Nafuraha kwa sababu nitakapoondoka ndani ya Bunge hili kuelekea Kigoma ninacho cha kuwaambia wananchi wa Kigoma maana najua kwa vyovyote wataniuliza ulizungumziaje barabara ya Kigoma-Nyakanazi, kwa hiyo nina majibu. Naomba sasa pesa zile zilizoelekezwa kwenda kujenga barabara ya Kigoma Nyakanazi zipelekwe ili barabara ile iweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kigoma ni kati ya mkoa ambao umeoneshwa kwamba ni mkoa maskini sana kati ya sababu zilizokuwa zinafanya tuwe maskini ni pamoja na miundombinu. Hata hivyo, kwa bajeti hii naomba niseme kwamba sasa umaskini tunauaga, kwa sababu wananchi watakuwa na miundombinu mizuri, watalima mazao yao, watasafirisha kwa kupitisha kwenye barabara nzuri, watasafirisha kupeleka mikoa mingine na kusafirisha ndani ya mkoa ule wa Kigoma; kwa hiyo naamini ule umaskini utaondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Kigoma sisi ni wakulima wazuri sana, kwa hiyo naamini miundombinu ya barabara na reli ikikamilika umaskini utapungua, wananchi wataweza kupata maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie jeshi la zimamoto. Kwa muda mrefu sana tumeshuhudia wananchi wakipata hasara sana, maduka yanaungua, vitu vyao vinaungua, mitaji yao inapotea kwa sababu wanakuwa wamepata hasara kutokana na moto ambao unakuwa umeteketeza mali zao. Ni kwa sababu jeshi la zima moto halina vitendea kazi, tumeshuhudia sekta ya ujenzi inakua kwa kasi sana, tunashuhudia ujenzi wa majengo mbali mbali yakiwemo maghorofa yenye ghorofa tisa, kumi, ishirini mpaka thelathini na mbili, lakini jeshi la zima moto halina vitenda kazi, halina vifaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo wawekezaji wanaweza kuogopa kuja kuwekeza mali zao huku kwa sababu zimamoto hawana vifaa vya kuweza kutumika pale linapotokea janga la moto. Kwa hiyo, naomba Serikali iweze kuliangalia hili. Katika bajeti hii inayotengwa sasa jeshi halijawezeshwa. Naomba hili nalo waliangalie jeshi la zimamoto litengewe fedha kwa kipindi kingine kama wakati huu haitawezekana kusudi wajiandae kukabiliana na majanga ya moto.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi tu Nzega maduka yameteketea ni kwa sababu hakuna vifaa vya zima moto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka kuzungumzia kuhusu lishe. Serikali ilitoa agizo kwa Halmashauri zote kutenga bajeti shilingi tano tu kwa kila mtoto. Agizo hili lilitolewa ili kila mtoto atengewe Shilingi tano tu kwenye kila Halmashauri. Lakini mpaka sasa Halmashauri imepuuza maagizo hayo na sisi wote tunashuhudia watoto wetu wakati mwingine wakienda shule wanashindwa kufanya vizuri kwa sababu wanapokuwa shuleni wakati mwingine wanakuwa na njaa. Kwa hiyo, naomba Halmashauri zitekeleze agizo lililotolewa na Serikali la kutenga ile Shilingi tano kwa kila mtoto ili watoto wetu waweze kufanya vizuri. Maana nikiuliza ni Halmashauri ngapi ambazo zimetekeleza agizo hilo, jibu ni hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu bado ina tatizo kubwa la utapiamlo, Serikali imefanya jitihada kubwa sana kuweza kuweka virutubisho kwenye vyakula vinavyozalishwa viwandani, lakini wanaonufaika ni wenye viwanda, wazalishaji wale wakubwa wakubwa. Naomba sasa Serikali iwawezesha wajasiriamali wadogo wadogo ili na wao waweze kupata hivyo virutubisho waweze kuweka kwenye biashara zao zile ndogo ndogo ili na wao waweze kupata soko wasihangaike kwa kusumbuliwa kwamba vyakula vyao havina virutubisho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maji. Mkoa wa Kigoma nimeona tumetengewa pesa kwa ajili ya maji, naomba pesa hizo zipelekwe, lakini nashauri; Mkoa wa Mwanza kwa kupitia Ziwa Victoria waliweza kufikisha maji Shinyanga, Geita, wakafikisha maji Igunga na Tabora; naomba sasa na sisi Kigoma tuweze kutumia maji ya Ziwa Tanganyika. Uangaliwe utaratibu wa kuweza kufanya mipango ya kuweza kuyatumia maji ya Ziwa Tanganyika. Hii ni kwa sababu mito tuliyonayo sasa hivi inakauka, maji baadaye yatatoweka, lakini tukitumia Ziwa Tanganyika tutaweza kupata maji mengi kama wanavyopata maji kwa kupitia Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, milioni 50 zitakazopelekwa kwenye kila kijiji naomba Serikali ipange utaratibu mzuri. Mimi natokea huko vijijini, wanawake wamejipanga kuzisubiri shilingi milioni 50 lakini elimu hawajapata. Naomba elimu ipelekwe, watu wajiandae ni jinsi gani watapokea hizo pesa na kuziendeleza zisiwe kama pesa za JK, kwa sababu wengine watazipokea watafikiri ni zawadi wakati zinatakiwa pesa zile zikifika kule upangwe utaratibu ili ziweze kukopeshwa kwa watu wengine baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu afya. Wananchi kwa kushirikiana na Serikali walijenga vituo vya afya, wakajenga zahanati lakiniā¦
Mheshimiwa Naibu Spika, hazijaweza kukamilika naomba Serikali ipeleke pesa ili vituo vya afya na zahanati ziweze kukamilika. Naunga mkono hoja.