Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mpango kwa kuleta mwelekeo wa Mpango huu, ili ujadiliwe na Bunge lako na mimi kupata nafasi ya kutoa mawazo yangu, lakini nasikitika itabidi nitumie sehemu ya muda wangu mzuri kuweza kueleza maeneo ambayo pengine yalikuwa very obvious.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya michango yetu inaonesha kwamba baadhi ya Wabunge tume-panic na Wabunge wengi tulio-panic tunaufanya umma wa Watanzania u-panic. Na ukifuatilia vitu vinavyotufanya tu-panic vinakosa mantiki na leo mbele ya Bunge lako Tukufu nalazimika kuongea kwa kutumia analogia kwa sababu ndio namna pekee ambayo nadhani nitaeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka kadhaa iliyopita hapa Dodoma watu wote wakiwemo Wabunge walikuwa wanakutana pale Chako ni Chako wanakula kuku. Miaka mitatu/minne baadaye sehemu mbalimbali zinazotoa huduma kama za Chako ni Chako zimefunguliwa na wateja wanachagua sehemu za kwenda, it is very natural. Miaka kadhaa iliyopita, labda kabla sijafika huko, kama unaishi mtaani, nasema ninatumia analogia, lugha rahisi kabisa na mifano rahisi, kama unakaa mtaani na katika mtaa wako unapakana na mitaa mingine minne/mitano katika mitaa hiyo mitano hakuna baa, kuna baa moja tu katika mtaa wako watu wote wanaokunywa katika maeneo hayo watakunywa katika baa yako, lakini siku mtaa wa tatu wamefungua baa tabia ya walevi ni kwenda kujaribu katika baa nyingine pia. Lakini wakiwa kule wataweza kulinganisha na ubora wa huduma ya baa yako; hiyo ndio lugha ya analogia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaendesha Bandari yetu ya Dar es Salaam bandari nyingine zimefuata baadae na kwa kawaida kwa tabia ya watu hupenda kujaribu. Leo bandari nyingine zipo kwa vyovyote vile huwezi kubaki na wateja wale wale ambao ulikuwanao kwa kipindi chote. Hiyo ni lugha rahisi, Watanzania tusiyumbishwe na kauli za baadhi ya Wabunge kuonyesha kwamba sababu za kupungua mizigo bandarini zinahusiana moja kwa moja na mambo ya kodi, si kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, hilo haliondoi jukumu la Waziri wa Fedha kuendelea kuchunguza sababu mbalimbali za kupungua wateja, lakini sababu nyingine ndio hizo. Lazima kazi ya ziada ifanyike ili kuweza kuvuta wateja zaidi na kuweza kuimarisha bandari yetu ili iweze kuchangia mapato zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana kuona baadhi ya Wabunge tunawalilia wafanyabiashara makanjanja. Ni ajabu kuona kwamba katika bandari ile ile ambayo tunasema kwamba mizigo imepungua, mapato yameongezeka, mantiki yake ni nini? Mantiki yake ni rahisi tu, wale ambao walizoea ubabaishaji wameenda kubahatisha maeneo mengine labda wakabahatishe kubabaisha. Lakini wafanyabiashara makini wanaendela kutumia bandari yetu na hao ndio wanaotupa mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la msingi kwenye eneo hilo ni upotoshwaji wa mantiki nzima ya kusimamia matumizi na kukusanya kodi. Humu ndani baadhi yetu wametafsiri kama kubana matumizi; sijaona mantiki, bajeti ya mwaka jana tunayoimaliza mwaka huu ni shilingi trilioni 29 na mpango huu unatupeleka kwenye shilingi trilioni 32. Hiyo sio kubana matumizi, Serikali ya Awamu ya Tano inachokifanya ni kusimamia matumizi, kuna utofauti kati ya kubana matumizi na kusimamia matumizi. Serikali inachokifanya ni kuhakikisha inaongeza efficiency katika matumizi ya fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale maeneo ambayo hayana tija Serikali imepunguza kupeleka pesa na badala yake imepeleka maeneo yenye tija zaidi. Kwa hiyo, Watanzania tuelewe kwamba hatujabana matumizi isipokuwa tunapeleka fedha maeneo yenye tija zaidi, maeneo ambayo yatakuza uchumi zaidi na ndio maana bajeti imetoka toka shilingi trilioni 29 kwenda shilingi trilioni 32, hiyo ndio mantiki, ni kusimamia matumizi. Sasa wale waliozoea fedha rahisi, wale waliozoea ubabaishaji hilo nalo linawaumiza. Niwaombe Watanzania makini, wanaolipenda Taifa hili wamuunge mkono Mheshimiwa Rais katika jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuhakikishia katikati ya giza nene ndipo inakaribia asubuhi, hapa tulipo ndipo wakati sahihi kunakaribia kucha. Mheshimiwa Zitto Kabwe alisema lazima kuwe na maumivu tunapotaka kufanya mabadiliko makubwa kama haya. Tukumbuke miongoni mwetu baadhi ya Watanzania walizoea fedha rahisi, walizoweza leo anaanzisha biashara ya shilingi milioni 10 na kila mwezi anapata faida ya shilingi milioni tano kwa sababu, alikuwa anakwepa kodi. Tumueleze mantiki ya kodi na tumueleze kwamba biashara zinakuwa steadly, hatua kwa hatua. Watanzania makini hawana tatizo na hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Mpango atoe ushirikiano na Mawaziri wengine waendelee kuasimamia matumizi ya Serikali na kuelekeza pesa katika maeneo yenye tija zaidi kwa Watanzania. Hilo lilikuwa kuweka tu mazingira sawa kwa sababu niliona linapotoshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa ambalo leo nilitaka nichangie ni dhana nzima ya kukuza viwanda. Katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi tumeweka bayana aina gani ya viwanda vitatutoa Tanzania kwa haraka zaidi. Tulisema tuwekeze kwenye viwanda vinavyosindika zaidi mazao ya kilimo kwa lengo kwanza la kumuwezesha mkulima mdogo apate soko la mazao yake, lakini pia kutoa ajira kubwa zaidi kwa Watanzania. Katika mpango tulioupata hilo halijawekwa bayana, tumeongelea viwanda vya General Tyre, tumeongelea viwanda vingine ambavyo kimsingi havigusi asilimia 80 ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosikitika kwenye mpango huu ni kwamba hatujaoanisha vizuri ile Ilani ya Chama cha Mapinduzi na huu mpango. Tunapowekeza nguvu nyingi kwenye kushughulikia viwanda tumesema ni jambo zuri, Magadi ya Soda - Bonde la Engaruka, tumeongea viwanda chini ya TEMCO na nini, lakini viwanda hivi katika ujumla wake haviendi kutatua tatizo la ajira kwa vijana wetu walio asilimia kubwa na wala haliendi kutatua tatizo la soko la mazao yetu ya kilimo. Kwa hiyo, niishauri sana Serikali kwenye hili lazima turudi tukafanye kazi upya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine kwa haraka haraka, tunahangaika sana na soko la mahindi ni vema katika mpango huu sasa ikawekwa bayana. Kinachomfanya mkulima akalime ni bei ya mazao. Tunatoa ruzuku, lakini bado wakulima hawazalishi kwa tija kwa sababu hawapati faida katika uzalishaji wao. Ipo haja sasa ya kuja na sera madhubuti itakayomfanya mkulima mdogo wa Tanzania awe huru kuuza mazao yake kokote na wakati wowote. Leo ukienda kila mahali pikipiki zimejaa, Serikali imetoa ruzuku sana kwenye power tiller, lakini huzioni kokote kwa sababu hazina manufaa
kwenye kilimo chao, lakini watu wangapi wananunua yebo yebo kwa sababu hizo bodaboda kwa sababu wanajua zinawalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutajenga mazingira mazuri kwenye sekta ya kilimo hatutahitaji kugharamia mbolea za ruzuku tena. Tujenge mazingira yenye ushindani kwenye sekta ya kilimo, tuwaache wakulima wadogo wauze mazao yao wanakotaka, anayetaka kupeleka Malawi, anayetaka kwenda Zambia na kama Serikali inataka kununua iingie kwenye ushindani. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumemuwezesha sana mkulima mdogo na wala hatutahangaika habari za kutafuta pembejeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia muda ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja.