Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja hii ya Wizara Fedha. Vilevile na mimi nimuunge mkono mjumbe aliyepita kwamba Mheshimiwa Naibu Spika uzi ni huo huo, sheria ni msumeno. Lazima Bunge letu lifuate sheria na kanuni ambazo tumejitungia sisi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze sasa na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wake na watendaji wote wa Wizara kwa kutuletea hii bajeti ili tuweze kuijadili. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais ambaye kwa kweli utumbuaji wake majipu umesaidia sana kuongeza kipato TRA na kwa kweli hakuna mtu ambaye hajui kwamba tumbuatumbua majipu imeweza kutuongezea kipato kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu naanza na kitabu cha Waziri ukurasa wa 59 kuhusu Shirika la Bima la Taifa (NIC). Kwa kweli nina masikitiko makubwa sana na inaniuma sana. Hili Shirika la Bima lilikuwa shirika ambalo lilisaidia sana nchi hii, wafanyakazi wengi waliweza kuajiriwa, lilikuwa na majengo mengi na mali nyingi sana ambazo leo hii lingeweza pia kuongeza pato kubwa sana katika nchi hii. Hata hivyo, bado Serikali haijawa na mpango haswa wa kuhakikisha kwamba hili shirika linafufuka ili liweze kuwa chanzo kikubwa sana cha mapato katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika bajeti iliyopita ya mwaka 2015/2016, aliyekuwa Waziri wa Fedha alipokuwa anasoma bajeti yake alituambia kwamba Serikali ina mpango wa kuongezea uwezo Shirika la Bima la Taifa kwa Serikali kukatia bima mali zake zote ikiwa ni pamoja na za taasisi na TAMISEMI kupitia shirika hili. Mbona sasa hakuna mpango wowote wa kuhakikisha kwamba haya mashirika yanakatiwa bima katika Shirika hili la Bima? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuamini mpaka sasa hivi hili shirika halina hata bodi ya wafanyakazi, shirika hili Mkurugenzi wake Mkuu na Wakurugenzi wengi sana wanakaimu tu, sasa kweli hili shirika litajiendeshaje kama bado halijajiwekewa mkakati kama huo? Tuna taasisi karibu 200 katika nchi yetu lakini katika kitabu hiki amesema taasisi 15 tu ndiyo ambazo zinatumia hili Shirika letu la Bima ya Taifa. Niipongeze sana Wizara ya Nishati kwamba imeweza kukata bima katika bomba lake la gesi linalotoka Mtwara mpaka Kinyerezi. Najua ni mapato makubwa sana yanapatikana kwa kukatia bima kwenye Shirika letu la Bima la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unajua siku zote huwa tunawasifia Wachina wanaongeza pato na sisi tulienda kweli tukaona Wachina jinsi walivyokuwa wazalendo. Kama nchi hii haitakuwa na uzalendo mashirika yetu mengi sana yatakufa. Kwa sababu ipo TTCL, Posta bado hatutumii mashirika yetu vizuri, tunaona mashirika na taasisi za Serikali zinaenda kukata bima sehemu nyingine. Unaona tu Wachina wamekuja hapa wamewekeza lakini wameleta pia mashirika yao ya bima, wameleta pia walinzi wao, wameleta kila kitu mpaka wafagiaji. Lazima iwepo sheria kwamba haya mashirika yetu ya bima yatumike pia ili kuongeza Pato la Taifa letu. Nitamuomba Waziri atakapokuwa anajibu angalau atupe mkakati kwamba ana mkakati gani wa kuyafufua haya mashirika na ni kwa nini mpaka leo hii hakuna hata bodi ya wafanyakazi kwenye hili shirika na Wakurugenzi bado wanaendelea kukaimu siku zote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi pia niendelee kuunga mkono kuhusiana na ile Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2011. Wabunge wengi sana siyo leo tu, siku zote tumekuwa tukiisema hii sharia, kwa nini hailetwi, kuna kitu gani kimejificha hapa nyuma? Kwa sababu hii sheria ingeletwa leo hii tusingekuwa tunalalamika, hii sheria ndiyo mkombozi. Naomba Mheshimiwa Waziri atujibu, tulipewa matumaini kwamba katika Bunge hili hii sheria ingekuja tungeweza kuibadilisha, mbona hakuna chochote, kuna tatizo gani katika uletaji wa hii sheria hapa Bungeni?
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia kuhusu VICOBA, hakuna siri VICOBA ni mkombozi wa sisi wananchi hasa wanawake. VICOBA hii imetufichia mambo mengi sana, wanawake walikuwa wanadhalilika sana kwenye taasisi nyingine za fedha kwa kuchukuliwa mali zao lakini VICOBA imekuwa kama ndiyo mkombozi. Tuliambiwa kwamba VICOBA inaendeshwa bila kusimamiwa na sheria yoyote ya fedha na tuliambiwa sheria ingeletwa hapa ili tuweze kuipitisha lakini hakuna sheria iliyoletwa mpaka leo. Sasa wanatuambia nini kuhusiana na VICOBA kuendeshwa bila sheria yoyote ya fedha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia kuhusu malipo ya wazabuni. Wazabuni wetu wanapata shida sana, ningeomba kujua ni lini Serikali italipa malipo wazabuni wanaozidai kwa muda mrefu sana Halmashauri na Wizara zetu. Wamekuwa wakizungushwa mno, wanaambiwa kwamba malipo yao yapo Hazina lakini wakienda Hazina bado hawalipwi, lakini hao wazabuni bado pia wanadaiwa kodi za Serikali. Sasa tutakusanyaje kodi kama hatuwalipi hawa wazabuni, watafanyaje biashara? Hawa wazabuni wamekuwa wakichukua mikopo kwenye benki, wanadaiwa riba, halafu TRA bado wanawatoza tena kwa nini wamechelewesha kulipa kodi zao. Serikali hii imesema kwamba itawasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati, huko ndiyo kuwasaidia wazabuni? Kwa sababu wazabuni walio wengi ndiyo ambao wanatoa zabuni kwenye Halmashauri zetu na kwenye Wizara zetu. Ningeomba kwa kweli uwepo mkakati wa kushughulikia suala hili kwa sababu ni muda mrefu sana wazabuni wamekuwa wakipata matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pia kuzungumzia kuhusu ucheleweshaji wa pesa za miradi katika Halmashauri na Wizara zetu. Huu ucheleweshaji siyo wa mara moja, siku zote pesa za maendeleo ya miradi zimekuwa zikicheleweshwa sana na ucheleweshaji huu wa miradi umekuwa ukisababisha miradi ile sasa inafanyika kwa gharama kubwa sana. Kwa mfano, katika Mkoa wetu wa Iringa kuna ule mradi wa machinjio wa kisasa, ulitakiwa tuujenge kwa pesa kidogo sana, lakini kadri fedha ambavyo zinacheleweshwa kuletwa ule mradi pia gharama zake zinaongezeka. Pia ule mradi kama tungekuwa tumeumaliza kwa wakati ungeweza kusaidia chanzo kikubwa cha mapato kwa sababu tunategemea kwamba tutapata mapato hata ya dola kwa sababu tutasafirisha zile ngozi nje ya nchi.
Vilevile tulikuwa tunategemea kuajiri wafanyakazi wengi sana katika Halmashauri yetu kupitia mradi ule. Sasa utaratibu gani huwa unatumika, ni kwa nini hizi pesa za miradi zinacheleweshwa sana? Karibu sehemu zote watu wanalalamika ucheleweshaji wa pesa katika miradi ya Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wengi sana wamezungumzia kuhusu riba kubwa inayotozwa na baadhi ya taasisi za fedha. Taasisi nyingi sana zimekuwa zikitoza riba kubwa sana na wananchi wengi sana wanashindwa kufanya biashara.
Wananchi wengi sana sasa hivi wakichukua mikopo benki mali zao zinauzwa, imesababisha wananchi wengi sana kupoteza maisha au kupata hata pressure kwa sababu mikopo halipiki dhamana zinachukuliwa. Ukichukua sasa hivi mkopo benki ujue kwamba wewe umeajiriwa na benki hupati chochote zaidi tu utafanya ile kazi, kama umechukua kwa ajili labda ya uzabuni basi utafanya kazi ya uzabuni, zabuni yenyewe wanakusumbua.
Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie upya hizi riba ambazo mabenki yetu yamekuwa yakitoza, ikae na ione ni kiasi gani ambacho kinaweza kikasaidia. Kwa sababu biashara ni ngumu sana, watu wanatozwa katika majengo, kuna tozo nyingi mno ambazo ukienda kuchukua mkopo unaona riba imekuwa kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nizungumzie kuhusu hizi mashine za EFDs. Wengi wamezungumzia suala hili, tulitegemea kwamba hizi mashine zingekuwa mkombozi, tungekusanya kodi nyingi sana. Tatizo utaona labda mtu mmoja au wawili ndiyo wana zile mashine wengine hawatumii, kwa hiyo, wengine wanalipa kodi wengine hawalipi, naomba hili suala liangaliwe. Pia Serikali ilisema ingetoa hizi mashine bure sijui zoezi hili limefikia wapi, ningependa kujua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nakushukuru.