Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kidogo kwenye mapendekezo ya mpango ambayo yako mbele yetu. Kwa sababu mengi yamezungumzwa na wengi sitazungumza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri anasema kwamba pato la wastani la kila Mtanzania kwa mwaka 2015 ilikuwa ni Sh.1,918,928. Nimekuwa najiuliza kwamba takwimu kama hizi zimechukuliwa kutoka katika maeneo gani? Kwa sababu kwa sisi ambao tunaishi na wananchi wetu vijijini wale ambao hawana uwezo wa kupata hata laki kwa mwezi, hawana uwezo wa kupata milo miwili ya uhakika kwa siku, unaambiwa kwamba kila Mtanzania ana uwezo wa kupata milioni moja na laki tisa, nadhani ni lazima Serikali inapochukua takwimu ichukue takwimu vijijini ambapo asilimia 80 ya watu wanaishi kule. Wakichukua takwimu za mjini hawawezi kupata hali halisi ya maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyoongea hali ni mbaya kwelikweli, ni matatizo matupu, ukiambiwa kwamba kila mtu ana milioni moja na laki tisa, unapata mashaka makubwa sana. Kwa hiyo, naomba kwenye takwimu nyingi za Serikali chukueni maeneo ambapo percent kubwa ya Watanzania inaishi kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la ongezeko la watu na nimekuwa nashangaa Serikali imekaa kimya sana kutokana na ongezeko kubwa la watu Tanzania. Ukiangalia kwenye sensa mwaka 2012 tulikuwa watu milioni 45 japokuwa wengine hawakuhesabiwa. Kwa takwimu za Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake 2016 tuko watu milioni 50.1, prediction 2025 tutakuwa watu milioni 63.
Mheshimiwa Mwenyekiti, spidi ya ongezeko la watu haiendani na spidi ya Serikali kutoa huduma muhimu, ni jambo ambalo liko wazi, haiendani kabisa. Ndiyo maana unaona leo wanafunzi wanagoma, mikopo haitoshi, huduma za afya hazitolewi kwa uhakika, elimu bado ni matatizo, Serikali inaogopa nini kuanza kuweka mikakati ya udhibiti wa ongezeko la watu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa nchi nyingine, China walivyoweka kwamba mwisho watoto wawili kuna factor waliziangalia na maeneo mbalimbali wanaweka idadi kwamba angalau mtu awe na watoto watatu mpaka wanne ili kuweza kutoa huduma. Haifai na haileti tija watu wazaliwe mshindwe kutoa huduma, ni kama sehemu ya familia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mzazi ukiwa na watoto kumi huwezi kuwapa elimu nzuri, huwezi kuwavalisha vizuri, huwezi kuwapa huduma nzuri, unawatesa. Simple applied kwa Tanzania kuendelea kuona idadi ya watu inaongezeka kwa spidi kubwa lakini Serikali hatuzungumzi chochote ni kuendelea kuwafanya watu wateseke bila sababu. Watu tuwe na watoto ambao tunaweza kuwahudumia vizuri angalau kila mwananchi apate huduma anazostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwenye suala la kufungamanisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu litekelezwe kikamilifu kwenye bajeti ijayo. Nikianza na mpango wa elimu, Serikali kweli imeanza na mpango wa kutoa elimu bure, tunatembea kwenye shule zetu bado fedha inayotolewa kwa retention haitoshi, changamoto ni lukuki katika shule zote. Kila unapokwenda ni kilio, Walimu wanalia wanafunzi wanalia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumetengeneza madawati, madawati maeneo mengi yako kwenye maturubai, yamewekwa shade kwa kutumia majani hakuna madarasa ya kutosha, lakini pia hakuna miundombinu ya nyumba za Walimu, hakuna vyoo, ukienda kwenye shule zetu bado changamoto ni nyingi sana. Kwa hiyo, kwenye bajeti ijayo lazima Mheshimiwa Waziri aje na mpango mkakati wa kuongeza miundombinu ya madarasa, nyumba za Walimu kwenye shule zetu za primary na secondary. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la kujenga vyuo vya elimu ya mafunzo, kwa spidi ambayo tunaongezeka nayo na kwa sasa hivi Serikali ambapo inasema division one na two ndio inaenda vyuo vikuu wengine wanaenda vyuo vya kawaida, vyuo vya mafunzo, wanafunzi wengi wanabaki vijijini, tunaulizwa maswali hatuna majibu. Tunaomba mpango ujao Mheshimiwa Waziri aje na mpango maalum kuhakikisha tunajenga vyuo vya VETA kwenye Wilaya zetu na atueleze ni vingapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye mpango huu hapa amesema mpango ni kumalizia chuo kinachojengwa Mahenge, haitoshi! Tunataka Wilaya zote ambazo hazina vyuo vya ufundi ni lazima vipate vyuo hivyo. Hii iende sambamba na kuweka karakana zinazoeleweka na miundombinu yote ili wanafunzi wetu wapate angalau stadi za kazi waweze kujitegemea kule vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la afya. Njia pekee ya kuondoa vifo vya akinamama na watoto, wazee na makundi mengine Tanzania ni kusogeza huduma karibu na walipo. Tulikubaliana na Serikali karibu miaka kumi sasa kujenga zahanati kila kijiji, kituo cha afya kila kata mpaka sasa hivi mpango huo bado unakwenda taratibu. Kwa hiyo, kwenye mpango ujao Mheshimiwa Waziri tunataka atuambie zahanati ngapi zitajengwa, za kutekelezwa siyo za kwenye vitabu, ngapi zitajengwa Tanzania nzima? Ni vituo vya afya vingapi vitajengwa kwenye kata zipi, zianishwe na zitekelezwe kwenye mpango ujao ionekane. Pia kuhakikisha kwamba tunapata watumishi wa kutosha na huduma zote muhimu zipatikane na vifaa tiba na dawa ziwepo za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la maji. Watu wanaongezeka changamoto ya maji inaongezeka kila siku. Tunaomba kwenye mpango ujao lazima Waziri atuambie namna gani ya kuondoa changamoto za maji kuendana na ongezeko la watu. Tusingependa mwakani tuanze kushika hotuba ya mwaka huu na ya mwaka kesho hatutaki kama ambavyo Serikali zilizopita. Tunataka tujue yaliyopangwa kwenye bajeti ya mwaka huu yawe yamepita ya mwakani tuwe na mipango mipya inayotekelezeka, tunaomba sana hilo. Kwa hiyo, lazima mipango mikakati ya maji ya kutekelezeka iweze kuletwa ndani ya Bunge, ianishe wazi na ikatekelezwe siyo kuja kubaki kwenye vitabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mikopo ya elimu ya juu. Nimeangalia hotuba ya Waziri anasema kwa mwakani wanategemea kutoa ruzuku kwa wanafunzi kama 124,243 hata wanaoomba mwaka huu ni wengi zaidi ya hao. Inawezekana Serikali haifanyi tathmini ya kutosha kuanzia sekondari, vyuoni kujua idadi ya wanafunzi wanaohitaji kupata ruzuku kwa ajili ya elimu. Tumekubaliana kwamba kila Mtanzania awe maskini awe tajiri, mtoto wa maskini asome wa tajiri asome. Kama wengi hatuwapatii mikopo wanapataje uwezo wa kusoma mpaka kufika vyuo vikuu na hao ni Marais watarajiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe wanafanya tathmini ya kutosha mwakani wawe na uhakika kwamba watoto kadhaa wanakwenda kupata mikopo na wapate mikopo yao kwa ukamilifu. Mtoto wa maskini unampa asilimia 10 au 20 haimsaidii kitu, anaishi maisha magumu kweli shuleni, wanaishi kwa kula mihogo na magimbi. Tunaomba itengwe fedha ya kutosha kuendana na mahitaji ya watoto maskini ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine hakuna mikakati mizuri ya kusimamia…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Hakuna mikakati mizuri ya kukusanya marejesho ya fedha za mikopo. Mimi nilisoma kwa kutumia mkopo wa Serikali, nimelipa miaka mitano iliyopita na nimekamilisha, juzi mwezi Agosti napata barua nadaiwa. Hii ikanipa picha kabisa kwamba hakuna mikakati ya kufuatilia mikopo, kama mtu amelipa miaka mitano iliyopita leo unampa barua anadaiwa, it seems kwamba hafuatilii mikopo inavyotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.