Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nianze kwa kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu changamoto ambazo ziko mbele yetu na kimsingi maendeleo ni matokeo ya mgongano wa mambo mbalimbali. Kwa hiyo, tunapozungumzia habari ya maendeleo tusiogope kukumbana na changamoto mbalimbali, la msingi ni tunafanyaje kwa maana ya kukabiliana na changamoto hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kufuatilia taarifa ya Kamati lakini hotuba ya Waziri na taarifa ya wenzetu kwa maana ya Kambi ya Upinzani, nimefarijika kuona kwamba wote wazo letu ni moja, ni namna ya kumsaidia Waziri tutoke hapo tulipo twende kwenye hatua nyingine. Kwa hiyo, naendelea kusema tusiziogope changamoto, la msingi ni kukabiliana nazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshaji wa reli kwa maana ya miradi ya vielelezo. Nafahamu lengo zuri kwa maana ya uboreshaji wa reli ya kati kwa maana ya kuwa standard gauge ni jambo jema, lakini naomba twende mbali zaidi. Nitatoa mfano hai, leo hii pamoja na nia hiyo njema ya kuboresha reli lakini utakapoboresha reli mabehewa ikawa tatizo, suala zima la uboreshaji linakuwa limefanyika ndivyo sivyo. Nalisema hilo kwa sababu gani? Nitawapa mfano hai. Leo hii ukienda Mpanda, Katavi, treni zinakwenda kule kwa reli hiyo ambayo ipo kwa sasa hivi lakini shida kubwa ni suala la mabehewa. Wananchi katika maeneo yale wanakabiliana na changamoto kubwa ya mabehewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme shirika letu linatakiwa litoke hapo liende kwenye hatua nyingine ya mbele zaidi. Litoke kwenye mfumo ambao ulikuwa ukitumika toka enzi hizo za ukoloni liende kufanya kazi kibiashara zaidi. Nashangaa ukifika sehemu unaambiwa hapa tunahitaji abiria 40 tu, kama kuna abiria 100 wanasema idadi ya abiria wanaohitaji ni 40. Sasa wewe kama unafanya kazi kibiashara niliamini ungefurahia kupata abiria 100 badala ya ku-limit kuwa na abiria 40 kwamba abiria 40 ndiyo unaohitaji, 100 siku nyingine, wafanye kazi kibiashara. Nalisema hilo nikitolea mfano hai katika mazingira ya Mpanda, mabehewa ni machache, abiria ni wengi na kama shirika linataka kufanya kazi kibiashara ni kuongeza mabehewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la njaa kama fursa. Nilisikia wakizungumza kwamba nchi za jirani kuna maeneo mengine wenzetu kutokana na hali mbaya ya hewa suala la njaa linawakabili. Sisi Tanzania habari ya chakula Mungu katusaidia, je, tunafanyaje kutumia nafasi hii ya njaa kwa wenzetu kuwa ni fursa kwetu sisi ambao tuna chakula? Wanasema adui mwombee njaa. Kwa hiyo, naomba katika mazingira haya ambapo wengine wanakabiliwa na njaa kwetu sisi iwe ni fursa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoke hapo niende kwenye suala la ongezeko la watu. Nilikuwa nikijaribu kufuatilia data hapa, zinaonesha ongezeko la idadi ya watu kwa maana ya 2016 ni milioni 50.1 lakini itakapofika mwaka 2025 kutakuwa na watu milioni 63, namshukuru Mungu lakini ongezeko hili la watu linakwenda sambamba na mipango mingine ya maendeleo?
Naomba hilo tuliangalie. Tunazungumzia habari ya watu kuongezeka lakini vipi kuhusu mipango ya uzazi bora?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani watu waongezeke lakini wakiongezeka katika mazingira ambapo mipango mingine iko nyuma ndiyo tunarudi kwenye matatizo haya ambayo tumeendelea kuyaona kama migogoro ya ardhi kwa maana watu wameongezeka lakini ardhi haiongezeki, migogoro kwenye maeneo ya hifadhi na maeneo mengine ya namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba wakati tutakapokuwa tukiliongelea Taifa kwenda kwenye ongezeko hilo la watu liende sambamba na mipango mingine hiyo kama suala zima hilo nililolisema la uzazi bora, lakini tuangalie na masuala mengine kwamba tumejipanga vipi kwa maana ya matumizi bora ya ardhi ili kuepuka migongano tunayoiona sasa hivi ya wakulima na wafugaji na mambo mengine ya namna hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ya Serikali kuhamia Dodoma ni jambo jema, ni jambo la maendeleo, lakini naomba niendelee kushauri jambo moja na si kwa maana ya Dodoma tu ni kwa maana ya miji yote inayoendelea kukua Tanzania. Changamoto tulizoziona kwa Jiji la Dar es Salaam ni kwa kiwango gani changamoto hizo zimekuwa elimu kwetu kwa maana zisijirudie katika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na Dodoma, Arusha, Mwanza na kwingineko? Yale yote tuliyoyaona ya kuhusu watu kubanana barabarani, wanashindwa kufika makazini kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia tija, unapokuwa na watu wamechelewa kufika katika vituo vya kazi, muda mwingi wako barabarani tija utaipataje? Kwa hiyo, naomba wakati mpango mzuri huu wa Serikali kuhamia Dodoma ukifanyika tutoke hapo twende tukachukue yale yaliyojitokeza katika maeneo mengine na kwetu tusiyaogope, hayo yawe ni fursa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, habari kuhusu makusanyo katika majengo. Jambo hilo ni jema lakini ukifuatilia hata katika taarifa ya Kamati inasema hivi:-
“…kuhusu majengo ambayo hayajafanyiwa uthamini kukusanya viwango vya kodi vinavyofanana kwa majengo ya kila kundi. Vilevile katika ufanyaji tathmini, Serikali iangalie hali ya uchumi wa eneo husika, thamani ya ardhi na thamani ya nyumba yenyewe katika eneo husika”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hilo kwa sababu gani? Haki iende sambamba na wajibu, utakapotamani kupewa haki ya kodi na vitu vingine vya namna hiyo lakini ni kwa kiwango gani na wewe umetimiza wajibu wako? Kuna maeneo leo hii tunaweza tukatamani tupate kodi hiyo ya majengo lakini ni kwa kiwango gani Serikali hii imetimiza wajibu wake wa kuwapatia haki yao ya kimsingi wananchi wa maeneo husika kwa maana ya kuwapa hati husika za maeneo hayo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hilo kwa sababu gani? Kwa mfano, sehemu kubwa ya Mji wa Mpanda watu wanakaa katika majengo ambayo hayajafanyiwa uthamini na hivyo hawana hati za kumiliki maeneo hayo. Kwa hiyo, wakati tukiwa tunakusudia kwenda kuwaomba wananchi hawa watulipe kodi, basi Serikali iendelee kutimiza wajibu wao wa kimsingi wa kuhakikisha watu hawa wanapewa hati zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niendelee kushauri, fursa alizotupa Mwenyezi Mungu, fursa ya kijiografia kwa maana ya bandari tusikosee na kama kuna sehemu tumekosea tujirekebishe, fursa hii ni adimu. Niliwahi kuzungumza siku za nyuma nikasema tumependelewa na Mwenyezi Mungu kwa maana kijiografia tumejikuta hapa tulipo. Sasa pamoja na zawadi ya jiografia aliyotupa Mwenyezi Mungu tunashindwa kuitumia! Naomba tuitumie fursa hii, changamoto zote zinazojitokeza kwa maana ya bandari tuzirekebishe na iwe ni fursa badala ya kuwa adha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu mapendekezo yakiendelea kujirudia mara kwa mara bila utekelezaji panakuwa na shida hapo. Naomba mapendekezo mbalimbali haya tunayoyatoa basi yaonekane katika taswira ya utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niongelee suala la vipaumbele. Tukiwa na vipaumbele vingi mwisho wa siku tutajikuta tuna vipaumbele ambavyo havijafanyiwa kazi. Tunaweza tusiweze yote kwa wakati mmoja pamoja na nia njema, basi twende kwenye vichache ambavyo tutavifanya kwa kiwango kinachostahili na watu wakaona hili na hili limefanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji, niendelee kuishauri Serikali yangu. Nafurahi kuona wananchi wa Kanda ile ya Ziwa tukitumia chanzo muhimu cha Ziwa Victoria, maji yanaendelea kuwafikia watu katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo, naomba tena, Ziwa Tanganyika ni chanzo muhimu ambacho ametupa Mwenyezi Mungu, tuna sababu gani ya kuendelea kuhangaika na visima virefu ambavyo vingine hata hupati maji wakati tuna ziwa na maji unayashangaa yale pale? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba mipango ile ambayo inaendelea katika ukanda ule na siyo huko tu tukiiangalia nchi yetu yote kwa ujumla wake, naomba mpango huu hata kama utakuwa ni wa muda mrefu tufike sehemu habari ya maji iwe ni historia. Kwa sisi ambao tuna water bodies zimetuzunguka, una Ziwa Victoria pale, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa, sijazungumzia mito mikubwa habari ya maji iwe ni historia. Kupanga ni kuchagua, kama tumechagua kwamba sasa tunakwenda kupambana na habari ya maji, tupambane! Ndiyo maana nimetangulia kusema tuwe na vipaumbele vichache ambavyo tunaweza tukavifanyia kazi kwa kiwango kinachostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ulindaji wa bidhaa za ndani na walaji pia, napata tabu sana. Siku za hivi karibuni kupitia vyombo vya habari nimeendelea kuona hata bidhaa kama dawa sehemu ambapo pameandikwa muda wa matumizi wa dawa hiyo watu wachache wasiowapenda Watanzania hawa wanakwenda kufuta ili bidhaa hiyo iendelee kuwepo sokoni. Hata kama tutakuwa na mipango mizuri wakati afya ya wananchi wetu iko mashakani hiyo mipango ni akina nani watakwenda kuifanyia kazi? Kama hatutahakikisha tunalinda afya ya watu wetu, kama hatutahakikisha chakula wanachokula watu wetu ni kile ambacho kinastahili, mipango yote hii itakuwa haina maana kwa sababu mwisho wa siku wale ambao walikuwa ni walengwa watakuwa wameshazikwa wote na wamekwenda kaburini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, nakuja eneo la changamoto, si kwamba Mheshimiwa Waziri haya yote tunayoyazungumza hayasikii au hayaoni, kuna sehemu nilifarijika kuona ameandika changamoto na namna ya kuzifanyia kazi. Kwa mfano, kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi, nimefarijika kuona Mheshimiwa Waziri kumbe anafahamu huko kwenye eneo la kodi kuna mwanya mkubwa na hata hizi mashine tunazozungumzia sasa hivi watu wengine wajanja wanaziharibu kwa makusudi. Ukiliacha hilo, kuna maeneo unaweza ukaenda mashine ipo lakini hupewi stakabadhi kutoka kwenye mashine unapewa ambayo imeandikwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani twende kwenye hatua moja zaidi, inawezekana hata tungekuwa na mashine nzuri namna gani, hata tungekuwa na mipango mizuri namna gani kuhusu suala zima la kodi, hebu turudi kwenye mioyo ya watu, turudi kwenye suala zima la elimu ikamfikie kila mmoja kuhusu umuhimu wa kodi. Kwa sababu leo tunapozungumza kuna sehemu fedha imekosekana, mtu ajue kabisa kwamba yeye ni sehemu ya kutukwamisha kufikia kule tulikokusudia kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, elimu hiyo ikiendelea kutolewa na watu wafike sehemu kama ni makanisani, mashuleni wawe pia na hofu ya Mungu. Kwa sababu mimi naamini hata hizo nchi nyingine ambazo tunaziona zimepiga hatua ni wakali katika suala zima linalogusa kodi. Kwa hiyo, nataka kusema hilo nalo la changamoto ambazo Mheshimiwa Waziri ameziona tuendelee kuzifanyia kazi kwa mustakabali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nafahamu unaweza ukawa na bilauri ina maji yamefika katikati itategemea mtu anakusudia kuleta picha gani. Mtu mwingine anaweza akakwambia ameiona bilauri maji yako nusu lakini mwingine akakuambia ameiona bilauri imejaa maji lakini imejaa maji nusu. Kwa hiyo, yupo atakayekuambia haina maji nusu lakini yupo atakayekuambia ina maji nusu. Kwa hiyo, ni namna ya mtazamo tu kila mmoja anakusudia kulitazama jambo kwa namna gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.