Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini naomba niseme ninaitwa Azza Hillal Hamad.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kusimama ndani ya ukumbi wako kuweza kuchangia Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe kwa ruhusa yako, nitumie fursa hii kuwapa pole ndugu, jamaa na marafiki ambao wameondokewa na wapendwa wao katika ajali ya gari ya aina ya Noah iliyotokea tarehe 6 Novemba, siku ya Jumapili katka Mji mdogo wa Tinde poleni sana Mwenyezi Mungu awape subira niko pamoja na ninyi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kuchangia katika Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa. Ukiangalia katika ukurasa wa 40 wa Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa mfuko wa wanawake na vijana asilimia kumi katika Halmashauri ambazo zimekafuliwa, tumekagua Halmashauri 164 katika Halmashauri 164, Halmashauri 112 hazikupeleka fedha ipasavyo katika mfuko wa wanawake na vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri 112 halmashauri 6 ziliagizwa na Kamati kuandika barua ya kuji-commit kulipa fedha hizo kabla ya tarehe 30 Septemba. Cha kusikitisha Halmashauri hizo mpaka hivi ninavyoongea au mpaka Kamati inaleta taarifa ndani ya Bunge hazijaleta barua hizo. Halmashauri hizo ni Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Halmashauri ya Jiji la Tanga na Halmashauri ya Ruangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri hizo zilizokaguliwa kuna Halmashauri ambazo hazikuchangia kabisa hata shilingi moja kwa mwaka 2014/2015 ziko ukurasa wa 43. Halmashauri hizo ni Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Halmashari ya Tunduru, Halmashauri ya Mpanda, Halmashauri ya Tunduma, Halmashauri ya Ludewa, Sengerema na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfuko wa wanawake na vijana umekuwa kama ni hisani kwa halmashauri. Watu wanafanya pale ambapo wanaona kwamba inafaa na Wakurugenzi wengi katika Kamati wamekuwa wakijibu kwamba wanatumia fedha hizi kwa sababu ya maagizo yanayotoka juu. Wengi wanasema wanatengeneza madawati, wamejengea maabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini fedha hizi zimekuwa kama shamba la bibi? Ni kwa sababu tu hakuna sheria ambayo ipo katika Halmashauri zetu inayowaelekeza Wakurugenzi kupeleka fedha hizi kwa wanawake na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukilisema kwa muda mrefu hili ni tatizo sugu kwa Halmashauri. Wanafanya hivi kwa sababu tu wanawake hawa na vijana hawawezi kwenda kwenye Halmashauri kudai haki yao kwa sababu haipo kisheria. Lakini kama Halmashauri inafikia kupewa maagizo na Kamati, kuandika barua ndani ya Kamati na Halmashauri inakaidi maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba Halmashauri hizi haziheshimu wala hazitambui mamlaka zilizopo juu kwa maana ya kwamba waraka huu wa kupeleka mfuko wa akina mama na vijana asilimia kumi ulipelekwa kutoka TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe na niishauri Serikali kwa kuwa Halmashauri zimekuwa hazipeleki fedha hizi, ni vyema basi Serikali ikaleta Muswada wa Sheria wa Mfuko wa Wanawake na Vijana ili wanawake na vijana hawa ambao wako kule na wanakosa nafasi ya kupata mikopo katika mabenki kwa sababu ya masharti yaliyopo ya mabenki waweze kukopeshwa fedha hizi kama haki yao ya msingi. Vinginevyo tutabaki kulalamika lakini fedha hizi hawatazipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaishauri Serikali mlete muswada wa sheria kwa ajili ya mfuko wa wanawake na vijana ili tuweze kuwakomboa wanawake na vijana waliopo kule majimboni kwetu. Katika taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Halmashauri pia ina tatizo sugu. Tatizo hili ni kwamba asilimia 20 ya vyanzo vya mapato zilivyofutwa Halmashauri haipeleki kwenye mitaa na vijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia ukurasa wa 45 wa taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa utaona kuna Halmashauri ambazo tumezitolea mfano hazijapeleka kwa miaka mitatu mfululizo fedha za vijiji na mitaa. Halmashauri hizo ni Halmashuri ya Kilwa, Halmashauri ya Ngara, Halmashauri ya Hai, Halmashauri ya Rombo, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiwauliza hata fedha hizi kisingizio ni hicho hicho; maagizo kutoka juu. Sasa najiuliza, kwa Halmashauri ambazo wanaweza kupeleka fedha hivi wao wanafanya nini kutengeneza madawati? Kama siyo kwamba ni uongozi mbovu uliopo katika Halmashauri hizi wanashindwa kukaa na kuamua watatengeneza vipi madawati wanakwenda kuchukuwa haki ambayo siyo ya kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatutaondoa tatizo la rushwa katika ofisi za Serikali za Mitaa katika ofisi za vijiji kwa sababu ofisi za Serikali za mitaa na ofisi za vijiji hawana nyenzo za kufanyia kazi. Ile haki yao ambayo wanatakiwa kuipata hawaipati; unakuta Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji na Mtaa, hana hata fedha ya kununua karatasi, unategemea nini kwa mwananchi aliyekwenda ana shida yake? Kama siyo kwamba ataombwa fedha ili aweze kukamilishiwa shida iliyompeleka ofisini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali badala ya fedha hizi kuzipeleka kwenye Halmashauri zetu na Halmashauri zinafanya ni shamba la bibi basi fedha hizi zipelekwe moja kwa moja katika vijiji na mitaa ziweze kuwafikia walengwa vinginevyo kila siku tutapiga kelele Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Mitaa hawawezi kupata haki yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka haraka nikitoka hapo niende, suala la Wakuu wa Idara na Vitengo kukaimu. Halmashauri nyingi zimekuwa zikikaimiwa nafasi hizi lakini cha kusikitisha wengine makuwa wakikaimu kwa muda mrefu na matokeo yake nafasi ile anakuja kupewa mtu mwingine, yeye aliyekaimu hapewi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru naunga mkono hoja.