Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Masasi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kusema kwa kifupi ili nitoe mchango wangu kwenye mapendekezo ya mpango. Kwanza kabisa tuipongeze Serikali kwa sababu kilicholetwa hapa ni mapendekezo na kama tukitoa mapendekezo mazuri yatafanya mpango wetu uwe bora zaidi kwa ajili ya bajeti ya mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumza katika maeneo mawili; kwanza nitazungumzia suala la kilimo, katika kuzungumzia suala la kilimo nitajikita kwenye miradi ya kimkakati. Katika ukurasa wa 43 tumeelezwa kwamba mradi namba saba utakuwa ni kuimarisha kilimo cha mazao ya chakula na malighafi nakadhalika. Mimi ninaomba niishauri Serikali eneo hili lisomeke kuimarisha ushirika na kilimo, tusiache ushirika, nikiangalia mpango huu sioni namna unavyozungumzia kwa kina suala la ushirika. Katika kipindi kifupi na uzoefu tulioupata wa kuwatetea wananchi katika majimbo yetu tunaona kwa kiwango kikubwa kabisa wakulima wanategemea ushirika, lakini ushirika lazima uimarishwe na usimamiwe vizuri ili kusudi wakulima wetu waweze kupata tija ya mazao wanayolima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa kusimamia vema suala la kilimo, mauzo na manunuzi ya zao la korosho kwa msimu wa mwaka huu, hili ni jambo kubwa kwa sababu bei ya korosho imepanda lakini bado kuna changamoto za hapa na pale ambazo kimsingi tunapenda Serikali iziangalie kwa kina. Nitazisema kwa kifupi, jambo la kwanza katika msimu wa korosho uliopita wananchi wa Mikoa ya Kusini wamepata shida kubwa baada ya vyama vya msingi kukata fedha kwa wakulima wetu. Fedha hizi ni nyingi na tunaomba Serikali ichukue hatua ya haraka ili wakulima walipwe fedha zao ambazo zilikuwa zimekatwa katika msimu uliopita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa ripoti iliyoandaliwa na TAKUKURU inaonyesha kwamba takribani shilingi bilioni 30 hazijulikani zilipokwenda, lakini bodi ya korosho imeeleza takribani shilingi bilioni 11 hazijulikani zilipokwenda katika Mikoa ya Kusini. Cha kushangaza bado wale wale waliohusika na wizi wa namna hii wanaendelea tena kusimamia mfumo wa mwaka huu. Wakulima wanaendelea kuuza korosho zao, lakini jicho lao lipo kwa Serikali ni namna gani watu hawa watachukuliwa hatua ili fedha zao zirudishwe na hatua zichukuliwe kwa ajili ya ubadhilifu mkubwa uliofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala lingine la msingi ambalo linapaswa kuangaliwa katika ushirika, katika msimu wa mwaka huu mazao mchanganyiko yameuzwa kwa bei holela mno. Tunaiomba sasa Serikali ije na mpango madhubuti wa kuona namna gani mazao mchanganyiko kama vile mbaazi, ufuta, choroko zitauzwa kwa bei inayofaa na kwa utaratibu unaoeleweka ili wakulima wetu waweze kupata manufaa makubwa, tunaiomba Serikali ilisimamie jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi ninapochangia katika eneo la elimu nimekuwa nikisema jambo ambalo na leo nitalisema, nina imani Serikali yangu sikivu italisikia jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoiangalia elimu tunapaswa kuiangalia elimu kwa jicho pana sana tusiiangalie elimu kwa mtazamo wa elimu rasmi peke yake. Nimekuwa nikilisema hili mara nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia utaratibu wenyewe wote wa kuendesha elimu rasmi uliowekwa katika mpango wetu unaonesha wazi kabisa kuna kundi kubwa la watu tunaowaacha, ambao kwa msingi huo hawatapata elimu kwa muda mrefu sana na baadaye tutakuwa na kundi kubwa la watu ambao hawajaelimika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia sensa ya watu ya mwaka 2012 tunaona kwamba takribani watu wazima milioni 5.5 hawawezi kusoma na kuandika. Lakini pamoja na hilo tukiangalia tena idadi ya watu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja.