Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karagwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha vizuri, vilevile nitakuwa mkosa fadhila nikianza kuchangia Mpango bila kwanza kuishukuru Serikali kwa jitihada wanazoendelea kuzifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli; Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu; Waziri Mkuu wetu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa; na Baraza la Mawaziri lote kwa jitihada wanazoendelea kuzifanya kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Kagera na janga la tetemeko la ardhi lililotupata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimshukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wabunge wote kwa kuguswa na kwa mchango wenu mlioutoa katika kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Kagera. Pia niishukuru Serikali kwa jitihada za kidharura ambazo wanaendelea kuzifanya kuwasaidia wananchi wa Wilaya ya Karagwe kwa janga la njaa lililotupata lililosababishwa na ukame wa muda mrefu ambao haujawahi kutokea katika historia ya Karagwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada za Serikali, nipende kuiomba Serikali ili kuwaondoa wananchi wa Karagwe kutoka kwenye utegemezi wa kuomba chakula Serikalini, Serikali ishirikiane na mimi na Waheshimiwa Madiwani kuhakikisha tunajenga mpango mkakati wa kati na wa muda mrefu wa kuwasaidia wananchi wa Karagwe kutoka kwenye utegemezi wa kuomba chakula, kwenda kwenye kujitegemea kama tulivyokuwa kabla ya kupata janga la njaa ambalo limesababishwa na ukame na ukame umesababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Serikali ituletee chakula chenye bei ya ruzuku haraka iwezekanavyo ili wananchi wengi wa Karagwe waweze kupata chakula, hasa maharage na mahindi, Serikali ituletee mbegu za mazao yanayostahimili ukame, taarifa tumeshaiwasilisha kwenye Kamati ya Maafa ya Taifa. Naiomba Serikali iifanyie kazi haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itusaidie kutatua migogoro ya ardhi, hasa migogoro mikubwa. Kuna mgogoro wa Kihanga ambapo Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja alipokelewa na halaiki kubwa ya wananchi wa Karagwe na akaiagiza Serikali ifanye haraka iwezekanavyo kuhakikisha zile hekta 2,000 ambazo wananchi wa Kihanga waliahidiwa toka NARCO ziende kwa wanakijiji, lakini mpaka hivi sasa maelekezo haya hayajafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali itusaidie, pori la akiba la Kimisi usimamizi wa kisheria umekuwa siyo usimamizi wa kisheria, umekuwa ni double standard, kuna mifugo mingi inatoka sehemu mbalimbali za nchi, kuna mifugo kutoka nchi za jirani iko Kimisi, lakini mimi na Waheshimiwa Madiwani tumekuwa tukiwaambia wananchi wetu wa Karagwe kwamba lazima watii utawala wa kisheria na ng‟ombe wao wasiingie mle Kimisi, sasa kinachoendelea ni double standards.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, kama lile pori la akiba la Kimisi wameshindwa kulitumia kwa tija na kwa kufuata misingi ya sheria, basi lirudishwe kwa wananchi kupitia Halmashauri ili katika Baraza la Madiwani tukae na kupanga matumizi bora ya kutumia hili eneo kwa kuzingatia sasa hivi Karagwe tuna tatizo la ukame, tunahitaji ardhi ya ziada kwa ajili ya kulima na kufuga. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali, tengeni eneo la pori la akiba la Kimisi angalau wananchi wangu wa Karagwe wapate eneo la kulima na kufugia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niiombe Serikali itusaidie, tuna Kata sita ambazo zina maji ya kutosha, tuwasaidie wananchi wa Karagwe waende kwenye kilimo cha kujitegemea. Serikali ilete wataalam waangalie ni namna gani tunaweza tukafanya kilimo cha umwagiliaji katika Kata ya Bugene, Kanoni, Kamagambo, Boranyange, Nyakakika na Lugu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nichangie mapendekezo ya Mpango. Hapa kikubwa sana, hasa ni kuangalia katika vile vipaumbele vinne. Napenda kuishauri Serikali mwisho wa siku tutapimwa ni namna gani maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu vimefungamana. Sasa, katika hili bahati mbaya sana tumekuwa tukitumia GDP kama kigezo cha kuangalia uchumi wa nchi unakuaje, siyo Tanzania tu ni dunia nzima. Bahati mbaya sana, kupima GDP kama kigezo cha maendeleo siyo kipimo kizuri kwa sababu ukiangalia ukuaji wa uchumi kwa takwimu tu hali yake haifanani na hali ya mtaani. Matokeo yake, taarifa zinakuwa zina takwimu nzuri lakini hali ya maisha ya wananchi haibadiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali katika Mpango wa kuwa na uchumi wa kati ifikapo 2025, katika malengo ya kuwa na uchumi wa viwanda, nirudie kwa mara nyingine; tujikite kwenye shughuli ambazo zinawahusisha Watanzania wengi na si shughuli nyingine bali ni Sekta ya Kilimo na Mifugo, ujasiriamali mdogo na wa kati, pamoja na mnyororo wa mazao yaani value chain ya mazao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iwapo Serikali itajikita katika maeneo haya matatu, kilimo na mifugo, biashara ndogo na kati na value chain ya mazao, tutakuwa tumewagusa Watanzania wengi zaidi ya asilimia 70 na tutakuwa tunakwenda kwenye mwelekeo mzuri wa kufikia uchumi wenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025, lakini tukiendelea kusaidia zile sekta ambazo multiply effect yake ni ndogo, kusema ukweli inaweza kufika 2025 bado tukawa tunaulizana maswali magumu humu Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusisitiza sana, kwenye upande wa value chain ya mazao lazima tuangalie ni namna gani tunawasaidia wananchi wa Tanzania kutoka pale walipo hata kama ni hatua ndogondogo lakini ni hatua ambazo zinamsaidia kila Mtanzania kukuza kipato chake popote alipo katika shughuli hizi ambazo anajishughulisha nazo. Baada ya ku-focus katika hivi vipaumbele vitahakikisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu vinafungamana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika hili lazima tuweke mazingira wezeshi, mikopo ya bei nafuu katika hizi sekta ambazo nimezitaja. Kwa mfano; tuna Benki ya Maendeleo ya Kilimo; mpaka hivi sasa ina bilioni 60 tu. Ukiangalia kwa vitendo kama kweli tunataka kusaidia kilimo na mifugo kwa kuwapatia wananchi wetu mikopo ya bei nafuu, lazima tuiwezeshe Benki ya Maendeleo ya Kilimo ipate mtaji wa kutosha iwasaidie wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna VICOBA Vijijini na Mjini kuna SACCOS, tuzisaidie zipate mitaji ya bei nafuu ili ziweze kukopesha vijana na akinamama vijijini na mjini ili waweze kutumia mitaji hii kufanya shughuli ambazo wanajishughulisha hata kama ni kidogo lakini multiply effect yake ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hatuwezi kupata maendeleo endelevu katika mpango wetu wa kuwa na uchumi wa kati kama hatuwekezi kwenye rasilimali watu. Niipongeze Wizara kwa kuliona hili katika mapendekezo ya mpango, lakini hii haitoshi. Kwa mfano, hivi sasa kuna wanafunzi wengi sana Vyuo Vikuu wanasubiri kupewa mikopo Serikalini, sasa tukifanya kwa vitendo kuonesha namna gani tunawekeza katika rasilimali watu tunatakiwa tuhakikishe katika Taasisi zetu za Vyuo Vikuu ili Taifa na work force ambayo tunaiandaa tunaiwezesha kupata mikopo ili waweze kusoma na tuweze kutumia hii work force kusaidia uchumi wetu na kusaidia kwenda kwenye malengo ya uchumi wa kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma taarifa ya ndugu zetu wa Upinzani. Niwapongeze, wana mapendekezo mazuri, lakini katika taarifa yao wamesahau ku-acknowledge kwamba Serikali yoyote makini kuna transition period. Toka Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikijipanga kuhakikisha inatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kama tulivyowaahidi wananchi na Watanzania wana imani sana na Serikali ya Awamu ya Tano, watupe muda tunajipanga, Serikali ni sikivu na naamini kabisa tutawavusha Watanzania kama tulivyoahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.