Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Wilfred Muganyizi Lwakatare

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Bukoba Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami pia nitumie fursa hii kushukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge wote, Mheshimiwa Spika, niwashukuru Wabunge wa CHADEMA na UKAWA pia Wabunge wa Chama cha Mapinduzi na pia Chama changu na hususan Mjumbe wa Kamati Kuu, Mheshimiwa Lowassa. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Abdallah Bulembo wa CCM, pia taasisi za ndani na nje ya nchi, makampuni mbalimbali, Mabalozi na watu binafsi ambao kwa kweli walitukimbilia katika Mkoa wetu wa Kagera kuweza kutoa misaada mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru sana Waziri Mkuu, pamoja na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani ndani ya Bunge, Mwenyekiti wa NCCR pamoja na Mawaziri mbalimbali wa Wizara nyingi ambao walitukimbilia katika Mkoa wetu kwa ajili ya kuangalia kwa karibu lile janga lililotupata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge lako na kupitia kwa Baraza la Mawaziri, Mawaziri waliopo hapa na hususan Waziri Mkuu niombe wamfikishie ujumbe Mheshimiwa Rais kwamba kutofika kwake katika Mkoa wetu na kuangalia majanga na kuhudhuria msiba ambao kimsingi unamhusu sana, niseme kabisa bado haijaingia akilini kwa wananchi wa Kagera. Wengi wanatoa tafsiri nyingi, nyingine huenda ni za kweli, nyingine huenda ni za uwongo, lakini ili kumaliza biashara hiyo na kuweza kuweka wigo vizuri, mimi binafsi nawasilisha kilio hicho cha wananchi wa Kagera, ni vema angefika. Kwa sababu kutofika kwake watu wengine wanafikiri yale majanga ni mepesi, kufika kwa Rais kutaweza kufunua macho watu wengine ambao wanataka kutusaidia sisi kama Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme majanga yale ya Mkoa wa Kagera yaliyotokea ya tetemeko, kama mtu hajafika kule hawezi kujua ukubwa wa tetemeko lile. Ndiyo maana katika mpango huu ninapozungumza hapa kwa niaba ya watu wa Bukoba Town na Mkoa wa Kagera kwa ujumla na hususan niliposoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba yatakayozingatiwa katika kukamilisha mpango na mwongozo ni pamoja na: nachukua kipengele cha kwanza: “Kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa mpango na miradi ya maendeleo”. Kipengele pia cha nne: “Kuchagua miradi michache ya kipaumbele kwa kuzingatia uwezo wa kibajeti.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huo mambo niliyojifunza katika janga la tetemeko la Kagera, ni kwamba kwa kweli mipango yetu haijajiandaa katika kukabiliana na majanga au maafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inatia aibu kwamba majanga yanatokea kama lile tetemeko halafu Kitengo cha Maafa hakina hata senti tano, kinaanza kutegemea hela ya kuchangiwa na kutembeza kapu, matokeo yake shida haina mwenyewe, haingojei, ni kwamba watu wanatakiwa kupata msaada wa haraka hawapati. Kwa hiyo, ningeomba katika mpango huu nilichojifunza kwa tetemeko la Kagera ni kwamba Serikali ilikuwa haijajipanga na bado haijajipanga kwa sababu matatizo bado ni makubwa kweli. Tuone kwamba janga hili linaweza likatokea wakati wowote na kwa bahati mbaya kama nilivyowahi kueleza huko nyuma na Naibu Waziri wa Fedha akanijibu Mkoa wa Kagera majanga makubwa ya Kimataifa na ya Kitaifa yamekuwa yanaanzia kule, sasa funga kazi imekuja kwenye hili la tetemeko!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Naibu Waziri wa Fedha alikiri kwamba Kagera ina matatizo na ile kuwa maskini kati ya mikoa mitano kuna sababu za kihistoria na tumezijata hapa. Sasa kumeongezeka tetemeko, kwa hiyo hapa kwa kweli hebu jaribuni kusaidia na mpango uje mahsusi kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri yeye alinihakikishia kwamba watatuweka kwenye Big Result Now (BRN), Big Result Now ianze kuonekana kwenye mpango wa kutunusuru hili janga la tetemeko. Kwa wataalam ambao wamefika pale na namshukuru Mheshimiwa Mbatia alisema kabisa ili kurudisha uchumi wa Kagera katika mstari wake baada ya janga la tetemeko kunahitajika si chini ya shilingi trilioni mbili, sasa shilingi trilioni mbili siyo hela ya mchezo bila kuiweka katika mpango mahsusi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia imeelezwa na wataalam kwamba lile janga litachukua zaidi ya miaka 10 kurudi kwenye mstari kama kweli Serikali itakuwa ina mpango mahsusi. Naomba wakati anapo-windup au wakati unapopanga mipango ya kuelekea huko mbele, basi Mkoa wa Kagera uainishiwe kabisa hatua za makusudi ambazo zitachukuliwa ili kutunusu katika umaskini ule uliopita kwa sababu zilizotajwa na hili janga la tetemeko ambalo limetupata hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningeomba kuzungumza ni kwamba, lile tetemeko linahitaji mipango ya short term, medium term na long term. Sasa short term ni hii ambayo imeanza kufanyika ingawa nayo haichukuliwi hatua kwa umakini. Hata hivyo, nianzie kusema kwamba, kuna mambo mengine ambayo nimejifunza yanayoleta matatizo. Kuna matamko yanayokinzana ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali baada ya kuzidiwa na suala la kuwahudumia watu walitoa tamko kwamba michango mingi ambayo ilikuwa inakusanywa chini ya Kamati ya Maafa, walieleza kwamba ile michango itaelekezwa zaidi kukarabati na kurejesha miundombinu pamoja na kukarabati taasisi za umma na wakatoa tamko na clip ninazo hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba wakasema watu waanze kusaidiana wenyewe katika kukabiliana na tatizo hili, Serikali haitakuwa na uwezo, tukalipokea. Baada ya siku mbili nyumbani kwangu kulijaa watu wanamlilia Mbunge, kwamba Mbunge wewe ndiyo mtu wa kwanza kutusaidia zile kura walizonipa zaidi ya 25, 000 si mchezo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge kwa umakini wake akaweka mipango ya kuanza kuwasaidia watu wake nikaandika barua na naiweka kwenye table naomba ije ichukuliwe iwasilishwe, nikaandikia marafiki zangu na sehemu ya wale walionichagua wanisaidie; nashukuru baadhi yao walionisaidia licha ya wapiga kura hata Wabunge bila kujali vyama vyao, hata wa CCM wakaanza kunisaidia na kwa kuogopa hela mimi nisizishike mkononi nikawaelekeza wanunue vitu vinavyohitajika, maturubai ambayo Serikali ilishindwa kuwapa watu wananyeshewa mvua, wanapigwa na baridi, nikawaomba wawape watu wangu mablanketi, wawanunulie kwenye maduka, wanipe vifaa
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu nilichojifunza watendaji wenu mmewatia nidhamu ya woga, watu wana woga sijawahi kuona na nakala ya barua hiyo nikampelekea Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa, Mkuu wa Mkoa kwa kumweleza utaratibu wangu mimi kama Mbunge ambaye nimeapishwa hapa ndani ya Bunge, kwamba utaratibu wangu wa kuwasaidia watu ni huu, marafiki zangu wanataka kunisaidia, lakini nilishangaa barua hii ikawa ni kigezo eti napelekwa Polisi Lwakatare atafutwe eti ananzisha utaratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mbunge ambaye nimeapishwa ndani ya jengo hili kwa Katiba, Rais ameapishwa pale uwanja wa Taifa wote kwa Katiba, hivi kama siwezi kuaminika na kukimbiliwa na wananchi wangu nani awakimbilie? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri kinacholeta matatizo ni watendaji wenu mmewajaza woga, mnawatumbua bila utaratibu matokeo yake wanashindwa kusimamia hata kazi mnazowapa matokeo yake tunakimbizana huku na huko. Sasa na mipango hii tunayoipanga hapa tusipowaondolea watendaji wetu woga, mipango ya Mheshimiwa Waziri itapwaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuleta maombi maalum kwenye mipango ambayo itapangwa na hili naomba niliwasilishe kupitia hapa, kwanza niseme kabisa nimeombwa na wananchi wangu niliwasilishe hili la kwanza tunaomba sisi kama Kagera tupewe tax holiday kwa kipindi maalum (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni miaka mitano, miaka kumi kwamba bidhaa za ujenzi zipunguzwe bei. Hili jambo si la kwanza, tunakumbuka enzi za Mwalimu wakati tukianza kujenga Makao Makuu Dodoma uliwekwa utaratibu kuwashawishi wafanyabiashara waweze kuja kuwekeza Dodoma na cement ikawa imepunguzwa bei, vifaa vya ujenzi vikapunguzwa bei ili watu wajenge. Katika hili ili kuweka utaratibu mzuri na watu wasichakachue viwanda vilielekezwa kuwekwa alama maalum, nembo maalum. Sasa wananchi wa Kagera tunajua Serikali haiwezi kutujengea sisi wote na janga ni kubwa, tunaomba iwekwe tax holiday kwa bidhaa za ujenzi ili wananchi wajijengee badala ya kubaki ombaomba, hili ni janga kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili wafanyabiashara wameniomba, kuna wafanyabiashara wanaidai Serikali zaidi ya bilioni moja, wamewakopa wametoa huduma mbalimbali za ku-supply hawajalipwa zaidi ya miaka minne. Hawa ndiyo matajiri wetu wa Mji wa Bukoba, ndiyo wenye majumba yaliyoanguka, hawakopesheki tena na kwa bahati mbaya nyumba wanasema haziwekewi bima kwa suala la tetemeko, kwa sababu ni natural disaster. Sasa wamenituma katika suala la kulipa kwenye majanga na wafanyabiashara hao muwaweke kwenye package ya kuwalipa ili hawa watu warudi kwenye reli, vinginevyo wamefilisika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu kuna watu walikopa kwa kutumia nyumba ambazo zimeteketea tunaomba Mheshimiwa Waziri katika mpango wake alitolee tamko kuzielekeza taasisi na mabenki yaliyokuwa yanawadai wananchi wa Bukoba na Kagera kwa ujumla waliopata janga, nyumba walizoweka kama security zimebomoka, zimeanguka wanafanyaje au mnataka wajinyonge? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la misaada inayotolewa, tunaomba misaada inayotolewa kama Serikali imeamua misaada yote kuweka kapuni, hili suala linajaribu kuwazuia na kuwa na walakini kwa wachangiaji wengine, pale mnapochanga kwa mgongo wa waathirika lakini kapu lote linaelekezwa kwenye kujenga taasisi za umma bila kwenda kuwasaidia waathirika wenyewe. Kama mmeamua kufanya hivyo basi watu wasiendelee kujitoa na kuingia mitini kutuchangia tuweke makapu mawili wanaochangia Serikali na wale wanaotangaza kuchangia waathirika wachangie waathirika kuliko kuweka kapu moja vinginevyo watu wanaona mmetumia matetemeko kama chanzo cha mapato ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano, tunaomba bajeti ya maafa ieleweke, katika mpango wa Mheshimiwa Waziri suala la maafa ajaribu kulitengea fedha zinazoeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la sita, wananchi wa Kagera wamenituma na bahati nzuri hili suala nilishafika hata kwa Waziri Lukuvi, wanasema mwaka kesho pale Luguruni kuna makampuni mbalimbali toka duniani kote yanakuja kuonesha nyumba za bei nafuu na ambazo ni earthquake proof, nyumba ambazo hazizidi milioni nne mpaka milioni tano.
Tunaomba zoezi hili lianzie Kagera ambako nyumba zaidi ya 3000 zimekwisha, tunaomba nyumba hizi zije na iwekwe mipango mahsusi ambayo inaweza ikazi-attract hizi taasisi mbalimbali kuweza kuanzisha mpango huu ukaonekane Kagera ambako zaidi ya nyumba 4000 zote zimeteketea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya suala la mwisho kabisa, ni kuhusu suala la njaa, Mheshimiwa Bashungwa amezungumzia suala la njaa; Karagwe wanalima na Kyerwa, Muleba wanalima na mikoa mingine wanalima, wanaonunua ni watoto wa Bukoba Town bidhaa zote zinaingia mjini sisi ndio wanunuzi, sasa huko wote wamepigwa na njaa tutanunua nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bukoba kuna njaa na Mkoa mzima wa Kagera una njaa, ukame unatumaliza. Tunaomba Mheshimiwa Waziri katika mipango yake na Waziri wa Kilimo nilisikitika alikwenda Karagwe tu, lakini janga la njaa liko mkoa mzima, tunaomba mipango kabisa ipangwe kabla ya wananchi hawajateketea na bahati mbaya wananchi wa Bukoba Mjini huwaga hatupendi kulialia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.