Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muleba kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kutupa dakika tano tano kuonesha kwamba ni dakika za majeruhi. Katika dakika tano sijui nitasema nini! Bora niseme tu kwamba naunga mkono hoja ila ningependa yafuatayo yazingatiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa suala zima la kupeleka ukusanyaji wa kodi ya majengo TRA kunaleta ukakasi mkubwa. Hili nalisema kwa sababu ya utaalamu wangu kama mchumi, kimsingi naona halitekelezeki, kwa sababu litaleta mtafaruku mkubwa sana katika kugatua madaraka kwenda katika ngazi za Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili naomba mlione, najua wengi labda hatujalitafakari vizuri, lakini naomba kwa sababu nina dakika tano nalisema kama lilivyo, tukipata nafasi tutalifafanua, halitekelezeki litatuletea matatizo makubwa. Ninavyomjua Mheshimiwa Rais wetu yuko katika „Hapa Kazi Tu‟ hatuwezi kurudi kwenye mwaka 1972 Mwalimu Nyerere alipoondoa mamlaka za Native Authorities ilikuja kuleta ukakasi akabadilisha mwenyewe mwaka 1982 na alibadilisha kwa kuomba radhi. Mimi ni mtu mzima ni lazima niwaambie mambo yalivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili Mheshimiwa Waziri ambaye ameleta hotuba nzuri, mambo ni mazuri lakini muda ni mfupi; kuna suala la mitumba.
Mimi hapa nawakilisha Mkoa wa Kagera imeshasemwa umefilisika. Mkoa wa Kagera watu wanafikiria kwamba, una fedha, hauna fedha. Kwa hiyo, lile andiko lako ulilotuletea Mheshimiwa Waziri liko sahihi, labda utuandalie semina watu waweze kukuelewa unavyopima umaskini, kwa sababu umaskini unaweza kuwa na hela leo kesho ukafilisika mambo yakawa hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mitumba ndiyo imeondoa aibu iliyokuwa inatukuta wakati Mheshimiwa Salim akiwa Waziri Mkuu watoto walikuwa wanavaa plastic bags! Mimi ni mtu mzima nimeyaona kwa macho! Kwa hiyo, nafikiria kwamba, mitumba viwanda tuvijenge, lakini tuende taratibu. Wanasema safari ndefu inaanza na hatua ya kwanza. Tusianze kujitutumua tukaleta matatizo makubwa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji limeshazungumziwa na mimi nakubali kwamba, hizo shilingi 50 ambazo zimependekezwa na Kamati ziwekwe zitusaidie. Akina mama wanateseka na ninarudia tena, haya maji mngekuwa mnachota wanaume mambo yangekuwa yameshakuwa mazuri zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la elimu ni la utata sana. Watu wanasema kwamba mtu atangaze mgongano wa maslahi! Mimi nilishawaambia mimi ni mdau wa elimu, sina mgongano wowote wa maslahi. Kuwaambia kwamba kodi ambazo zimewekwa kwenye shule binafsi ni sawasawa na kuziua hizi shule binafsi. Kwa hiyo, ni lazima tuziangalie hizi shule binafsi tuziwekee uwezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, TRA wanafanya kazi nzuri, lakini TRA siyo panacea, anasema mzungu. TRA is not a panacea for all our problems! Hawawezi kumaliza matatizo yote. Tusiwabebeshe mzigo ambao utawashinda. Wafanye kazi na Halmashauri na Halmashauri tuzibane. Hata ya kwangu ya Muleba inanipa headache kabisa, lakini nafikiria kwamba, mchango wangu ni kuiimarisha ile Halmashauri na siyo kuiondolea mapato yake na siyo kuiondolea kuiwezesha. Kwa hiyo, suala la kuwezesha ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu viwanda na biashara; nimeona bajeti ilipokwenda, iko kwenye miundombinu na hilo nashukuru, lakini kilimo na viwanda na miundombinu vinakwenda pamoja. Suala la kilimo, kwa mfano Mkoa wa Kagera, kodi za kahawa ziko palepale. Hapo Mheshimiwa Waziri utakaposimama utuambie maana Mheshimiwa Rais mwenyewe ndani ya jumba hili alizungumzia kodi 27 kwenye kahawa. Sasa kwenye kitabu chako naona kahawa ni kama haipo. Mkulima wa kahawa ataachaje kupeleka kahawa Uganda kama unamuacha alivyo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nimepewa dakika tano, ninakushukuru sana, lakini ninasema kwamba bajeti iliyo mbele yetu italeta ukakasi tutakapofika kwenye Finance Bill! Hatujafika kule, lakini itabidi tupewe muda tuangalie mambo yanayopendekezwa kwa kweli mengine yana-far reaching implications, hayawezi kuruhusiwa kwenda hivi yatatuletea matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo mchango wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sijui kama muda bado upo, lakini ninasisitiza suala la mitumba, ninyi hamjawahi kuwaona watoto ambao hawajavaa nguo, mimi nimewaona kwa hiyo, lazima tuwalinde kabisa tuende pole pole, viwanda tuvijenge, lakini wanasema subira yavuta kheri. Nashukuru sana kwa kunipa muda.