Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Moshi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, hii na namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na kuweza kuchangia katika hoja hizi za Kamati hizi mbili za PAC na LAAC.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitajikita kwenye Kamati ya Serikali za Mitaa na ninaunga mkono hoja zote ambazo zimeibuliwa na Kamati ya LAAC kwamba ni hoja za msingi zinazoonyesha baadhi ya matatizo ambayo yapo kwenye utendaji wa Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nilikuwa naomba pia mindset za Wabunge zibadilike kidogo. The way tunavyokwenda tunataka kuipeleka Serikali inapotaka kwa mtazamo wangu. Lengo la Serikali ni kuua Serikali za Mitaa, ndilo lengo la Serikali. Tunapojaribu kwenda tunataka kuwathibitishia kwamba Halmashari hazina uwezo wa kutimiza wajibu wake jambo ambalo si la kweli kabisa. Halmashauri zetu zina uwezo wa kutimiza wajibu wake. Kama tutarudi nyuma, reform iliyofanyika mwaka 1998 mpaka 2008 ilikuwa ina lengo la kuzifanya Halmashauri ziwe na uwezo wa kujitegemea zaidi jambo ambalo Serikali ya Awamu ya Tano hailitaki kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja za Kamati zinasema Halmashauri hazina uwezo wa kukusanya fedha vizuri, zinakusanya kutoka wapi? Vyanzo muhimu vya mapato vimechukuliwa na Serikali Kuu. Sasa Halmashauri zinakusanya kutoka wapi? Mimi naamini bado Serikali ya Awamu ya Tano haina dhamira ya dhati ya kuzisaidia Halmashauri, ina dhamira ya kupora madaraka ya wananchi kuyarudisha kwenye central government. Mimi ndiyo ninachokiona katika mawazo yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi naomba, la kwanza kubwa kuliko lote Wabunge wailazimishe Serikali itambue wajibu wa Serikali za Mitaa na dhamira ya kuanzishwa kwa Serikali za mitaa za kupeleka madaraka kwa wananchi.
Tukifanikiwa kuifahamu hiyo dhana vizuri, na nimuombe Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI awaite Wenyeviti wa Halmashauri na Mameya wakae na Wabunge, kila mmoja azungumze matatizo ya Halmashauri ili Wabunge watambue vizuri matatizo ya Halmashuri ili wakijadili hapa ndani waelewe vizuri kwamba Halmashuri zina matatizo gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu inawezekana hata sisi baadhi ya Wabunge hatufahamu vizuri matatizo ya Halmashauri ndiyo maana tunapelekea kuzilaumu Halmashauri kama vile wao ni wakosaji kuliko Serikali Kuu. Kwa hili la kwanza nilikuwa naomba kama Waziri mwenye dhamana anaona inafaa na itampendeza basi afanye hivyo kwa manufaa na malengo mazima ya kusaidia Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunazungumzia habari ya Wakurugenzi. Ukizungumzia Wizara nyingi kama Wizara ya Ujenzi utasikia wanakuambia tunataka tupate ma-CEO wazuri watakaoimarisha shirika la ndege, watakaoimarisha bandari, wengine mpaka tumewatoa nje. Lakini ni maajabu kwamba Wakurugenzi tunawachukua kutokana na itikadi zao za kisiasa tunawapeleka kwenye Halmashauri, kitu ambacho ni contrary kabisa na dhana ya uboreshwaji wa Serikali za mitaa tuliofanya 1998 mpaka 2008. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la uboreshwaji ni kwamba Wakurugenzi watafutwe watu wenye uwezo na ndiyo maana wakatakwa wasiusike na mambo ya kisiasa. Lakini leo Mheshimiwa Waziri wa Habari anatuambia kwamba Serikali imepeleka watu wa kutekeleza ajenda, watu wa kutekeleza ajenda ni Wakuu wa Wilaya. Watu wa kutekeleza ajenda ni Wakuu wa Mikoa, watu wa kutekeleza ajenda si Wakurugenzi wala Makatibu Tawala.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unapopeleka hawa watu wa kutekeleza ajenda Wakurugenzi ni nani atakayesaidia Halmashauri zifanye kazi? Unapopeleka mtu kwa sababu unamfahamu kwa uzuri, haiba yake kwa namna anavyovyaa au kwa sababu ni rafiki yako, utafanyaje hizo Halmashauri zifanye kazi? Kila siku Taarifa za Kamati zitakuwa na madudu yasiyoisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mmeona mwaka 2013/2014 kulikuwa na taarifa za hati safi za Halmashauri zaidi ya 133, 2014/2015 zaidi ya asilimia 68 ya Halmashauri zina hati chafu, ni kwa sababu gani, kwa sababu mmepeleka watu gani wenye uwezo wa kusimamia hizo Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo rai yangu kwa Serikali kama tunataka kuisaidia nchi hii lazima tuzisaidie Serikali za Mitaa. Kama tunataka kuua nchi hii tubaki na kauli na maneno yasiyoisha ya kisiasa tuue Serikali za Mitaa, ndio mtazamo wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tufike mahali ambapo tunawachagua Wakurugenzi kwa vigezo. Kama ni lazima sana tubadilishe Sheria Namba 7 na Namba 8 hapa ili tupeleke Wakurugenzi ambao wamechaguliwa kwa vigezo, si Wakurugenzi wanaopelekwa kwa sababu ya kujuana. Ukiangalia wakurugenzi waliopelekwa katika Halmashauri leo kuna watu wanaowatetea hapa. Kuna Wakuu wa Idara wenye uwezo kabisa lakini hawakuchaguliwa kuwa Wakurugenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninajua ni mamlaka ya Rais na mimi sitaki kubishana na mamlaka ya Rais lakini Rais ashauriwe vizuri. Anachagua akina nani wa kwenda kwenye Halmashauri? Leo mnazungumzia habari ya ubovu wa mwaka 2014/2015 sasa mtaona madudu mwaka wa 2016/2017, ndio mtakaoona madudu kwa watu mliowapeleka Halmashauri. Naomba hilo suala lichukuliwe katika uzito wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna suala la Halmashuri, kama nilivyosema kwamba mnasema halikusanyi vyanzo vya mapato. Tumekuja kwenye Bunge la Bajeti hapa mmechukua chanzo muhimu sana cha Halmashauri cha kodi ya majengo na mmetudanganya hapa ndani ya Bunge kwamba chanzo kile mmeshakikusanya mtakuwa mnakusanya kama vile mnavyokusanya asilimia 30 ya land rent na mtarejesha. Tunapozungumza leo hakuna shilingi moja imerejeshwa, Halmsahauri zinafanyaje kazi? Mtakuja kuzilaumu kila siku kwenye Taarifa za LAAC na LAAC yenyewe ndiyo hiyo hata fedha hamuipi, hamumpi Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Mahesabu ya Serikali fedha kwa sababu hamtaki Halmashauri zifanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba vyanzo ambavyo ni vya lazima, kwa sasa hivi kuna mpango kwa mujibu wa sheria tuliyopitisha, inawezekana hata mkachukua service levy katika Halmashauri, Halmashauri zitajiendesha na nini? Kwa hiyo naomba vyanzo vya Halmashauri viachwe, halafu tuwapime Wakurugenzi na Watendaji wa Halmashauri kwa uwezo wao. Tuwaongezee manpower, tuwaongezee namna ya kukusanya vizuri, TRA hawana uwezo wa kukusanya mapato yote katika nchi hii kama mnavyotaka kuwapa hiyo burden ambayo hawaiwezi. Mapato ya bandari hawawezi kukusanya, mapato ya utalii hawawezi kukusanya, mnataka kuwaongezea mapato ya Halmashauri ya sababu gani? Nilikuwa naomba Serikali iliangalie hilo kwa makini sana kama mnataka kuzilaumu Halmashauri kwamba hazina uwezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za miradi ya maendeleo haziendi, hazipo. Angalau kule nyuma tulikuwa tunapata asilimia nane, asilimia tano, leo hazipo mpaka tunavyozungumza karibu nusu ya kwanza inakwisha, hakuna fedha za mradi wa maendeleo. Leo kuna hoja yetu ya Kamati inasema miradi mingine inachukua muda kukamilika, itakamilikaje kwa muda kama fedha haziendi? Miradi inakamilikaje kwa muda wakati fedha hampeleki? Miradi mingine mingi inategemea fedha za Serikali kuu, haziendi! Itakamilikaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna hoja ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwamba hati nyingi chafu zimesababishwa na Halmashauri kutokuwa na taarifa sahihi ya mali zake iliyonazo.
Sasa mimi nashauri Serikali na nakushauri Mheshimiwa Waziri, zisukume Halmashauri zote zitengeneze database, zifahamu wapi zinakusanya mapato, zifahamu mali zake iliyonazo (inventory) zake ili hiyo hoja ya ukaguzi isijirudie tena. Na ili zifanye hivyo ni lazima zitenge fedha ya kutosha kwenye bajeti katika kitengo cha takwimu. Bila ya kutenga fedha za kutosha katika kitengo hawatafanikiwa, hizi hoja za ukaguzi zitaendelea na bado Halmashauri zitapata hati chafu, zenye mashaka ambazo sio za lazima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la kukaimu, kwamba ni mojawapo ya sababu ambazo zinazifanya Halmashauri zisifanye vizuri. Kamati imeonesha kwamba Serikali inachelewa kupeleka permanent employer’s katika Halmashauri, hilo ni tatizo la kwanza ambalo Serikali inatakiwa ikabiliane nalo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, Wakurugenzi wetu tunaowachagua hawakai maofisini kufanya kazi zao, wanakaimisha nafasi zao kila siku. Mkurugenzi anakaimisha nafasi yake kikao cha Kamati ya Fedha hayupo, yupo kwenye Kamati ya Siasa ya CCM anakuwa anapeleka taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, sasa utafanyaje kazi? Mkurugenzi hakai. Leo ameitwa na Mkuu wa Mkoa asubuhi, Mkurugenzi anaripoti kwa Mkuu wa Mkoa asubuhi, kwa Mkuu wa Wilaya jioni. Halafu hawezi kukaa kwenye Halmashauri, atafanyaje kazi zake?
Sasa matokeo yake sio tu kwamba kukaimisha kwa maana hiyo ya kwamba Serikali haijapeleka hao waajiriwa wa kudumu lakini hata Wakurugenzi wenyewe hawakai kwenye Halmashauri zao kufanya wajibu wao. Matokeo yake Mkurugenzi muda wote anapata taarifa zake za utekelezaji kupitia kwa watu wa kukaimu tu, kwa hiyo hapati taarifa ambazo ni sahihi, hapati namna ya kupambana na madiwani wake ili ajue namna ambavyo anaweka madiwani wake sawasawa ili wapeleke Halmashauri mbele. (Makofi)
Kwa hiyo ni lazima utoe agizo, Wakurugenzi wasimamie vikao vyote wanavyovisimamia katika Halmashauri unless kuwe na strong reason. Lakini kila Mkurugenzi kikao cha Baraza anakuwa yeye, kikao cha Kamati ya Fedha anakuwa yeye, kikao cha Afya na Uchumi anakuwa yeye, kikao cha Mipango Miji anakuwa yeye ili apate taarifa halisi kama Katibu halisi wa Baraza. Otherwise kila siku watakuwa wanaletewa taarifa za uongo na hata kujibu kwenye Kamati hawawezi kujibu wanapoitwa kwenye vikao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka nizungumzie suala la internal auditors ambalo limezungumzwa kama tatizo pia kwenye Taarifa ya Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, internal auditors tulionao ni kweli kwamba wanafanya kazi chini ya Mkurugenzi, na kwa misingi hiyo wataripoti according kwa matakwa ya Mkurugenzi kwa sababu hawana fedha wakipewa fedha kidogo wataripoti kadri Mkurugenzi anavyotaka. Sasa usipopeleka Mkurugenzi ambaye ni mahiri ukapeleka Mkurugenzi mla rushwa, Mkurugenzi asiye na mtazamo, asiyefahamu kwamba Halmashauri ni sehemu yake kwa vyovyote vile internal auditors hawezi kumsaidia Mkurugenzi na Halmashauri lazima ifanye vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati mwingine internal auditors wanaweza wakawa wanasaidiana kuharibu Halmashauri kwa sababu wakati mwingine wanaweza wakatumiwa vibaya na hata madiwani ambao hamtaki kuwapa mafunzo. Mmeamua sasa hivi kwamba Madiwani hawapati mafunzo, Diwani hawezi kwenda hata kwenye Halmashauri nyingine kujifunza mpaka Mkuu wa Mkoa atake.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hizi Halmashauri mnapozibana namna hii, zinapokuwa na intervention ya Mkoa namna hii, Wakuu wa Mikoa wanaingilia Halmashauri, Wakuu wa Wilaya wanaingilia Halmashauri, kila mmoja na kauli yake, mnapelekaje Halmashauri? Halmashauri kwa mujibu wa Katiba yetu ni Serikali ambayo ni ndani ya Serikali Kuu, na zina utaratibu wake. Wajibu wa Mkoa ni kutoa ushauri, wajibu wa Wilaya ni kutoa ushauri, si kuziingilia Halmashauri. Leo Wakuu wa Mikoa, Wilaya wanaziingilia Halmashauri kama ni vyombo vyao vya pale ofisini, kama ni Idara katika ofisi zao. Zinawezaje zikafanya kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunalalamika hapa bure tu kuhusu Halmashauri. Wanaoua Halmashauri hapa ni Serikali Kuu, anayeua ni Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa. (Makofi)
Kwa hiyo kama tunataka kuzisaidia Halmashauri, Waziri mwenye dhamana ya Serikali za mitaa asaidiwe, aelimishwe, zifanyeni Halmashauri zilizo na creativity, watu wawe wabunifu, watu wawe na uwezo wa kujituma, watu waweze na kubuni mikakati yao halafu wasaidieni. Saidieni Halmashauri katika dhana ya PPP zifanye kazi vizuri na hizi hoja za ukaguzi yatapungua sana. Lakini bila kuzisaidia hizi hoja za ukaguzi yatakuja kila siku mpaka mtachanganyikiwa hapa Bungeni tu. Wabunge mtawalaumu Madiwani Bure, mtawalaumu Wakurugenzi bure lakini tatizo liko kwenye central government, ndio mtazamo wangu na mimi nashauri Serikali ilichukue katika uzito wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama muda wangu haujaisha nilikuwa naomba sana tuyatilie uzito mawazo ya wenzetu kwamba CAG apewe fedha ya kutosha, Kamati ya LAAC ipewe fedha ya kutosha, iende kwenye Halmashauri ifanye ukaguzi wa kutosha, itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya PAC ipewe pia fedha za kutosha. Tuzisaidieni hizi Kamati kama overside committees zetu ziweze kutusaidia kujua Halmashauri zilivyo na kujua na sisi tulivyo ili tusaidiane katika kuhakikisha kwamba nchi hii inakwenda mbele. Bila kusaidiana sisi Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, mtakaa mkitoa maagizo; ni kweli kabisa kwa mujibu wa taarifa ya Kamati Halmashauri nyingi zimekuwa zikibadilisha matumizi yake kutokana na maelekezo ya Serikali Kuu, kutokana na maelekezo ya Mkuu wa Mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wana mpango wao wanaambiwa kuanzia leo mnajenga maabara, fedha zinatoka wapi? Hawaambiwi. Lazima Mkurugenzi afanye hivyo maana ni muoga atafanye? Asipofanya vizuri atatumbuliwa. Madawati yameagizwa anafanya nini? Asipofanya hivyo anatumbuliwa, hata akifanya akija kwenye hoja ya ukaguzi inampiga, anatumbuliwa. Wakurugenzi hawana hata mahali pa kupumulia wakati mwingine kwasababu mnawaumiza. Wakuu wa Idara hawana mahali pa kupumulia, ni waoga kwa sababu wanakwenda pale wakitishwa na mambo ya itikadi. Tuacheni mambo ya itikadi tuamueni kupeleka hili Taifa mbele ili tuweze kufanikiwa katika mambo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie tena kuipongeza Kamati, imefanya kazi yake vizuri na nadhani tuna umuhimu wa kuchukulia uzito matatizo waliyoyaona lakini Serikali itimize wajibu wake ili twende mbele. Ahsante sana kwa kunisikiliza.